33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

GARI LA WAGONJWA LAKAMATWA NA MAGUNIA 34 YA MIRUNGI

Na SHOMARI BINDA -MUSOMA


JESHI la Polisi Mkoa wa Mara, limekamata gari la kubeba wagonjwa (ambulance) aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba DFPA 2955 mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, likiwa limebeba magunia 34 ya dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilo 821 yakisafirishwa kwenda mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, alisema tukio hilo lilitokea Julai 10, mwaka huu saa 10 jioni katika eneo la Bitaraguru, Kata ya Kabasa wilayani Bunda.

Alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na George Matai, ambaye ni mwajiriwa wa halmashauri akiwa na mkazi wa Sirari, Ruda Joseph, wakitoka Kijiji cha Nyanchabakenye, wakiwa wamebeba mirungi hiyo.

Kamanda Ndaki alisema polisi walilikuta gari hilo limeegeshwa eneo la Bitaraguru na walipolifikia na kulichunguza, walikuta likiwa limebeba mirungi.

Alisema dereva na abiria wake walikamatwa kwa mahojiano zaidi.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hili na wapo watu ambao tutawahoji kwa kuwa gari hili ni mali ya Serikali na pale uchunguzi utakapokamilika wahusika wote tutawafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Ndaki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo linazidi kuchafua taswira ya mkoa wake na kuendelea kuonekana ni eneo lenye matukio ya ajabu.

Alisema wakati wagonjwa wakiwa na uhitaji wa magari kuwafikisha kwenye maeneo ya kupata huduma, watumishi wasio waaminifu wanayatumia kushiriki kufanya kazi ambazo hazihitajiki na kushiriki kuwaharibu vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.

Alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kulikamata gari hilo na kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa kweli wapo watumishi ambao ukiwafikiria unashindwa kupata majibu ya kutosheleza, wakati mama wajawazito wakiwa wanasubiri gari kwa ajili ya kupatiwa huduma, anatokea dereva analitumia gari hilo kwa kutafuta masilahi yake, tena kwa kitu haramu, hili ni jambo ni baya sana,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, aliliomba jeshi hilo litakapomaliza taratibu zake, liliachie gari hilo kwa kuwa limekamatwa kama sehemu ya ushahidi (kidhibiti) ili liendelee kutoa huduma kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles