27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

HATA NAPE!

Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam


HATA Nape! Ndio mshangao ambao mtu anaweza kuupata, baada ya jana aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutolewa bastola na mtu anayedhaniwa kuwa ni wa Usalama wa Taifa, akimzuia kuzungumza na waandishi wa habari aliokuwa amewaita katika Hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay, Dar es Salaam.

Tukio hilo ambalo liliibua purukushani kati ya Nape na mwanausalama huyo, lilitokea saa chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kumwondoa katika nafasi yake ya uwaziri.

Hata hivyo, baadae Nape alizungumza na waandishi wa habari akiwa juu ya gari lake lililokuwa limesimama nje ya Kanisa la Mtakatifu Petro.

Kitendo cha kutolewa bastola kilichotanguliwa na kile cha Meneja wa Hoteli ya Protea, aliyejitambulisha kwa jina moja la Suleiman, kutangaza kuzuia mkutano wake na waandishi wa habari usifanyike katika hoteli hiyo kwa kile alichodai kuwa ni maelekezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda, kiliibua taharuki kwa wanahabari na watu waliokuwa wakifuatilia kile alichokusudia kukizungumza.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa hasira na uchungu baada ya mwanausalama huyo kushindana naye na kisha kumwacha, Nape alihoji aliyempa mamlaka mtu huyo aliyemtolea bastola.

“Nani amekupa mamlaka hayo? Unalipwa kwa kodi ya kwetu wavuja jasho hapa, halafu anakuja mpuuzi anatoa bastola, rudi kwenye gari, how? (kwa vipi?) You know how I fought for this country? (unajua nilivyopambana kwa ajili ya nchi hii?) Nimekwenda miezi 28 nalala porini, angalieni mkono wangu huu (anaonyesha mkono wake wa kulia ambao una kovu), napigana kuirudisha CCM madarakani, anakuja mpuuzi mmoja anatoa bastola hapa, mnataka tuonee? it can’t be.

“Mimi mtoto wa Kimakonde, ngoja nisimame vizuri sasa, naomba mnisikilize, mimi Nape nataka kurudia, sina kinyongo na uamuzi wa rais wangu, kama ambavyo sikumshawishi kunichangua, ndivyo ambavyo sikumshawishi kunichagua na ndivyo ambavyo sisemi kwa uamuzi alioufanya.

“Lakini wakati anaunda baraza, walikuwa watu wengi sana, alipoamua kunichukua mimi kuna watu walikuwepo na walikubali, mimi leo nakatalia nini, sina sababu ya kukataa,” alisema Nape na kuongeza:

“Nimejitahidi kutimiza wajibu wangu na jana wakati naongea na vyombo vya habari juu ya ripoti (ripoti ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia Clouds), nilisema  kuna gharama ya kulipa kwenye kusimamia haki za watu na mimi nipo tayari kulipa gharama hiyo, sioni sababu kwanini vyombo ‘vina-panic’, sioni sababu kwanini watu ‘wa-panic’.” 

Nape ambaye wakati anazungumza alikuwa amezungukwa pia na askari kanzu, alisema yeye ni Mtanzania na ni mdogo kuliko nchi hii, huku akisisitiza kuwa Tanzania ni kubwa kuliko yeye, hivyo wasihangaike naye bali wahangaike na Tanzania  inakokwenda kwani hilo ndilo kubwa kuliko yote.

Alisema uzalendo wake kwa nchi yake hauwezi kutiliwa shaka hata kidogo na vijana ‘wahuni’ waliofika na kumyooshea bastola.

“Nimekuwa mzalendo kwa nchi yangu, nimekuwa muungwana kwa nchi yangu na ninaapa kuendelea kuwa muungwana kwa nchi yangu, hilo hakuna mtu atakayelibadilisha, lakini mimi nimekuwa mzalendo kwa CCM ambayo niliikuta ipo kwenye shimo inakwenda, nikasimama kuiinua, Watanzania wanajua, uzalendo huo hauna mashaka hata kidogo na kwa uzalendo huo ndiko nilikoambiwa nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko na nilichokisimamia juzi ni kusema kweli, kinachowakutanisha watu sio magwanda ya kijani, ni imani kwamba tuwe wakweli daima tuachane na fitina,” alisema Nape kwa uchungu.

Akizungumzia kuhusu uteuzi wa Waziri aliyerithi nafasi yake, Dk. Harrison Mwakyembe alisema wakati yeye alipoteuliwa hakuulizwa, hivyo kama amewekwa Mtanzania mwingine hana haja ya kuulizwa na wala hana kinyongo na Rais wake.

Pamoja na hayo, alionya pasipo kutaja jina la yeyote akisema isifike mahali wao ndio wawe waamuzi wa vijana wa nchi hii na kwamba vijana wa Kitanzania lazima wasikie.

“We have nothing, nothing to fear except the fear itself (hatuna cha kuogopa isipokuwa woga wenyewe),” alisema na kuongeza:

 “Lakini mimi naweka jambo hili, nimekuwa nasimamia katika ukweli na kile ninachokiamini, ninyi mnakumbuka mimi nimeshawahi kufukuzwa CCM, wala si shida, katika maisha ya kisiasa usipopitia migogoro bado hujakomaa, ili mbegu iote lazima ioze ndipo iote, na mbegu niliyoipanda kwa hakika itaota,” alisema Nape.

Hata hivyo, Nape hakusita kuwaasa vijana kutoogopa na kuwataka kusimamia kile wanachokiamini, kwani Tanzania ni ya wote.

“Nchi hii ni yetu, Mwalimu alikuwepo akaondoka, Kawawa na wenzake kina mzee Nnauye walikuwepo wakaondoka, na sisi tutaondoka, swali la kujiuliza ni tunawaachia Watanzania nchi ya namna gani, tunawachia watoto wetu nchi ya namna gani, uamuzi wa nchi ya kuwaachia ni wa kwetu,” alisema Nape.

Aidha, Nape alitanabaisha lengo la kuitisha mkutano wake na waandishi wa habari lilikuwa ni kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi alioufanya na kumshukuru kwa kumwamini kwa mwaka mmoja.

“Kwa mwaka mmoja ameniamini kama kijana wake, akanipa heshima ya kuingia kwenye baraza moja kwa moja, ninamshukuru sana na kama alivyoniamini yeye, anadhani nimetumika ipasavyo, amemuweka kaka yangu Dk. Harrison Mwakyembe na mimi namuunga mkono, nampongeza Harrison kwa kuteuliwa, yeye ni mwanahabari, ni mwasheria atasimamia haki.

“Wito wangu nimefanya kazi kwa mwaka mmoja na tasnia ya habari, tasnia ya sanaa, tasnia ya utamaduni na wanamichezo, ninaamini nimetumia uwezo wangu wote, nguvu zangu zote kuwatumikia, niko hapa kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu, mmenipa ushirikiano wa kutosha, tumefanya kazi pamoja kwa ushirikiano and I really really love you people (na ninawapenda sana ninyi watu) na nilipenda kufanya kazi nanyi, nimefurahi sana kwa dhati ya moyo wangu, nimefurahi kufanya kazi na ninyi.

“Ninawaomba muungeni waziri mpya ndani ya wizara hii, muungeni mkono, fanyeni naye kazi, lakini endeleeni kumuunga mkono Rais Magufuli, ndiye rais tuliyepewa na Mwenyezi Mungu, ndiye rais tuliyempigia debe Watanzania mkamuamini mkampa dhamana, nawaomba mumuunge mkono na sisi Watanzania tudumishe umoja na mshikamano wa nchi yetu,” alisema Nape huku baadhi ya waandishi wa habari wakimjibu; “hatumuungi mkonooo!”

Nape ambaye wakati anazungumza alikuwa kwenye gari la Serikali lenye namba STL 3107 alisema anajua wako watu kwa namna moja ama nyingine wameumia, lakini anawaomba kama yeye waliyemwamini yuko vizuri, maisha lazima yaendelee, hivyo watu watulie na kuituliza nchi na kwamba yako mambo mazuri mbele na hakuna sababu ya kuvurugana.

“Narudia, Nape ni mdogo kuliko nchi, tusije tukamgeuza Nape akawa badala ya Tanzania, ninawaombeni sana, moyo wangu, nafsi yangu na mwili wangu unawapenda na nilipenda kuendelea kufanya kazi nanyi, lakini wakati wa aliyeniweka umefika, tutakwenda pamoja wala msivunjike moyo, simamieni mnachokiamini, songeni mbele, endeleeni.

“Mwisho nataka niwaambie wananchi wangu wa Mtama, wamenitumia jumbe (ujumbe) nyingi za kunitakia mema, ninawashukuru kwa upendo wao, nataka niwaahidi nitaendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote. Nilipoondoka na kuacha ukatibu mwenezi, nilikwenda kuomba ubunge si uwaziri na mimi ubunge nikapewa na ninarudi kufanya kazi yangu ambayo Wanamtama wamenituma kufanya, nitawatumikia kwa moyo wangu wote, nitapambana kwa maendeleo yao na yale niliyoyaahidi nitayafanya, ninawaombeni sana tutulie, tuendelee na shughuli zetu, nawaombeni sana,” alisema Nape.

Baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari, Nape alirudi katika kiti cha gari lake na kisha kuondoka, ingawa alipofika katika geti la kutokea, alizuiliwa na gari la Kamanda wa Polisi wa Kinondoni lenye namba PT 2574.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=oEdovxg2Fn0[/embedyt]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles