31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

HALI NI MBAYA KIBITI

*Kiongozi mwingine wa CCM auawa kwa risasi nyumbani kwake, motto wake ajeruhiwa
*Watendaji wa vijiji, kata wakimbia vituo vyao vya kazi kwa hofu ya kuuawa


 

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


HALI ni mbaya katika Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, baada ya watu wasiofahamika kumuua Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Iddy Kirungi huku mtoto wake, Nurdin Kirungi akipigwa risasi ya tumbo.


Wauaji hao baada ya kutekeleza unyama huo walitokomea kusikojulikana hali inayotishia usalama wa raia na mali zao, huku wengine wakilazimika kuzikimbia nyumba zao kwa hofu ya kupoteza maisha.


Jeshi la Polisi Pwani limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema linaendelea kuwasaka wahalifu na kuimarisha ulinzi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alisema Kirungi aliuawa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake juzi usiku.

“Aliyeuawa ni mwenyekiti mstaafu wa CCM na jitihada za kuwatafuta wahalifu zinaendelea tunaomba wananchi watoe ushirikiano,” alisema Lyanga.


DIWANI KATA YA MTUNDA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Diwani wa Kata ya Mtunda, Omary Twanga (CCM), alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:30 usiku na kwamba mwenyekiti huyo aliuawa akiwa nyumbani kwake.


“Polisi walikuja asubuhi (jana) wakauchukua mwili na kuupeleka katika Kituo cha Afya Ikwiriri, baada ya kumaliza taratibu zote za kipolisi hivi sasa (saa 8 mchana) ndiyo tuko kwenye mazishi,” alisema Twanga. 


Alisema mwenyekiti huyo alizikwa katika shamba lake lililoko Njia Nne katika Kijiji cha Muyuyu wilayani humo.
Alisema kutokana na mauaji yanayoendelea wilayani humo hali imekuwa tete kwani wananchi wengi wanahofia usalama wao na watu waliofika katika msiba huo hawazidi 20.


“Jambo hili ni la muda mrefu na wananchi wengi sasa wameingiwa na hofu, wanataka kuharibu sifa nzuri tuliyonayo ya kuitwa kisiwa cha amani,” alisema. 


MKUU WA WILAYA

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo, alisema kabla ya kuuawa kwa mwenyekiti huyo wauaji walianza kumjeruhi kwa kumpiga risasi ya tumboni mtoto wa marehemu, Nurdin.


Mganga wa zamu katika Kituo cha Afya Ikwiriri, Dk. Rashid Omar, alisema walimpokea Nurdin akiwa na jeraha kubwa tumboni mwake ambapo walimpatia rufaa kwenda Hospitali ya Mchukwi kutokana na kuvuja damu nyingi.


WATENDAJI WAKIMBIA 


Mauaji yanayoendelea wilayani humo yamesababisha baadhi ya watendaji kukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na kuingiwa hofu.
Vyanzo vya habari vimeliambia MTANZANIA kuwa Mtendaji wa Chumbi C katika Kata ya Chumbi amekimbia kituo chake cha kazi.


Taarifa zinaeleza kuwa mtendaji huyo alikimbia baada ya kufuatwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana kwa zaidi ya mara tatu nyakati za usiku. 


Baadhi ya wakazi wa Kibiti waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, walisema hali bado ni mabaya na kuiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa matukio hayo. 


“Kila mmoja anahofia yaani hata kwenye shughuli mtu unaogopa kwenda. Kama sasa hivi tuna uchaguzi katika ngazi ya shina na matawi lakini kutokana na haya mauaji watu wanaogopa kujitokeza kugombea,” alisema mmoja wa wakazi hao.

MAUAJI MENGINE


Huu ni mwendelezo wa matukio ya mauaji ya watu mbalimbali wakiwamo askari wa Jeshi la Polisi, viongozi wa vyama na Serikali za vijiji mkoani Pwani.


Kwa mujibu wa rekodi za matukio ya mauji katika mkoa huo mpaka sasa zaidi ya watu 30 wameuawa.

Tukio la hivi karibuni ni lile lililotokea Mei 13 mwaka huu ambapo Katibu wa CCM Kata ya Bungu, Wilaya ya Kibiti, Halife Mtulia, alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka uani.


Aprili 14 mwaka huu, askari nane waliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti.
Januari 19, mwaka huu, mjumbe wa serikali ya kijiji cha Nyambunda , Oswald Mrope, aliuawa baada ya kupigwa risasi mbele ya familia yake. 


Februari 3, 2017, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka. 


Februari mwaka huu, watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi. 


Machi Mosi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa.
Aprili 29 mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Mgomba Kaskazini, Kata ya Mgomba, Ikwiriri, Hamad Malinda, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.  


Mei 5, mwaka huu kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 
Oktoba 24, 2016 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu, alipigwa risasi na kufa na Novemba 6, 2016 Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyang’unda Kijiji cha Nyambunda, Mohammed Thabiti alipigwa risasi akielekea kwake. 


Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi, mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio. 


Katibu wa CCM Wilaya ya Kibiti, Zena Mgaya, alikaririwa na vyombo vya habari akisema Kijiji cha Nyambunda Kata ya Bungu kimeshapoteza Mwenyekiti, Mtendaji na wenyeviti watatu wa vitongoji vilivyoko katika kijiji hicho. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles