26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

HATIMA YA MUGABE MIKONONI MWA BUNGE LEO

HARARE, ZIMBABWE

MCHAKATO wa kumng’oa Rais Robert Mugabe umeanza jana asubuhi na ramani ikichorwa namna ya kumfukuza kikatiba kwa kura ya kukosa imani naye bungeni wakati chombo hicho kikikutana leo, imebainika.

Chama chake tawala cha ZANU-PF kilichomfukuza uongozi juzi Jumapili, kilikuwa kimempa nafasi ya mwisho hadi jana mchana awe amejiuzulu mwenyewe, kitu ambacho Mugabe alikipuuza kama alivyowahadaa majenerali wa jeshi juzi usiku.

Katika taarifa nyingine, Shirika la Habari la Marekani (CNN), liliripoti kuwa Mugabe amekubali kujiuzulu na kwamba hotuba ya kujiuzulu  tayari imeshaandikwa.

Shirika hilo limeinukuu duru inayofahamu mazungumzo kati ya Mugabe na makamanda wa jeshi waliotwaa mamlaka wiki iliyopita.

Katika makubaliano ya kujiuzulu, Mugabe na mkewe Grace watapewa kinga kamili dhidi ya kukamatwa, kushtakiwa au kunyang’anywa mali walizochuma.

Mugabe (93) imeripotiwa akisisitiza kinga ya kutoshtakiwa kwake, mkewe Grace (52) na wanawe kama moja ya masharti ya kukubali kung’atuka.

Usiku wa kuamkia jana, Mugabe aliwaacha Wazimbabwe wengi kwenye mataa baada ya kukwepa kutangaza kujiuzulu, badala yake akiapa kuendelea kuiongoza ZANU-PF kutatua matatizo ndani kuliko kukabidhi chama kwa makamu wa rais aliyemfukuza, Emmerson Mnangagwa.

Mugabe alitoa hotuba katika televisheni kwa umma juzi usiku ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu jeshi lishike madaraka, ikiwa ni saa kadhaa baada ya chama chake kumfukuza uongozi.

Aidha imekuja huku maandamano makubwa yakiwa yamefanyika Jumamosi iliyopita yakimtaka ajiuzulu.

Mapema jana, kulikuwa na umati wa waandamanaji katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe mjini Harare wakimtaka Mugabe ajiuzulu.

Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni usiku wa kuamkia jana, huku akikwama mara kwa mara, Mugabe alisema: ”Chama tawala, ZANU-PF kitakuwa na mkutano mkuu Desemba mwaka huu na ‘nitauongoza mchakato huo.”

Kauli yake hiyo iliingiza Zimbabwe katika hali ya sintofahamu kubwa, sababu inaashiria kuwa anataka kuendelea kuwa rais hadi angalau katikati mwa Desemba. 

AFUMBIA MACHO HALI HALISI

Makamanda wa jeshi waliochukua udhibiti wa nchi, wamekuwa katika mazungumzo na Mugabe ambayo inaelekea yaliambulia patupu wakati huo.

Katika hotuba yake Mugabe, hakusema chochote kuhusu miito inayomtaka ajiuzulu, wala kuzungumzia hatua ya jeshi kuchukua udhibiti wa nchi wiki iliyopita akisema ”haikutengua utaratibu wa kikatiba wala kuondoa mamlaka yangu kama mkuu wa nchi na Amiri Mkuu wa Jeshi.”

Badala yake alizungumza kana kwamba hakuna kilichotokea, akitoa rai ya utulivu na mshikamano, lakini pia akikiri makosa chini ya uongozi wake, akitaka apewe muda kuyarekebisha.

Matamshi ya Mugabe na ukaidi wake viliwakasirisha Wazimbabwe wengi, na kuibua wasiwasi kwamba nchi hiyo inaweza kutumbukia katika ghasia na mivutano ya kisiasa.

Inafahamika kuwa Mugabe huenda alikubali katika majadiliano yake na majenerali wa jeshi juzi jioni kujiuzulu, lakini chama tawala hakikutaka afanye hivyo mbele ya jeshi. Chanzo kimoja ndani ya chama kimesema kwamba hilo lingefanya ionekane uingiliaji wa jeshi kuwa mapinduzi.

Lakini Mwenyekiti wa Chama cha Maveterani wa Vita ambao wana ushawishi mkubwa katika siasa za Zimbabwe, Chris Mutsvangwa, ametoa mwito kufanyika maandamano mapya na hatua za kisheria kumshinikiza Mugabe kuondoka.

Mutsvangwa, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kumwondoa Mugabe alisema: “Mpango wa kumng’oa unaendelea.

“Alipewa nafasi ameiharibu. Wanasheria wa Serikali wanaandaa nyaraka sasa. Kila kitu kiko vizuri, Bunge litamng’oa kesho (leo).”

Chama cha maveterani wa vita vya ukombozi wa nchi hiyo, kilipigana bega kwa bega na Mugabe, lakini uhusiano wao ulivunjika mwaka jana, baada ya kutofurahishwa kupanda haraka kwa mkewe kisiasa.

Mutsvangwa ambaye ni kiongozi wa maveterani, alisema wataongoza maandamano zaidi dhidi ya Mugabe na pia wataelekea mahakamani kuwasilisha kesi  kumshtaki kwa kushindwa katika majukumu yake.

“Rais Mugabe aliwashangaza Wazimbabwe katika hotuba yake iliyopeperushwa katika televisheni usiku wa kuamkia leo (jana), pale alipokwepa kutaja lolote kuhusu kujiuzulu, badala yake aliahidi kuongoza mkutano wa wajumbe wa chama tawala ZANU-PF mwezi ujao, hii ni licha kuwa chama hicho kilimwondoa  kama kiongozi jana (juzi),” alisema.

Akizungumza mjini Harare, alisema: “Mugabe, nenda sasa, nenda sasa, saa yako imefika! Tafadhali ondoka Ikulu iache nchi ianze ukurasa mpya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles