30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HATUA SAHIHI ZICHUKULIWE  KWA WATUMISHI HAWA  

 


Karibu siku tano sasa, gazeti hili limekuwa likiripoti habari kuhusu mjamzito mmoja, mkazi wa Wazo, Dar es Salaam, Sonia Daud, anayedaiwa kujifungulia nje ya zahanati  ya Madale wilayani Kinondoni.

Tukio hilo limekuwa na mjadala mkubwa si kwa vyombo vya habari pekee, bali hata kwenye mitandao ya jamii.  Watu wengi wanashangaa kuona inakuwaje mjamzito ajifungulie nje ya kituo cha afya wakati wauguzi wanatakiwa kuwapo muda wote.

Hali hiyo imesababisha hofu kubwa kwa wagonjwa au wajawazito wanaotumia zahanati hiyo kwa sababu inaonyesha wazi   suala la uajibikaji lina kasoro kwa watumishi wa umma kushindwa kutimizwa wajibu wao.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kwa watumishi wote wa zahanati hiyo waliokuwa zamu siku hiyo.

Alisema kila mtu aliyekuwa zamu atachukuliwa hatua kulingana na uchunguzi utakaofanywa na timu yake ya watalaamu.

Alisema  hadi sasa  hatua iliyochukuliwa ni   watumishi wote kutakiwa kuandika maelezo yao  kwa nini waliondoka kazini kabla ya wakati.

Alisema  uongozi wa Manispaa ya Kinondoni umesikitishwa na tukio na kuahidi kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria bila kumuonea mtu yeyote katika suala hilo.

Kwa miaka kadhaa sekta ya afya ilikuwa miongoni mwa sehemu  zilizokuwa zikilalamikiwa   na Watanzania kutokana na   kushamiri   vitendo vya rushwa na lugha chafu.

Lakini baada ya Serikali ya awamu  ya tano kuingia madarakani, ilianza kuisafisha hadi kufikia hatua ya Watanzania  kufurahia huduma za tiba katika hospitali nyingi   za Serikali ambazo zilikuwa zikilalamikiwa.

Pamoja na hatua hizo zote kuchukuliwa wapo baadhi ya watumishi ambao wanaonekana  ni wagumu kubadilika. Tukio hilo la mjamzito limeibua tena machungu makubwa.

Sera ya afya inasema lazima mjamzito ajifungulie sehemu salama kwa uangalizi wa wataalamu,  inakuwaje hawa ambao wamepewa dhamana ya kusimamia wanakosekana sehemu ya kazi?

Tunapatwa na wasiwasi kwamba inawezekana watumishi hao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea mno, jambo ambalo wao wanaliona ni la kawaida  kumbe hawajui kama wanahatarisha usalama wa wagonjwa.

Tunajiuliza maswali mengi kuliko majibu, inakuwaje mkuu wa zanahati hiyo anakwenda kulala bila kuhakiki kama watumishi wanapaswa kuwa zamu wako kazini? Hayo ni matokeo ya kufanya kazi kwa kubebana na kulindana.

Tunapenda kutoa wito kwa watumishi wa afya kwamba zahanati  zinapaswa kufanya kazi saa 24 kwa sababu huwezi kujua mtu anayehitaji huduma atafikishwa hapo saa ngapi. Tukio hilo linapaswa kutoa funzo kwa uongozi wa manispaa nzima kujipanga upya hasa katika maeneo ya pembezoni ambako watumishi hujiona wako huru zaidi.

Hatua hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanyonge wanaonyanyaswa na wauguzi. Kwa mfano, tukio limetokea Dar es Salaam ambako kuna vyombo vya habari, je lingetokea sehemu nyingine tofauti  ambayo haifikiwi kwa urahisi na vyombo vya habari, si ndiyo lingezimika kimya kimya! Tunasema hapana lazima watumishi wa sekta hii wabadilike  na kupenda kazi yao.

Tunaushauri  uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua stahiki bila kumuonea hata mmoja ili kurudisha nidhamu na kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Tunamalizia kwa kusema Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe, lazima tutangulize uzalendo   bila kusukumwa na viongozi wa juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles