31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

GWAJIMA: POLISI WANANISUMBUA

*Wazingira nyumbani yake, agoma kufungua mlango


Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi kwa mara nyingine jana lilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata na kuthibitishwa na Askofu Gwajima mwenyewe, zinaeleza kuwa polisi walifika nyumbani kwake wakiwa katika gari lao.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi hao walipojaribu kutaka kuingia nyumbani kwa askofu huyo, walizuiwa mlangoni kwa sababu hawakuwa na kibali chochote wala maelezo yanayojitosheleza ya kutaka kukutana na kiongozi huyo wa kiroho.

Akizungumza kwa simu na MTANZANIA jana, Askofu Gwajima alikiri polisi hao kumfuata nyumbani kwake na hivyo kulazimika kumtafuta wakili wake mara moja.

“Ni kweli walikuja wakiwa na gari la polisi, lakini walipofika nami nilimpigia mwanasheria wangu ambaye aliniambia tuwaulize wametumwa na nani na kama wana ‘search warrant’ (kibali cha kufanya upekuzi) au ‘arrest warrant’ (kibali cha kukamata),” alisema.

Askofu Gwajima alisema walipowauliza, walimtaja Afande Kingai kama ndiye mtu aliyewatuma, lakini hawakuwa na kibali chochote.

Kwa mujibu wa Askofu Gwajima, mwanasheria wake alifanya mawasiliano ya simu na Afande Kingai ambaye amepewa jukumu la kuwafuatilia wale wote waliotuhumiwa katika sakata la dawa za kulevya na kumuuliza sababu za kumfuata nyumbani.

“Afande Kingai amemweleza mwanasheria wangu kuwa walikuwa wamekuja kwa ajili ya ‘observation’ (uangalizi) tu, kwa hiyo mwanasheria wangu akasema kama ni ‘observation’ tu tusiwaruhusu kuingia ndani kwa sababu sheria ya hivyo hakuna, na sisi tumewazuia hawakuingia ndani,” alisema Askofu Gwajima.

Alipoulizwa kama kufuatwa kwake sasa na polisi kuna uhusiano wowote na kauli alizozitoa kanisani kwake hivi karibuni kuhusu elimu ya Paul Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema huenda ikawa hivyo, lakini akasisitiza kuwa hana uhakika kwa sababu hajazungumza na askari waliomfuata.

Na alipoulizwa kama anadhani ujio huo pia unatokana na andiko ambalo linasambaa kwenye mitandao ya kijamii ambalo linasema Jumapili ijayo mwalimu aliyemfundisha mtu mmoja anayetajwa kwa jina la Bashite atakuwapo kanisani kutoa ushuhuda, Askofu Gwajima alikana akisema andiko hilo si lake.

Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alikwenda mbali na kuhoji: “Hata kama ni kweli, sasa unaogopa mwalimu kuja… kanisani kwangu wapo watu wengi waliosoma naye Bashite kuanzia shule ya msingi na Sekondari ya Pamba… vyeti kama huna huna tu.”

Alipoulizwa haoni kauli yake kwamba Rais Magufuli ni tofauti kabisa na Makonda ilikuwa na nia ya kuwatenganisha viongozi hao, Askofu Gwajima alisema aliyemtaja kwa kumshambulia ni Makonda na si Rais.

“Aliyenitaja kwa kunishambulia katika sakata la dawa za kulevya ni Makonda na si Rais, mimi nimemuongelea Makonda, mimi ni mtumishi wa Mungu siwezi kuongozwa kwa ‘speculation’, si unajua hata Yesu alisema kama wewe huna dhambi basi uwe wa kwanza kushika jiwe,” alisema Askofu Gwajima.

Alipoelezwa kuwa katika mahubiri yake ni kama anaonekana kumshtaki Makonda, askofu huyo alisema: “Nilisema nitamshtaki kwa mahakama iliyo juu yake na nilisema Makonda aombe radhi, angekuwa mstaarabu baada ya sakata lile yeye mwenyewe angenipigia simu na kuniambia Gwajima nilikengeuka, lakini hajafanya hivyo.”
Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alisema kwa aliyoyafanya Makonda tayari amekwishamsamehe na ndiyo maana hajampeleka mahakamani.

Baada ya kupata taarifa za polisi kuzingira nyumbani kwa Askofu Gwajima, MTANZANIA lilifika katika eneo hilo lakini walikuwa wameshaondoka, huku kundi la walinzi la askofu huyo likiongezeka.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alipotafutwa na MTANZANIA ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, simu yake iliita bila kupokewa kwa muda mrefu.

Jumapili iliyopita, Askofu Gwajima aliibuka na madai mapya dhidi ya Makonda kwamba anatumia cheti cha kidato cha nne ambacho si chake.

Katika mahubiri yake yaliyofanyika kanisani kwake, ambako alizungumza na waamini wake huku akiwaita ni wanafamilia yake, Askofu Gwajima alidai kuwa anao ushahidi wa kutosha kuwa Makonda alitumia vyeti visivyo vyake.

Akizungumza kwa kujiamini kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Askofu Gwajima alisema mkuu huyo wa mkoa jina lake halisi ni Daud Bashite na si Paul Makonda kama alivyodai, kauli ambayo imezua mjadala mkubwa mitandaoni.

Februari 8, mwaka huu, Makonda alitaja orodha ya watu 65 aliowataka kuripoti polisi akiwahusisha na dawa za kulevya.

Orodha hiyo ya Makonda ambayo iliweza kutafsiriwa kuwa ni taa nyekundu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, imekuja ikiwa ni mwaka mmoja na miezi mitatu tangu Rais Magufuli kuhutubia Bunge na kuahidi kupambana na wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles