26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

GWAJIMA AZINDUA OPERESHENI MPYA

*Makonda avunja ukimya, aapa kutorudi nyuma


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amezindua operesheni mpya aliyoipa jina la ‘Operesheni 81Mzizima’ huku akimtaka mtu anayeitwa Daud Bashite ajitokeze hadharani kuthibitisha uhalali wa vyeti vyake.

Hivi karibuni, Askofu Gwajima alihubiri kanisani kwake na kusema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anatumia vyeti vya mtu anayeitwa Paul Christian, wakati jina lake halisi ni Daud Albert Bashite.

Akizungumza wakati wa ibada kanisani hapo, Ubungo jijini Dar es Salaam jana,  Askofu Gwajima alisema operesheni hiyo mpya ni vita ya mwisho ya kumshikisha mtu adabu.

Alisema, tangu aanzishe hoja hiyo, hadi sasa wahusika hawajajitokeza hadharani kujibu tuhuma hizo, jambo ambalo alisema linaonyesha alichokisema ni kweli.

“Tangu niibue hoja ya Makonda anatumia vyeti vya Daud Albert Bashite, hakuna aliyejitokeza hadharani kukanusha madai yangu.

“Mimi naamini nilisema ukweli kwani kitendo cha kukaa kimya kinaonyesha wazi kuwa ni kweli ninachokisema na kama anabisha, aje hadharani kukanusha akiwa na vyeti vyake na mimi nitakuja na vyangu…

“Kuna baadhi ya watu wananisihi sana niache kumchambua eti wanasema, Gwajima acha, hiyo inatosha.

“Mbona wakati Makonda aliponihusisha na dawa za kulevya hakuna aliyejitokeza kumwambia aache?

“Hii ni vita ya mzizima ya kushikisha adabu iitwayo hold the final battle of good manners,”alisema Askofu Gwajima.

“Hizi ni salamu tu ili ajue kuwa ukimshambulia baba wa imani, hauwezi kubaki salama kwa sababu viongozi wa dini wanapigana vita mbalimbali ikiwamo majini na mashetani, lakini wanashinda kwa jina la Yesu.

“Nina uhakika na nina ushahidi usio na shaka kuhusiana na suala hilo, labda ajitokeze na kuniomba msamaha.

“Nina material na mazagazaga kibao kuhusu Daud Bashite, niseme,” alihoji Gwajima huku waumini wake wakiitikia semaaa.

“Lakini, kwa leo sitaki nimwongelea sana, kwa sababu namwonea huruma, ila ninachotaka kumwambia ni kwamba, usiweke miguu yako kwenye mashine ya kusaga na kukoboa, utageuka sembe.

“Akumbuke kuwa, baba wa familia akiguswa, hata watoto wanaamka, ndicho kilichojitokeza katika maisha yangu kwani baada ya kushambuliwa sana, waumini wameongezeka tofauti na awali.

“Hata wale waliokuwa hawaji kanisani, hivi sasa wanakuja,”alisema. Katika mahubiri hayo, Askofu Gwajima alisema kuna wakati Mungu huwainua watu wake kwa makusudi maalumu ili kutimiza kusudio lake.

“Sasa nataka kumwambia kuwa, hizi ni salamu tu, nimerusha ka kipande tu… kuhusu Bashite, lakini kelele kibao.

“Hapa sitaki maigizo wala ngonjera, ninachotaka ni samahani tu, lakini anapaswa kujua kuwa, ukimshambulia baba wa imani, awe askofu, mchungaji, padri au wa dini yoyote, hauwezi kubaki salama, lazima na wewe utashambuliwa tu,”alisema.

Pamoja na hayo, alisema kama ataamua kukaa kimya kama anavyoombwa na baadhi ya watu, akikaa kimya Mungu atawainua watu wengine ili waweze kuzungumza kwa niaba yake.

Kwa mujibu wa Gwajima, hana nia ya kumchafua mtu kwenye suala hilo wala hana mgogoro na hana tatizo, ila aliamua kusema alichokisema kwa sababu alichokozwa.

“Nilichokozwa na siwezi kunyamaza kwa sababu ninachokisema ni kweli na wala hakiwezi kubadilika leo, kesho wala keshokutwa.

“Sijawahi kumpiga mtu bila  kunichokoza na wala sijawahi kumchokoza muumini wangu kanisani, awe muislamu au mtu mwingine.

“Sisi ni wakristo, lakini waislamu ni ndugu na marafiki zetu. Hivyo, basi hakuna mshale utakaoweza kunipiga mimi na vita kwangu haijaanza leo wala jana,”alisema.

Pia, Askofu Gwajima alisema ana historia ndefu inayoanzia Oktoba 21, mwaka 1996 wakati alipoanzisha kanisa lake na kupitia changamoto mbalimbali ambazo alizishinda kwa nguvu za Mungu.

Alisema kwamba, hadi sasa ana makanisa 400 yaliyopo maeneo mbalimbali ndhini na mengine 300 yaliyopo katika nchi mbalimbali duniani.

Katika mabuhiri hayo, Askofu Gwajima alimtolea mfano Erick Shigongo kwa kile alichosema kuwa ni miongoni mwa watu wa kuigwa kwani wanatafuta mafanikio kadri wawezavyo.

“Mtu ukipata mafanikio kunakuwa na chuki kibao zinazotolewa ili wakuvunje moyo badala ya kukaa na kuanza kutafakari ili kuona umewezaje ili wakuige.

“Mwisho naamini utafiti unapingwa kwa utafiti, hivyo basi kauli yangu kwa Daudi itapingwa kwa vielelezo ili na mimi niweze kutoa vielelezo vyangu,” alisema Askofu Gwajima.

Wiki iliyopita Jeshi la Polisi kwa mara nyingine lilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi.

Polisi hao walipojaribu kutaka kuingia nyumbani kwa askofu huyo, walizuiwa mlangoni kwa sababu hawakuwa na kibali chochote wala maelezo yanayojitosheleza ya kutaka kukutana na kiongozi huyo wa kiroho.

Makonda avunja ukimya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema haumizwi na maneno ya watu kwani hizo ni dalili kwamba kazi anayoifanya inalipa.

Makonda ameifananisha vita ya kupambana na dawa za kulevya sawa na vita vya ulimwengu wa roho ambavyo havipaswi kupiganwa kienyeji.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam  katika ibada Usharika wa Kimara (KKKT), alisema hatakaa kimya na kwamba ataendelea na mapambano hadi aikamilishe kazi aliyotumwa na Mungu hapa duniani.

“Hizi ni dalili kwamba kazi ninayoifanya katika ulimwengu wa roho inalipa, hakuna aliyemcha Mungu anayeweza kuacha kusimama katika kusudi zuri ambalo Rais wetu ametuelekeza akabaki kupiga kelele hizo ndogondogo.

“Sijui kama unafahamu baba mchungaji wamefikia hatua ya kusema sasa hata mke wangu si raia wa Tanzania…vita hii haipiganwi kienyeji ni lazima uwe umekaa sawasawa,” alisema Makonda.

Alisema historia ya vita vya dawa za kulevya haijawahi kumuacha mtu salama ndani ya Taifa na kwamba hata sasa maswali yamekuwa mengi juu yake.

“Kila aliye jaribu ama alikufa, alifungwa, alipata kila aina ya msukosuko na hatimaye jambo hilo likafanya waovu, wauaji wapate mali kwa njia isiyokuwa halali. Wakapata nguvu na kutengeneza hofu ya kwamba yeyote yule ajaribuye kushughulika nao atashughulikiwa.

“Ndio maana mara kadhaa nimekuwa nikisema ni lazima uwe unamjua Mungu, uwe na uhakika na Mungu unayemwamini na kama huna uhakika usithubutu kuingia kwenye mapambano haya,” alisema.

Aliwabeza wanaoendelea kumjadili na kusema kuwa ukuu wa mkoa si tatizo bali hoja ni namna gani ameitumia nafasi aliyopewa kutekeleza kusudi la Mungu hapa duniani.

“Maswali yamekuwa mengi juu ya njia lakini unapotaka kuwavusha watu kwenda ng’ambo ya pili hakuna mjadala juu ya njia.

“Kuwa mkuu wa mkoa si tatizo, tatizo umeikamilishaje kazi ya Mungu aliyokupa hapa duniani, hapa tuko kwenye vita na vita hii si ya ulimwengu wa mwili bali ni ya ulimwengu wa roho.

“Wananchi wa wamechanganyikiwa, kila wakipita mahala wanaona watoto wanatumia dawa za kulevya na wakiangalia nyuma wanaona wale wauzaji wakubwa hawashikiki, wanatisha, hawajui wapite wapi,” alisema.

Alisema Jiji la Dar es Salaam ndilo lango kuu la uchumi ambapo asilimia 80 ya mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatoka Dar es Salaam. Hata hivyo limekuwa lango la uchumi mbadala wa kuingizia dawa za kulevya na kuangamiza taifa.

“Rais hawezi kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari ama kuwakopesha watoto wasome halafu wakaendelea kuvuta bangi ama kutumia dawa za kulevya je, ni mzazi gani mwenye akili timamu atakaye furahia hilo, kiongozi gani mwenye ufahamu wa kimungu anayefurahia hilo?

“Mcha Mungu gani anaweza akakaa kwenye mkoa kama huu akaruhusu madawa yapite halafu watoto wanateketea, mcha Mungu anaweza akaruhusu uovu uendelee kutawala halafu anajiita anamtumikia Mungu?

“Mcha Mungu gani huyo…nikisema mtamjua, sikatai dini yake na wala sitaruhusu akatize katika anga la utawala nililopewa, nimepewa bendera ya Tanzania, nimepewa mamlaka nina ‘operate’ kutoka kwenye mamlaka ya juu sana. Nitasimama hadi mwisho kuhakikisha jina lipitalo majina yote linainuliwa,” alisema Makonda huku akishangiliwa.

Mara kwa mara katika mahubiri yake alikuwa akitoa mifano kwa kutumia baadhi ya maneno kutoka katika kitabu cha Biblia na kushangiliwa na waumini wa usharika huo.

“Vita tuliyonayo ni kazi ya mauti na uzima, kuhakikisha tunamtoa mtoto fulani kwenye makucha ya shatani na hii kazi yesu alishaifanya…ukitaka kujua kaifanya wapi soma.

“Shetani anafitinisha, anachonganisha, anaharibu, anateketeza lakini yesu amekuja kurejesha kilichopotea na ndio kazi tunayoifanya sisi,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na PATRICIA KIMELEMETA,  CHRISTINA GAULUHANGA na NORA DAMIAN (DAR)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles