27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Gambo awatuhumu maofisa elimu kuwahujumu wanafunzi

ELIYA MBONEA-ARUSHA

BAADHI ya maofisa elimu Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, wanatuhumiwa kupanga mbinu chafu za kuhujumu zoezi la uandikishaji wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliita tuhuma hizo kuwa ni mpango wa kuuhujumu mkoa katika sekta ya elimu.

Gambo alizitoa tuhuma hizo jana kwenye ziara yake ya kukagua maendeleo ya sekta ya elimu kuelekea kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Akiwa katika Kata ya Mwandeti wilayani humo, Gambo, aliyeongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa alijikuta akipigwa butwaa baada ya kukuta Sekondari ya Mwandeti haijapangiwa mwanafunzi hata mmoja.

“Kuna matatizo tunaambiwa ya kukosa madarasa, lakini nahisi kuna baadhi ya watu wamepanga kuuhujumu Mkoa wa Arusha. Haiwezakani shule hii ilikuwa na wanafunzi waliomaliza kidato cha nne wameacha madarasa manne tupu tuambiwe kuna uhaba wa madarasa,” alisema Gambo.

Aliongeza kwamba mkoa huo unafanya uchaguzi wa wanafunzi kuingia kidato cha kwanza, cha ajabu hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepangwa kwenye shule hiyo.

“Mimi nahisi kuna watu wamejipanga kuhujumu mpango wa Serikali wa kutoa elimu kwa watu wake, tunakwenda kuwatafuta na tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu.

“Niwahakikishie madarasa manne yaliyobakia ya waliomaliza kidato cha nne, tutahakikisha tunawaletea wanafunzi wote 243 wa kata hii ya Mwandeti, wote watapangiwa shule na watakuja hapa.

“Hapa hakuna shida yoyote ni usanii tu, kuna watu wamepanga kuhujumu zoezi hili. Taarifa zenyewe ukiziangalia Mkurugenzi kutoka kwa watu wako wa chini nyingine ni za kughushi. Ukiangalia pia watu wa mkoani masuala ya elimu na wenyewe nao madarasa yapo lakini wanakataa kuchagua wanafunzi,” alisema Gambo.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Arusha, Nelson Saro, alisema wanafunzi waliokuwa wamefaulu walikuwa ni 6,846 ambapo wavulana walikuwa ni 2,662 na wasichana 3,844.

Alisema ufaulu huo ni wa kipekee kutokana na wanafunzi kufaulu kwa wingi ikilinganishwa na miaka mingine.

“Kati ya hao wanafunzi waliopata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza ni 2,025 na hivyo kusababisha wengine kukosa nafasi,” alisema Saro.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry  Murro, alisema wilaya hiyo ilitakiwa kujenga vyumba 170 kwa Halmashauri ya Meru na Arusha ambapo kwa sasa wapo katika hatua ya kuangalia ni ujenzi gani umekamilika.

“Kati ya shule nne tunazozipambania ziingie kwenye usajili ikiwamo shule ya sekondari Uwiro, Majengo, Oldonyowasi na Losikito kwa sasa zote zipo katika hatua nzuri ya kukamilika,” alisema Murro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles