Hasunga atoa matumani kwa wakulima wa pamba

0
2542

MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI wa Kilimo,   Japhet Hasunga, amewaeleza wabunge wa maeneo yanayolima pamba kuwa wizara hiyo imedhamiria kumkomboa mkulima wa pamba.

Alisema  kwa kuanza imeanzisha hatua ya kuwasajili wakulima wote nchini wakiwamo wa pamba.

Amesema serikali imetengeneza mfumo maalumu wa kuwatambua kwanza wakulima, maeneo wanayotoka, mashamba yao yapo wapi na yana ukubwa gani.

Hayo aliyasema jana wakati wa kikao maalumu na wabunge hao katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo  Dodoma.

Kikao  hicho kilikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa mauzo ya pamba ambao unatarajia kuanza Aprili mwaka huu.

Alisema moja ya mambo ambayo Wizara ya Kilimo itahakikisha inayashughulikia ipasavyo,   na kuwatambua wakulima wa pamba ni pamoja na kuupitia upya mfumo wa ushirika katika ununuzi wa pamba, mfumo wa uagizaji na uingizaji wa viuatilifu vya pamba   na masoko ya zao hilo.

  Hasunga alisema katika kipindi   kifupi amekuwa akipata malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wa mazao mbalimbali kuhusu udhaifu wa mfumo wa uagizaji wa uingizaji wa pembejeo za kilimo yakiwamo madawa na mbegu hafifu.

“Napenda nikiri kuwa tuna tatizo katika mfumo wa uagizaji na uingizaji wa pembejeo za kilimo, bado haujakaa vizuri lakini baya zaidi ni viuatilifu hafifu.

“Serikali kamwe haiwezi kutazama wakulima wakionewa na wajanja wachache na huu ni uhujumu uchumi, lazima wanaofanya mambo haya wachukuliwe hatua kali za  sheria,” alisema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Wabunge wameshauri muda wa kupeleka pembejeo za kilimo kama mbegu bora na madawa uwe mapema zaidi kuliko ilivyo sasa.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here