26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

GRACE MUGABE: HATUA MOJA MBELE KUELEKEA URAIS

BADO sijafahamu nimweke fungu lipi Mke wa Rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe.  Bado sijajua kama nimweke kwenye fungu la wanawake jasiri wasioogopa nguvu za wanaume, au mtu anayetumia karata ya kuwa mwanamke ili aupate urais, wakati haustahili.

Ninayasema haya kutokana na mwenendo wake wa muda mrefu, kutoka kuwa Katibu Muhtasi wa Rais Mugabe, hadi kufikia hatua ya kuchungulia kiti cha urais, ambacho huenda akakipata kama ataendelea kuhofiwa kama ilivyo sasa.

Tukio la hivi karibuni ambalo Grace Mugabe amefanikiwa tena, ni kufukuzwa kwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangangwa.  Mnangangwa amefukuzwa kazi na Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, ambaye ni Mume wa Grace.  Rais Mugabe ametumia mamlaka yake ya kikatiba kumuondoa madarakani Makamu wake huyo, akidai kwamba anamuondoa kutokana na “kuendelea kuonyesha kutokuwa na uaminifu, kutokuwa na heshima, kutokuwa mkweli na kutosimama kwenye misingi.”

Sawa, Rais Mugabe ameyasema hayo.  Hata hvyo, si siri hata kidogo kwamba Makamu huyo wa Rais alikuwa akipigwa vita kali na Grace Mugabe na kiini chao cha kuwa na msuguano ni urais.  Urais kwa maana kwamba inasemekana Mnangangwa alikuwa na mipango ya kugombea urais kupitia chama cha ZANU-PF, wakati akijua fika kwamba Grace naye macho yake yote yapo kwenye kiti hicho.

Ilifikia hatua wawili hao walikuwa wakikashifiana vibaya na kusingiziana makubwa.  Grace mwenyewe alikuwa akimtuhumu Makamu huyo kwa kutaka “kumpindua” Mume wake.  Makamu huyo juzi alitoa kauli kwamba aliwahi kula ice cream zinazotengenezwa na kampuni ya mwanamama huyo na zilimuumiza tumbo.

Kwa kutumia cheo chake cha U-first lady na kile cha Mwenyekiti wa Wanawake ndani ya ZANU-PF, Grace alikuwa akisema hadharani kwamba Makamu huyo wa Rais anatakiwa kufukuzwa kazi.  Wengi tulikuwa tukijiuliza sababu hasa za hatua ya kufukuzwa kazi, kwani suala la kutolea macho kiti cha urais halina ubaya wowote.  Hata hivyo, huenda kwa Zimbabwe ukitolea macho kiti ambacho Grace naye anakitolea macho, basi ni kosa.

Ni Grace Mugabe huyu huyu ambaye mwaka 2014 alisababisha aliyekuwa Makamu wa Rais, Joice Mujuru, kufukuzwa kazi.  Sababu ya kweli: kuutaka urais.

Ni Grace Mugabe huyu huyu ambaye watu wanaofuatilia siasa za Zimbabwe, wanadai kwamba anamzuia mumewe kung’atuka.  Mugabe ana umri wa miaka 93, lakini badala ya kung’atuka ili kiti hicho kichukuliwe na mtu mwingine, ameendelea kugombea na ameshateuliwa na chama chake cha ZANU-PF kugombea tena kiti hicho mwaka kesho.

Wapo wanaosema kwamba Grace hataki mumewe aondoke kwenye kiti hicho, kwani anahofia kwamba mali walizonazo ndani na nje ya nchi hiyo zitataifishwa na pia huenda akashitakiwa kutokana na makosa mbalimbali ya kiutawala ambayo amekuwa akijihusisha nayo kwenye utawala wa mumewe.

Ni Grace huyu huyu pia ambaye katika miezi ya hivi karibuni alikuwa akimlazimisha mumewe atamke mrithi wa kiti chake cha urais atakuwa nani, kwa madai kwamba asipomtaja mrithi huenda kukatokea mgogoro mkubwa ndani ya ZANU-PF pindi Mugabe atakapoondoka.  Rais Mugabe mwenyewe alishakataa kumtaja mrithi wake na kusisitiza kwamba wananchi wa Zimbabwe ndio watakaochagua wanayemtaka kuwaongoza.

Hatuna uhakika kama kauli hiyo ya Mugabe ni ya kumaanisha, au alizungumza tu kwakuwa hakutaka kuonekana kumpendelea moja wa moja Mke wake na kukubaliana na kila anachokitaka.  Hata hivyo, tunachokijua ni kwamba licha ya hayo yote, bado Grace amekuwa ama akifanya maamuzi mengi sana, au akichangia kufanyika kwa maamuzi mengi makubwa ya kiutawala, kiasi cha watu kujiuliza anayeiongoza Zimbabwe hasa ni nani?

Naam. Huyo ndiye Grace Mugabe, Mwanamama mwenye ujasiri mkubwa na mwenye kuhofiwa sana na viongozi pamoja na watu wa kawaida nchini Zimbabwe.  Dunia nzima inatambua kwamba Grace ni Mwanamama ambaye ukipingana naye, ukifanya yale yasiyo mapenzi yake, basi atafanya lolote kuhakikisha anakumaliza kisiasa.  Huyu ndiye mtu anayeutaka Urais wa Zimbabwe ambao mumewe amekuwa nao tangu mwaka 1987, na ndiye mtu ambaye amechangia kuifikisha Zimbabwe mahala ilipo hivi sasa.

Kama unaiona Zimbabwe ni nzuri, basi Grace Mugabe amechangia kwa kiasi kikubwa na kama unaiona yenye changamoto kubwa, basi ni sababu ya matakwa ya Grace Mugabe. Unaweza kupima mwenyewe. Ni kazi kwa Wazimbabwe kuamua kama huyu ndiye wanayemtaka kuwa Rais wao, maana akiwa Rais, basi Zimbabwe ya sasa ndivyo itakavyoendelea kuwa hivyo hivyo kwa miaka yote ya utawala wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles