25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Highway ni chachu ya mapinduzi ya kilimo, uvuvi

YOHANA PAUL – MWANZA

MAPEMA mwezi huu, Mamlaka ya Huduma za Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitambulisha mradi wa kuboresha huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Victoria uitwao High Impact Weather Lake Systems (Highway), ambao unatekelezwa katika wilaya za Sengerema mkoani Mwanza na Muleba mkoani Kagera kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).

Mradi huo unaotarajiwa kufanya kazi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani utawalenga zaidi wavuvi na wakulima ili kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa kuendana na taarifa za hali ya hewa za uhakika kutoka TMA.

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi anasema umekusudia kuboresha huduma za hali ya hewa na unatekelezwa kwenye nchi za Ziwa Victoria ikiwemo Tanzania.

Anasema lengo hasa ni kupunguza majanga na ajali majini kwa wavuvi ambao mara nyingi wamekuwa wakifanya kazi zao bila kujua mwenendo wa hali ya hewa ziwani na kupelekea wengi wao kupoteza maisha pale tafrani inapotokea.

Kijazi anasema mbali na mradi kuwanufaisha wavuvi, pia utakuwa na msaada kwa wakulima wote Kanda ya Ziwa kwani wataweza kupokea elimu ya hali ya hewa pamoja na utabiri mapema na kutumia utabiri na elimu hiyo kufanya uchaguzi sahihi wa mazao ya chakula na biashara.

Anasema mabadiliko ya hali ya hewa kwa karne hii yamekuwa na nafasi kubwa katika kutambulisha aina ya shughuli za eneo husika hivyo iwapo wananchi watapata uelewa wa taarifa za hali ya hewa itawapatia uhakika wananchi nini na muda gani wa kulima au kufanya uvuvi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, anasema ujio wa mradi huo Ziwa Victoria ni jambo lenye tija kwa wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani hasa wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi.

Mongella anasema mradi una manufaa makubwa kwa mkoa kwani ikizangatiwa kuwa nusu ya wakazi wa Mwanza na maeneo ya mikoa ya jirani wanategemea uvuvi kama chanzo chao muhimu cha mapato.

Anaeleza kuwa Mwanza kama kitovu cha uzalishaji wa samaki nchini, itafaidika na mradi huo na huenda ukaongeza mara tatu zaidi uzalishaji wa samaki viwandani na kuchangia kukuza  uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Mongella anawaomba viongozi wa TMA kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa chini ndani ya jamii katika sekta za kilimo na uvuvi ili elimu ya hali ya hewa ifahamike kwa kila mmoja bila kuangalia kiwango chake cha elimu na kuufanya mradi huo kuwa na manufaa chanya zaidi.

Binafsi pia nauangalia mradi huu kama nyenzo mpya katika shughuli za kilimo na uvuvi nchini kwani mafanikio yake katika Kanda ya Ziwa yatakuwa na tija siyo tu kwa mikoa ya eneo hili bali pia kwa mikoa ya jirani na Tanzania kwa ujumla.

Ili malengo ya mradi yafikiwe ni lazima tukubali kuwekeza zaidi kwenye utekelezaji wa vitendo na sio mipango ya ofisini kwa kufanya hivyo ninaamini mapinduzi katika sekta hizo yatafikiwa bila kikwazo.

Ni wazi kuwa endapo wote wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi watakuwa na uelewa wa mwenendo pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa katika ukanda huu wataweza kuendesha shughuli zao kwa tahadhari na pengine kuepuka kuingia hasara isiyotarajiwa.

Nitoe pongezi kwa DFID kwa kushirikiana na TMA kuandaa mpango kazi utakaowezesha mradi wa Highway kutekelezwa ukanda wa Ziwa Victoria, hii ni ishara tosha kuwa ni wakati sasa kwa Watanzania wanaojishughulisha na shughuli za kilimo, uvuvi na nyinginezo kufanya kazi zao kuendana na teknolojia yenye msaada katika kuongeza uzalishaji wa mazao.

0768864097
[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles