25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hali tete ajali Morogoro

*Waliofariki sasa wafikia 85, kati yao 11 wamefariki wakiwa Muhimbili, wengine 17 bado wapo ICU

*Orodha vifaa vinavyotakiwa kusaidia majeruhi kutolewa, Dk. Mashiru ataka zitengwe barabara za malori

Mwandishi wetu -DAR ES SALAAM

MAJERUHI sita kati ya 38 wa ajali ya moto wa mafuta iliyotokea Jumamosi mkoani Morogoro, waliokuwa wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Kutokana na vifo hivyo, idadi ya waliofariki dunia hadi sasa imefikia 85.

Majeruhi wengine 17 wa ajali hiyo iliyotokea baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto pale watu walipolivamia na kuanza kuiba mafuta, wanaendelea na matibabu chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) hospitalini hapo.

Baada ya ajali hiyo, majeruhi 46 walisafirishwa kutoka Morogoro na kupelekwa Muhimbili Jumapili na usiku wa siku hiyo watatu walifariki dunia, Jumatatu wakafariki wanne, Jumanne mmoja na usiku wa kuamkia jana wakafariki sita.

Idadi hiyo inafanya majeruhi waliopoteza maisha wakiwa Muhimbili kufikia 14 na waliobaki wakiendelea na matibabu wakiwa 32 ambao kati yao 17 wamelazwa ICU na 15 katika wodi ya kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Muhimbili, Aminieli Aligaesha, aliwataja waliofariki dunia usiku wa kuamkia jana ni Joseph Lewanga (48), Jafari Kilombero  (30), Magreth Mtungu (44), Ramadhani Ally  (26), Musa Athumani (28) na Garadia Mbaruka (26).

 Alisema majeruhi 15 mahututi wapo wodi ya jengo la Mwaisela, majeruhi mtoto yupo chumba mahututi cha watoto, huku mama mmoja akiwa chumba mahututi cha kinamama.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, akiwajulia hali majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea Msamvu, Morogoro, waliolazwa Hospitali ya Rufaa Morogoro jana

“Jana tulikuwa na majeruhi 38, lakini leo wamebaki 32. Majeruhi sita tayari wameshafariki dunia na hadi sasa majeruhi 17 wako katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

“Mahututi 15 wako ICU iliyopo jengo la Mwaisela, kuna mtoto mmoja yupo ICU ya watoto na kwenye ICU ya kinamama yupo mmoja pia. Majeruhi wengine 15 wako katika wodi 22 jengo la Sewahaji,” alisema Aligaesha. 

Alisema wagonjwa mahututi tayari wameshachukuliwa sampuli ili kulinganishwa na ndugu zao, huku watu sita waliofariki sampuli zao zilishachukuliwa na wanasubiri kupima za ndugu ili kulinganishwa.

“Tunaendelea kuchukua sampuli za wagonjwa wote waliopo ICU ili kuzilinganisha na ndugu zao, hata waliofariki tutahakikisha watachukuliwa na ndugu zao kwa kulinganisha sampuli zao,” alisema Aligaesha. 

Hata hivyo, alisema hospitali hiyo inaendelea kupambana kuhakikisha majeruhi waliobaki wanarudi katika hali nzuri.

“Bado madaktari na wauguzi wanaendelea kupambana kuhakikisha majeruhi 32 waliobaki wanapona,” alisema Aligaesha.

Juzi Aligaesha alisema majeruhi wengi wameungua kwa asilimia 80 hadi 95.

MISAADA YAMIMINIKA

Katika hatua nyingine, wananchi wameendelea kujitokeza Muhimbili kutoa misaada mbalimbali kwa majeruhi wa ajali hiyo.

Akizungumza jana wakati akikabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 20 kwa majeruhi hao, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumayi, alisema wameguswa na tukio hilo ambalo limeleta maafa ndani ya jamii.

Alisema tukio lililotokea hakuna wa kulaumiwa kwakuwa linaweza kumpata mtu yeyote, hivyo cha msingi ni kuhakikisha majeruhi hao wanasaidiwa kwa hali na mali.

“Tumepokea misaada kwa vyama vingine rafiki vya usafirishaji na tunashukuru hili tumelitimiza,” alisema  Lukumay.

 Akipokea msaada huo, Mkuu wa Idara ya Utasishaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Batusaje John, alisema vifaa hivyo ni muhimu kwa majeruhi wa moto ambao wamekuwa wakihitaji joto kwenye vidonda na usafi.

Alisema vifaa walivyopokea ni pamoja na gozi, pamba na mafuta ambavyo vitasaidia wagonjwa hao wasipate bakteria na kuweza kutunza ngozi zao.

Batusaje alisema wamejipanga kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuokoa maisha ya majeruhi.

“Msaada huu utawafikia walengwa moja kwa moja kwani tuna imani wanahitaji zaidi vifaa tiba kuliko fedha,” alisema Batusaje.

UCHANGIAJI DAMU

Wakati huohuo, jumla ya uniti za damu 170 zimepatikana tangu kuanzishwa kwa uchangiaji damu Muhimbili, ili kuokoa maisha ya majeruhi wa moto waliolazwa hospitalini hapo.

Aligaesha alisema damu hiyo imepatikana baada ya wachangiaji wengi kuhamasika kujitolea kuokoa maisha ya majeruhi.

Alisema katika uchangiaji huo, Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo, Abdallah Ulega na timu yake ya vijana wake kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), walichangia jumla ya uniti 100.

Alisema pia Taasisi ya Kamanda mstaafu, Suleiman Kova ya Sukos walichangia kiasi cha uniti 70.

“Tunashukuru Mungu hali ya majeruhi inaendelea vizuri na watu wanaendelea kujitokeza kwa wingi kuchangia damu,” alisema Eligaesha.

UCHUNGUZI WA AJALI

Tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda timu ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto huo.

“Hii tume inaanza kazi, hadi Ijumaa (Agosti 16) inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii si mara ya kwanza, ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi,” alisema.

Majaliwa alisema ni lazima kujua kama kila mmoja alitimiza wajibu wake.

Alihoji kitendo cha wananchi kujichotea mafuta na kuchomoa betri ya lori hilo bila kuzuiwa licha ya kuwa eneo hilo kuwa karibu na Kituo cha Polisi Msamvu.

POLE YA MAGUFULI

Rais John Magufuli alikemea vitendo vya wananchi wanaovamia magari yenye milipuko akitaka vikomeshwe mara moja.

“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi, hasa familia za marehemu wote, nawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka.

“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko na kadhalika, nawaomba sana tuache tabia hii,” alisema Rais Magufuli.

Habari hii imeandaliwa na AVELINE KITOMARY, CHRISTINA GAULUHANGA , FAUSTINE MADILISHA na BOSCO MWINUKA (TUDACo) – Dar es salaam

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles