24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hillary mshindi aliyeshindwa

Hillary Clinton
Hillary Clinton

Na Tobias Nsungwe,

INGAWA Hillary Clinton amekubali kushindwa Uchaguzi Mkuu wa Marekani dhidi ya Donald Trump wa Republican, ukweli unabaki kwamba, katika sura ya kidunia mwanamama huyo ameshinda.

Mama Clinton katika kura za jumla alipata kura 59,814,018, sawa na asilimia 48 dhidi ya kura 59,611,678, sawa na asilimia 47 alizopata Trump. Hata hivyo, Trump amemshinda Hillary baada ya kupata kura za majimbo 276, dhidi ya kura 218 alizopata Hillary.

Mwanamama huyo alimaliza ngwe yake ya karibu miaka 30 katika siasa huku akiacha hotuba yenye hisia kali ya kukubali matokeo. Namnukuu; “Inaumiza na hili litatusumbua kwa muda mrefu”, alisema mama huyo wiki iliyopita, huku akitaka zoezi la kukabidhiana madaraka liende kwa amani.

“Donald Trump atakuwa rais wetu. Nina matumaini atakuwa rais mwenye mafanikio kwa sisi wote Wamarekani,” aliuambia ukumbi uliojaa wafuasi wake waliojaa hamasa, huku wakiwa hawaamini kwamba Clinton anatoa hotuba ya kukubali kushindwa. Aliwataka wafuasi wake kukubali matokeo ya uchaguzi, kwani huo haukuwa mwisho wa mapambano ya kupigania kile wanachoamini.

“Tumeona kwamba nchi yetu imegawanyika sana kuliko tulivyodhania. Wakati wote naamini na nitaendelea kuamini katika ukuu wa Amerika. Kwa kuzingatia hilo, sisi sote lazima tukubali matokeo ya uchaguzi huu. Sote tumuunge mkono Trump na kumpa nafasi ya kutuongoza,” alisema.

Aliyekuwa mgombea mwenza wa Mama Clinton, Tim Kaine, alisema mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Democrat mwaka huu ni ‘mtengenezaji mzuri wa historia’. Mama Clinton anaingia kwenye historia ya Marekani kama ndiye mwanamke wa kwanza kuteuliwa na chama kikubwa kugombea urais wa nchi hiyo.

Anaingia katika historia kama mwanamke wa kwanza ‘kushinda’ urais walau kwa kura za pamoja (popular vote). Mafanikio aliyofikia Mama Clinton yanaweka misingi inayoonyesha kuwa ipo siku moja taifa hilo kubwa litakuja kuongozwa na rais mwanamke.

Katika hotuba yake ya kukubali matokeo, Mama Clinton aliwataka wanawake, hasa wenye umri mdogo kutokatishwa tamaa na matokeo ya uchaguzi mwaka huu.

“Kwa vijana nasema kushindwa kunauma, lakini tafadhali msiache kuamini mnachokipigania. Kwani kuna tija kupigania unachodhani ni sahihi,” alisema, huku akiwasihi wanawake waliokuwa wanamuona kama ni mwanamke wao wa mfano kutokata tamaa.

“Hatukuweza kufikia mafanikio ya juu tuliyoyataka. Bado tuna kazi ngumu mbele. Lakini siku moja mwanamke mmoja miongoni mwetu atafikia mafanikio ya juu. Nawaambia mafanikio hayo yatakuja mapema zaidi kuliko tunavyofikiria sasa,” aliendelea Hillary kutoa hamasa, huku mume wake Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bill Clinton, akimtazama.

Amewataka vijana wa kike kutokatishwa tamaa na kile kilichotokea. Amewataka wazidi kujiona kuwa wana thamani na nguvu na wanastahili kuitumia kila fursa duniani kutimiza ndoto zao.

Mafanikio ya Hillary japo hajawa rais wa Marekani yanaamsha ari ya mapambano ya kumkomboa mwanamke duniani kote.

Hapa Tanzania kuna wanawake wamekuwa wakipanda ngazi ya siasa kwa kasi kubwa. Hivi sasa wapo wabunge wengi zaidi wanawake wanaowakilisha majimbo. Mwaka 2006 nchi ilipata waziri wa kwanza wa fedha mwanamke, Zakia Meghji. Hii ni nafasi kubwa sana. Mama huyu alishika wadhifa huo hadi mwaka 2008. Baadaye Saada Mkuya akawa mwanamke wa pili kushika nafasi hiyo mwaka 2015.

Tanzania imepata kuwa na Spika wa Bunge mwanamke, Anna Makinda (68). Mama huyu amekuwapo kwenye siasa za ushindani kwa miaka 40, alishika wadhifa wa uspika kati ya mwaka 2010 na 2015. Kabla ya hapo alikuwa Naibu Spika na amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na waziri katika wizara kadhaa.

Februari mwaka 2007, nchi ilipata heshima kubwa katika siasa za kimataifa baada ya Dk. Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Msomi huyo pia amewahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Sasa tunaye Naibu Spika mwanamke kijana, Dk. Tulia Ackson (40), ambaye nyota yake inang’ara.

Tangu wanawake waanze kupigania nafasi kubwa katika uongozi wa juu, pengine mwaka jana ndio ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa wanaharakati wa maendeleo ya wanawake.

Mama Samia Suluhu Hassan (55) aliteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea mwenza wa Dk John Magufuli. Hatimaye historia iliandikwa pale alipoapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza mwanamke Novemba 5, mwaka jana, baada ya CCM kushinda uchaguzi mkuu.

Katika Bara la Afrika jirani zetu Malawi walipata Rais mwanamke, Joyce Banda, ambaye alidumu toka Aprili 7, 2012 hadi Mei 31, 2014, aliposhindwa katika uchaguzi mkuu dhidi ya Rais wa sasa, Peter Mutharika.

Hivi sasa Liberia inatawaliwa na rais mwanamke, Ellen Johnson-Sirleaf, aliyechukua madaraka hayo toka Januari 16, 2006. Ndiye rais wa kwanza mwanamke katika Bara la Afrika. Afrika imepata kuwa na viongozi wengine wanawake kama Catherine Samba-Panza wa Afrika ya Kati na Waziri Mkuu wa Senegal, Aminata Toure.

Bara la Ulaya pia limetoa wanawake wenye nguvu kama Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May. Kuna viongozi wengine wanawake, kama Dalia Grybauskaite wa Lithunia, Atifete Jahjaga wa Kosovo, Kolinda Grabar-Kitarovic wa Crotia na Tarja Halonen wa Finland.

Asia ni maarufu kwa kuwa na viongozi wanawake.

Kati ya mwishoni mwa miaka ya 1970 na 1984, India ilikuwa na Waziri Mkuu mwanamke, Indira Ghandi. Huyu ni mmoja wa wanawake waliokuwa na nguvu wakati wa vita baridi ya dunia katika ya nchi za Magharibi na Mashariki. Waziri Mkuu wa Bangladesh ni mwanamke, Sheikh Hasina Wajed. Aliingia madarakani mwaka 2009.

Kwa sasa Rais wa Korea Kusini ni mwanamama Park Geun-hye (64), aliyeingia madarakani baada ya kushinda urais mwaka 2013.

Wapo wanawake ambao wameshika nafasi ambazo zina ushawishi mkubwa duniani, ingawa si za uendeshaji wa Serikali moja kwa moja. Hawa ni pamoja na Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza aliyetawazwa kushika wadhifa huo mnamo Februari 6, 1952.

Mwanamke mwingine katika nafasi hiyo ni Malkia Margethe wa pili wa Denmark, aliyeshika nafasi hiyo tangu mwaka 1972, Gavana Mkuu wa Kisiwa cha Lucia, Dame Pearltte na Gavana Mkuu wa Australia, Quentin Bryce.

Baadhi ya Wamarekani wamesikitishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu. Wengi walitaka kuweka historia ya kuona rais mwanamke akipatikana katika kizazi chao. Lakini kama alivyosema Hillary, wanawake wa Marekani wasikate tamaa, ipo siku Marekani itapata rais mwanamke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles