25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Haya yatamtofautisha Tshisekedi na Kabila

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

BAADA ya takribani miaka 60, hatimaye Desemba 30, mwaka jana, ilikuwa siku ya mabadiliko makubwa katika siasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ni siku ambayo kwa mara ya kwanza wananchi ya taifa hilo waliitumia haki yao ya kidemokrasia kusimama kwenye vituo vya kupigia kura kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali, akiwamo rais.

Hatimaye ni mgombea wa chama cha upinzani cha UDPS, Felix Tshisekedi, ndiye aliyeingia Ikulu kukikalia kiti cha aliyekuwa Rais wa DRC kwa miaka 18 kupitia Chama cha PPRD, Joseph Kabila, akitajwa kujikusanyia asilimia 38.6 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani wake wa karibu katika mbio za kukikalia kiti cha Kabila, Martin Fayulu, alipata kura milioni 6.4, huku Emmanuel Ramazani Shadary akiambulia milioni 4.4.

Awali, kulikuwa na upingaji wa matokeo kutoka kwa mpinzani mwenzake, Martin Fayulu, aliyedai Tshisekedi na Rais Kabila walimfanyia ‘figisufigisu’.

Katika kile kinachoshabihiana na hilo, nao uongozi wa Kanisa Katoliki DRC, taasisi yenye nguvu kubwa ya ushawishi katika siasa za nchi hiyo, walionesha kutokubaliana na ushindi wa Tshisekedi, wakisema ulikinzana na matokeo halisi.

Hata hivyo, baada ya mvutano wa siku kadhaa, hatimaye Mahakama ya Kikatiba nchini humo ilikata mzizi wa fitina kwa kutangaza kuwa matokeo hayakuwa na dosari, hivyo Tshisekedi aapishwe.

Aidha, wakosoaji wake wamekuwa wakimuona kuwa ni kibaraka wa Kabila na hata Fayulu alipolalamikia kuchezewa rafu katika matokeo ya uchaguzi mkuu, hakuacha kumnyooshea kidole rais huyo wa zamani.

“Huyo si rais aliyechaguliwa. Ni rais aliyeteuliwa na Kabila,” alisema Fayulu katika mahojiano yake na gazeti la Reuters la Uingereza akimzungumzia Tshisekedi, ambaye Marehemu baba yake, Etienne, alikuwa mpinzani mkubwa wa Kabila.

Hata hivyo, huku hali ikiwa hivyo, wafuatiliaji wa siasa za DRC wanaamini Tshisekedi ana nafasi kubwa ya kuwaaminisha wananchi zaidi ya milioni 80 kuwa yeye si kibaraka wa Kabila bali ameingia Ikulu kuleta mabadiliko ndani ya nchi hiyo yenye changamoto lukuki.

Kwa kuanza, kumaliza machafuko kunaweza kuwa faraja kubwa kwa wananchi wa DRC, kazi ambayo Kabila anaondoka ikiwa imemshinda licha ya juhudi zake za hapa na pale.

Hali tete ya usalama inachangiwa na mapigano kati ya Serikali na vikundi vya waasi, mfano mzuri ukiwa ni yale yanayoendelea Mashariki mwa taifa hilo, ambako kunatajwa kuwa na vikundi visivyopungua 70.

Watu wanaotajwa kufikia10,000 hupoteza maisha kila mwezi kutokana na hilo na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Majanga ya Umoja wa Matifa.

Vilevile, hali ni mbaya zaidi kwa wanawake kwani takwimu zilizopo zinadai kuwa wapatao 200,000 wameshakumbana na vitendo vya udhalilishaji, 40 wakibakwa kila siku.

Umoja wa Mataifa (UN) unaitaja DRC kuwa na watu wasiopungua milioni 2.7 waliokimbia makazi yao na wengine 450,000 walioamua kuvuka mipaka na kwenda nchi jirani.

Haina kificho kwamba hali ilikuwa mbaya zaidi pale Rais Kabila alipoamua kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, kipindi ambacho muda wake wa kukaa madarakani kilikuwa umefikia ukomo.

Historia inaonesha kuwa tangu kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe huko Rwanda mwaka 1994, DRC haijawa shwari. Wanamgambo wa Kabila la Hutu, ambao walikuwa wakipingana na wenzao wa Tutsi ndio walioingia DRC.

Serikali ya DRC iliposhindwa kuvikabili na kuvitokomeza vikundi hivyo, viliweza kujenga ngome inayoendelea kuwatesa wananchi wa DRC hadi leo hii.

Ni kama kuna dalili nzuri ya kukabiliana na changamoto hiyo baada taarifa ya mwishoni mwa wiki iliyopita kudai kuwa waasi 600 kuahidi kuacha vurugu ili kumuunga mkono Tshisekedi.

Kuirejesha DRC katika hali ya utulivu na wananchi wakarudi katika shughuli zao za maendeleo ndicho kinachoweza kupimwa kama mafanikio makubwa ya Tshisekedi. Kwa furaha watakayokuwa nayo Wacongo, haitakuwa rahisi tena kusikiliza wakosoaji wake.

Pili, ni kwa kuhakikisha rasilimali za DRC zinakuwa na tija kwa maisha ya wananchi, tofauti na ilivyo sasa. Kuzitaja kwa uchache, DRC ina utajiri wa rasilimali za dhahabu, almasi, shaba na mafuta lakini kwa bahati mbaya takwimu hazioneshi kuwa zinawanufaisha walio wengi.

Ni kwa sababu nusu ya wanachi wa taifa hilo wanaogelea katika dimbwi la umaskini. Hiyo ni kusema rasilimali hizo zimekuwa zikiyafaidisha mataifa ya Magharibi na wajanja wachache serikalini, huku wananchi wakibaki kuishi maisha ya ‘kuungaunga’.

Nalo hili ni tatizo la kihistoria kwani mataifa ya Kizungu kutegemea utajiri wa DRC ilianza kitambo, ikikumbukwa kuwa wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, asilimia 75 ya shaba zilitoka nchini humo ilikwenda Ulaya kutengeneza risasi.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika karne hii ya 21, sasa mataifa yaliyoendelea yamekuwa wakiyatumia madini  hayo kutengeneza simu janja (smartphones), kompyuta na vito.

Joseph Kabila anatajwa na wakosoaji wake kuwa chanzo cha umaskini unaowatesa Wacongo, wakisema amekuwa akiiba misaada inayotoka nje, ukiiacha ‘skendo’ ya kumilikisha rasimali ya madini kwa watu wake wa karibu.

Iliwahi kuelezwa kuwa Rais huyo na familia yake wana mtandao katika kila sekta ya uchumi wa DRC. Ni kipindi hicho ndipo iliposemekana kuwa wanamiliki ardhi yenye ukubwa wa hekta 71,000.

Ikaripotiwa pia kuwa dada zake wanamiliki hisa katika kampuni za simu, kaka yake ni kigogo wa biashara za madini na ujezi. Kwa pamoja, wakahusishwa na umiliki wa kampuni zaidi ya 80 ndani na nje ya DRC.

Endapo sera na mikakati ya Tshisekedi itafanikisha kumaliza tatizo hilo, wananchi wa DRC wakaanza kuuona umuhimu wa rasilimali zinazowazunguka, huenda akawaziba mdomo wakosoaji wake na hatimaye kuifanya hoja ya kuwa kibaraka wa Kabila ionekane ilikuwa propaganda ya kumzuia kwenda Ikulu.

Sekta ya elimu na ile ya afya nazo zinakabiliwa na changamoto kubwa. Katika hilo la elimu, inaelezwa kuwa ni asimilia 67 tu ya wananchi zaidi ya milioni 80 wanaoweza kusoma na kuandika.

Wanawake ni wahanga wakubwa katika hilo kutokana na ukweli kwamba ni asilimia 57 tu ya waliozidi umri wa miaka 15 wanaweza kusoma na kuandika.

Changamoto ambayo imekuwa ikitajwa zaidi ni sehemu kubwa ya wazazi kushindwa kumudu gharama za elimu. Ukiliweka kando hilo, pia hali ya usalama nayo si rafiki katika mchakato wa utoaji elimu kutokana na hofu ya wazazi kupeleka watoto wao shule na uharibifu wa miundombinu ya elimu.

Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) imewahi kuonesha ukubwa wa changamoto hiyo ya elimu nchini DRC, ambapo mwaka 2003, ilionesha kuwa asilimia 50 ya watoto hawako shuleni, idadi kubwa ikiwa ni wale wa maeneo ya vijijini.

Mwaka 2016, Serikali ya Kabila ilianzisha mkakati wa Sekta ya Elimu ya 2016 – 2025, lakini ukweli ni kwamba kufikia mwaka jana, watoto milioni 3.5  sawa na asilimia 26.7  waliotakiwa kuwa shule ya msingi walikuwa mitaani, milioni 2.75 kati ya hao wakiwa ni wa vijijini.

Kwa upande wa afya, magonjwa kama Ukimwi, malaria na homa ya manjano yamekuwa yakisumbua na hapo ni kwa kuiweka kando Ebola ambayo mara kwa mara imekuwa tishio kwa maisha ya Wakongo.

Takwimu zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2012, asilimia 1.1 ya watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 walikuwa wakiishi na maambukizi ya virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi.

Kama hiyo haitoshi, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limewahi kuitaja DRC katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Matarajio  ya wananchi wengi wa DRC ni kuona namna Tshisekedi atakavyoweza kukabiliana na mfupa huo aliouacha Kabila, hivyo kujiweka mbali na ile dhana ya kuwa ni kibaraka wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles