23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Haya ndiyo mambo yaliyomjengea Bashe imani, asiyaache

 Na ANDREW MSECHU

NI imani iliyojengwa kwa muda mrefu, hata Rais Dk. John Magufuli, kuona umuhimu wa kumteua Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Bashe anashika nafasi hiyo kuungana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akijaza nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na aliyekuwa mtangulizi wake, Innocent Bashungwa, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Baada ya uteuzi wake huo wa Julai 21, 2019, Rais Magufuli amemtaka Naibu Waziri wa Kilimo, Bashe, kutimiza kwa vitendo mambo yote aliyokuwa akishauri akiwa bungeni kuhusu sera nzuri za kilimo zinavyoweza kuleta matokeo katika uzalishaji viwandani.

“Bashe nakupongeza kwa kuchaguliwa naibu waziri wa sekta ambayo ni muhimu, nimekuwa nakusikiliza sana bungeni michango yako imekuwa ni mizuri.

“Unatoa ‘analysis’ (uchambuzi) ya namna kilimo kinavyoweza kuleta manufaa katika uchumi wa nchi yetu, ‘analysis’ zile ‘zimeni–impress’, nilizipenda, sasa zile zilikuwa za bungeni, nataka sasa ukaziweke kwenye ‘practical’ (vitendo).

“Ndiyo maana nimekuweka kwenye Wizara ya Kilimo, hayo yote ya ‘theory’ (nadharia) uliyokuwa ukiyazungumza bungeni na tukafurahia, sasa yakawe kwenye ‘practical’ (vitendo).

“Na mimi nina matumaini makubwa kwa sababu huwezi ukazungumza tu ‘theory’ (nadharia) halafu ‘practical’ (vitendo) ikakataa, ni matumaini yangu kwamba yale ambayo uliyafikiria, umeyashauri, sasa kayatekeleze,” anasema Rais Magufuli.

Anasema sekta ya kilimo ni muhimu, lakini ina changamoto nyingi na wizi mwingi hivyo, akaitaka Wizara ya Kilimo kuwasimamia wakulima wanyonge na kushirikiana na wizara nyingine kama ya Biashara na Jeshi la Magereza kuzimaliza.

“Mtapigwa vita, mtazungumzwa, nendeni muyavumilie mumuachie Mungu, kashirikianeni na wanyonge, nina uhakika mtafanya makubwa,” anasema. Anaitaka wizara hiyo pia kwenda kusimamia mazao ya kilimo yalete faida na wananchi ili wapate utajiri kutokana na kilimo.

Kwa kauli hii ya Rais Dk. Magufuli, inadhihirisha kuwa uteuzi wake kwa Bashe, miaka mitatu na nusu tangu aingie madarakani umekuwa wenye mchakato mrefu wa tathmini ya kiongozi huyo, ambaye yeye mwenyewe amekuwa akijipambanua kuwa ni mwakilishi wa wananchi wa Nzega, lakini katika upana wake, awapo bungeni ni mwakilishi wa Watanzania wote

Hii inaweza kutafsiriwa kuwa uteuzi wa Bashe, imekuwa sehemu ya safari yake ndefu ya kisiasa, lakini zaidi katika Serikali ya Awamu ya Tano, inayoonesha mchango wake katika kuhudumu kwenye Bunge.                          

Mtiririko wa matukio unaonesha kuwa Bashe amekuwa mstari wa mbele, bila hofu, kuchambua kwa kina na kuonesha madhaifu katika utendaji wa Serikali na hasa katika wizara kadhaa, ikiwamo ile ya Fedha na Mipango, Miundombinu na hata ya Kilimo.

Bashe, ambaye amekuwa akitajwa kama miongoni mwa ‘vijana jeuri’ ndani ya CCM, ambao pamoja na changamoto wanazokumbana nazo hajawahi kukata tamaa, ana historia ndefu kwenye harakati zake za kisiasa.

Ikumbukwe kwamba, ni Bashe huyu huyu ambaye baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kuteuliwa mwaka jana, alisema hadharani kwamba anahitaji vijana wa aina ya Bashe na Nape Nnauye, ambao wanaweza kuzungumza na kuikosoa Serikali, kisha kuwachukua na kuwatumia ipasavyo katika uchaguzi wa mbunge kule Buyungu.

Akimchambua Bashe na Nape, alipokuwa katika Mji wa Nzega, Julai, 2018, Dk. Bashiru aliwataja kuwa ni wabunge wawili ‘watukutu na wadadisi, ambao CCM inapaswa kujivunia.’

Anasema kwa sasa CCM inapaswa kujivunia kutokana na namna wanavyodadisi mambo na kuyafuatilia, jambo linalofanya mawaziri wafikiri kwa kina kabla ya kutoa majibu na uamuzi.

Wakati Bashe akipata uteuzi huo ambao sasa unamfanya kutokuwa mzungumzaji bungeni, bali kuingia katika safu ya watendaji wa Serikali ambao ndio watakaokuwa watetezi wa Serikali bungeni, kumbukumbu za misimamo yake zinarejea michango yake ya hivi karibuni katika Bunge la Bajeti, Juni 27, mwaka huu, ambapo alitoa ushauri wake wa mwisho kwa Serikali kabla ya uteuzi huu, uliohusu Muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2019.

Katika ushauri huo, alizungumzia na kuitaka Serikali kuruhusu wakulima wa pamba kuuza moja kwa moja zao hilo kwa wanunuzi ili kuwapunguzia gharama za usafirishaji.

Ushauri wake mkuu katika uchangiaji wa muswada huo, ulikuwa pamoja na msamaha wa kodi kwa wasindikaji wa mvinyo unaotokana na zabibu.

Kuhusu pamba

Katika uchangiaji wake, Bashe alisema hadi hivi sasa hakuna wanunuzi wa pamba katika mikoa ambayo wanalima pamba na kwamba Serikali ya Tanzania imetoa bei elekezi kwa zao hilo ambayo ni Sh 1,200 kwa kilo moja lakini bei ya pamba inategemea soko la dunia.

Aliainisha kuwa utaratibu uliowekwa ni wakulima kupeleka pamba katika Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) na hivyo kumlazimu mnunuzi kugharamia usafiri wa kupeleka katika kiwanda.

Alisema ukichanganya na ushuru na kodi anazotozwa mnunuzi inamfanya kununua kwa zaidi ya Sh 1,200 kwa kilo.

Bashe alisema taasisi za fedha zikiangalia mkataba zinaona hatari ambazo mfanyabiashara anazo na hivyo kusita kutoa mkopo.

Aliishauri Serikali kuruhusu wakulima kupeleka moja kwa moja pamba kwa wanunuzi badala ya kupitia AMCOS ili kupunguza gharama mnunuzi.

Pia alitaka kufutwa kwa Sh100 ambayo inalipwa kwa Bodi ya Pamba ili wanunuzi waweze kumudu bei ya bidhaa hizo.

Mazao ya wanyama

Bashe alitoa ufafanuzu akieleza kuwa suala la ngozi za wanyama, taarifa ya kikosi kazi cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetaja changamoto mbili za sekta ya ngozi nchini ambazo ni kodi ya mauzo ya nje (Export levy).

Alisema matokeo yake viwanda saba vilivyopo nchini vinashindwa kununua ngozi kutoka kwa wafugaji kwa sababu ngozi haziuziki nje ya nchi. “Nawaomba Serikali muwaite wenye viwanda msaini nao mikataba ya ufanisi, muwasimamie waweze kusindika ngozi hii na kuongeza thamani,” anasema.

Kuhusu mvinyo

Katika uchambuzi wake mkubwa wa mwisho kuufanya bungeni, kabla ya uteuzi wa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, ambayo sasa itamfanya asiwe mchangiaji wa kuiwajibisha Serikali bali kuitetea, Bashe aliipongeza Serikali kwa kutoa msamaha kwa mvinyo unaozalishwa kwa ndizi lakini akashauri kuongeza wigo kwa kuongeza zao la zabibu.

Anasema zabibu ina changamoto ya vifungashio jambo ambalo linamfanya msindikaji kushindwa kushindana na wazalishaji wa nje ya nchi.

Anasema katika mpango wametenga Sh10 bilioni katika ngozi lakini ushauri wake fedha hizo zipelekwe katika kilimo cha zabibu ili wakulima wa zao hilo mkoani Dodoma waweze kunufaika.

Siku chache kabla ya Juni 27, yaani Juni 18, mwaka huu, Bashe aliichambua bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020 ya Sh trilioni 33.1 kwa kueleza jinsi wizara tatu zinazochangia asilimia zaidi ya 30 ya Pato la Taifa zilivyotengewa fedha kidogo za maendeleo.

Huku akichambua mfumo mzuri wa ufanyaji biashara ili kuondoa malalamiko na nchi kupata mapato zaidi, Bashe anasema ni lazima kuunganisha uzalishaji wa malighafi na ukuaji wa viwanda.

Mbunge huyo (Kwa sasa Naibu Waziri wa Kilimo) alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti kuu ya Serikali huku akizitaja wizara hizo tatu kuwa ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Viwanda na Biashara.

Bajeti ya Kilimo mwaka 2019/2020 ni Sh bilioni 253.85 zikiwamo Sh bilioni 143.57 za maendeleo; Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sh bilioni 64.91 bilioni (Sh bilioni 17.69 ni za maendeleo) na Wizara ya Viwanda na Biashara Sh bilioni 100.38 (Sh bilioni 51.5 za maendeleo). Fedha za maendeleo katika bajeti ya 2019/2020 ni Sh trilioni 12.25.

“Ukichukua bajeti yote ya maendeleo ya Sh trilioni 12 na kuangalia kiasi kilichotengwa katika sekta ya kilimo na mifugo, utabaini ni jumla ya Sh bilioni 61 sawa na asilimia 1.3 ya fedha zote za maendeleo. Kwa hali hii hatuwezi kupiga hatua.”

“Sisi tunauza mazao ya kilimo, tumbaku imeshuka kutoka tani milioni 1.2 hadi tani 50,000; korosho 2016/17 ilikuwa tani 265,000 na 2018/19 ni tani 224,000; mkonge tani 36,000 hadi tani 15,000; chai kutoka tani 26,000 tunakwenda tani 19,000; sukari kutoka tani 330,000 tunaenda tani 327,000; pareto kutoka tani 2,150 hadi tani 1,800,” alikaririwa.

Februari 4, 2018, Bashe alikaririwa akisema kuwa takwimu mbalimbali ambazo zinatolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonyesha mambo hayapo sawa hivyo kuna haja kubwa kwa Serikali kupitia Waziri wa Fedha kubadili sera zake za kibajeti.

Bashe alidai takwimu mbalimbali kutoka BoT mwaka 2011 hadi Desemba 2017 zinaonyesha kuwa kuna mabadiliko makubwa na vitu kushuka kwa kasi kubwa.

“Umefika wakati kama nchi hasa Wizara yetu ya Fedha kukubali kubadili sera zake za kibajeti, nitatoa takwimu chache ambazo ukitazama takwimu hizi zinazoonekana kwenye taarifa za BoT kuanzia mwaka 2011 hadi 2017, mzunguko wa fedha umeshuka kutoka asilimia 22 ya mwaka 2011 hadi asilimia 1.8 ya sasa hivi, ukiangalia export (mauzo ya nje) hasa ya mazao ya kilimo ambayo ndiyo yameajiri asilimia 70 Tanzania.

“Ukichukua zao la kahawa mwaka 2011 gross rate yake ilikuwa asilimia 55 lakini sasa hivi ni asilimia 5.4, pamba mwaka 2012 ilikua kwa asilimia 16 sasa hivi ziimekua kwa asilimia 3.8, mkonge ndiyo imekuwa na ongezeko la asilimia 2.9 iliyokuwa mwaka 2012 sasa hivi ipo kwa asilimia nne,” alisema Bashe

Aliendelea kufafanua: “Manufacturing mwaka 2011 ilikuwa kwa asilimia 96, gross rate sasa hivi imekuwa kwa asilimia – 244, tafsiri yake ni ndogo tu sera zetu hazichochei ukuaji wa biashara na uchumi katika nchi. Takwimu zinaonyesha Watanzania tunakua kwa wastani wa asilimia mbili na kitu lakini ukuajia wetu wa kilimo ni asilimia 0.4, hakuna uwiano hapa.

“Hili ni jambo ambalo hata tukasema humu ndani ya Bunge lisifurahishe upande wa Serikali kwa kauli zetu lakini tuna jukumu la kusema ukweli na ni muhimu kabisa Wizara ya Fedha ikakubali kwamba sera za kibajeti za Wizara ya Fedha si rafiki katika kuchochea kukuza uchumi wetu.”

Matatizo ya Serikali

Katika moja ya uchangiaji wake mijadala bungeni, Novemba 8, 2018, Bashe alielezea mtazamo wake kwa Serikali akisema: “Serikali ina matatizo, Waziri wa Fedha namuonea huruma.” Huku akiitaka Serikali kuhakikisha inawasilisha Bungeni mpango mkakati wenye tija na endelevu ili kuwa na mipango ya muda mrefu katika kukuza uchumi wa taifa.

Anasema binadamu hutazwamwa katika macho matatu, la kwanza ni jinsi unavyojitazama na kujifahamu wewe mwenyewe, la pili ni jinsi Mwenyezi Mungu anavyokuelewa na la tatu ni namna wenzako wanavyokutazama na kukufahamu.

Alisema Tanzania kama Taifa ni lazima tutambue ni namna gani tunajitazama na kujipima, lakini kwa kuwa hatuishi peke yetu kama kisiwa, tunaishi katika ulimwengu wenye mataifa lukuki, wenzetu pia wanatutazama.

“Kwa Wizara ya Fedha na mipango huu utakuwa mpango wa nne hivyo, kama hatutaamua kama Taifa, kufungua mambo matatu ambayo wabunge wamepigia kelele kwa miaka mitatu sasa, hatuwezi kupiga hatua kama nchi.

“Katika Taifa letu asilimia 60 hadi 70 ni wakulima na hawa ndio drivers ya kuanzisha viwanda na kujenga uchumi. Tunafanya ujenzi mkubwa wa reli na barabara kwa ajili ya kusafirisha bidhaa na binadamu, lakini mazao yote ya kilimo chakula na ya biashara yanaanguka kwa ‘factor’ za nje na za ndani. Ninamshauri Waziri wa Fedha kwa heshima kwanza aje na mpango wa kuanzia price stabilization fund kwa ajili ya kusaidia kilimo,” alisema.

Alisema mfuko huo utakaokuwa maalumu kwa ajili ya kuimarisha bei za mazao ya kilimo utaangalia gharama zote anazotumia mkulima na kusaidia namna ya kuweka subsidies kwenye bei ya mazao ya mkulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles