24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hizi ndizo sababu shambulio la kigaidi Sri Lanka?

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

TUKIO la mashambulio ya bomu lililotokea wakati wa Sikukuu ya Pasaka nchini Sri Lanka na kuua watu 290, huku wengine 500 wakijeruhiwa, imeendelea kuwa habari iliyoshika nafasi kubwa katika vyombo vya habari duniani.

Makanisa matatu yalishambuliwa wakati wa Ibada ya Pasaka, huku ikiwa hivyo pia kwa hoteli tatu za kitalii zilizoko katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, ambapo hata hivyo Marekani imevipa onyo vyombo vya usalama vya Sri Lanka, ikisema huenda bado magaidi wakatekeleza mashambulio. 

“Magaidi wanaweza kushambulia wakiwa wametoa onyo dogo au bila taarifa yoyote,” ilisomeka taarifa hiyo.

Huku tukio hilo likiendelea kulaaniwa duniani kote, wengi wakijiuliza sababu ya kutekelezwa kwa shambulio hilo, ukweli ni kwamba katika miaka ya hivi karibuni, Sri Lanka imejikuta ikikumbwa na mashabulio ya aina hiyo.

Kwa wafuatiliaji wa siasa za kimataifa, watakiri kuwa huo ni mwendelezo wa matukio ya kujitoa mhanga, ambayo hayajaliacha salama taifa hilo tangu zilipomalizika vita za wenyewe kwa wenyewe.

Je, nini sababu ya shambulio la Pasaka na mengine yaliyoitikisa Sri Lanka katika miaka ya hivi karibuni? Hilo ndilo swali pasua kichwa kwa sasa juu ya tukio hilo.

Licha ya kwamba hakuna kundi lililojitaja kuhusika na shambulio la safari hii, si rahisi kuepuka kulihusisha tukio hilo na jamii ya Kiislam.

Itakumbukwa kuwa wakati wa vita za wenyewe kwa wenyewe miaka mingi iliyopita, waumini wa dini hiyo walikuwa wahanga wakubwa, wakishikiliwa, wakiteswa na kuuawa na kikundi cha waasi cha Tamil Tiger.

Inafahamika kuwa bado viongozi wa Kiislam nchini humo wamekuwa wakipaza sauti zao kudai kuwa serikali zote zilizofuata baada ya machafuko hayo hazijaweza kuwahakikishia usalama waumini wao.

Msingi wa madai yao ni shambulio la mwanzoni mwa mwaka jana mjini Digana, ambalo lililenga maduka na misikiti ya Waislam, ikielezwa kuwa mtu mmoja alipoteza maisha.

“Baada ya kile kilichotokea Digana, baadhi ya Waislam walipoteza imani yao kwa ulinzi wa Serikali dhidi yao. Baadhi walifikia hata hatua ya kuibua wazo kuwa wanapaswa kujilinda wenyewe,” anasema Makamu wa Rais wa Balaza la Waislam nchini Sri Lanka, Hilmy Ahamed.

Katika hatua nyingine, hakuna namna ya kuepuka ukweli kwamba hiyo imekuwa sababu ya kuibuka kwa makundi kama National Thowheed Jamath (NTJ), ambalo ni la Waislam na mara kadhaa limekuwa likitajwa kuhusika katika mashambulio.

Mbali ya lile dhidi ya waumini wa Dhehebu la Budha, ambalo lililaaniwa vikali nchini humo, pia Msemaji wa Serikali, Rajitha Senaratne, amelinyooshea kidole Kundi la NTJ akisema linaweza kuwa limehusika katika kile kilichotokea Pasaka.

Kuonesha ni kwa kiwango kikubwa kumekuwa na uhasama kati ya serikali na waumini wa Kiislam, hivi sasa kuna presha kubwa kutoka kwa mhubiri anayetokea Mashariki mwa taifa hilo, Zaharan Hashim.

Kupitia mitandao ya kijamii, Hashim amekuwa akiweka video zinazoeneza chuki dhidi ya Wakristo na waumini wa dini zingine nchini Sri Lanka, bahati mbaya ikiwa ni mahubiri yake kufanikiwa kuiteka idadi kubwa ya vijana wa Kiislam.

Hatari zaidi ni kwamba viongozi wa Kiislam wamekuwa wakiweka wazi kuwa vijana wao wengi wanaondoka nchini humo kwenda Syria kujiunga na Kundi la Dola ya Kiislam (IS), wengine wakiwa wameshafariki katika matukio ya kujitoa mhanga.

Wakati hali ikiwa hivyo, huku aliyewahi kuwa Ofisa wa Jeshi, Maj Gen Chandrasiri, akipuuza kwa kusema Waislam wengi wanapingana na matukio hayo, inaibua shaka kuona shambulio la wiki iliyopita liliwalenga Wakristo tu.

Ukiliweka kando hilo la dini, pia kuna shaka kubwa kuwa waliotekeleza shambulio la Pasaka walikuwa na sapoti ya mtandao wa kimataifa.

“Kwa operesheni ya aina hii, unahitaji msaada kutoka nje. Unahitaji fedha, mafunzo na mbinu za kufanya kazi hii,” anasema Gen Chandrasiri na kuongeza: “Huwezi kufanya mwenyewe haya mambo. Huenda kulikuwa na msaada kutoka nje.”

Je, baada ya kuyatesa mataifa mengi kwa mashabulio yake ya mabomu na kuacha vilio, ni zamu ya Sri Lanka kutikiswa na al Qaeda na IS?

Akilizungumzia hilo, Shiral Lakthilaka, ambaye ni Mshauri Mkuu wa Rais wa Sri Lanka, Maithripala Sirisena, alisema: “Kulikuwa na mtandao wa kimataifa, kama isingekuwa hivyo shambulio lisingewezekana.”

“Hatuamini kuwa mashambulio hayo yamefanywa na watu wa hapa peke yao,” alisema Senaratne, kabla ya taarifa ya Ikulu iliyokuja baadaye kusomeka: “Taarifa za kiitelejensia zinaonesha kuwa vikundi vya kigaidi vya kimataifa viko vyuma ya magaidi ya hapa. Hivyo rais ataomba msaada kwa nchi jirani.”

Hata hivyo, wakati hayo yakitajwa, wapo wanaoamini udhaifu wa vyombo vya usalama ulikuwa na nafasi yake katika kutokea kwa shambulio hilo la Pasaka. Inaelezwa kuwa hata kabla ya tukio lenyewe, tayari kulikuwa na meseji nyingi za vitishio juu ya mashambulio.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Ranil Wickremesinghe, ilikuwa hivyo na hata Rais wake, Sirisena, analijua hilo. Kinachoweza kuonekana hapo ni kwamba huenda hakukuwa na jitihada zozote za kufuatilia, yaani viongozi na vyombo vya usalama vilipuuzia, vikiamini ni uzushi tu.

Ipo taarifa pia kwamba hata serikali za Marekani na India ziliipa onyo Sri Lanka juu ya uwezekano wa kutokea kwa hatari, hivyo kutoacha kuzifuatilia meseji za vitisho vya kutekelezwa kwa shambulio.

Ni kwa maana hiyo basi, utakuwa ni uzembe mkubwa kwa vyombo vya usalama, hasa endapo wahusika wa shambulio hilo wanatokea ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles