27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

GAMBO AKWEPA NJIA YA MAKONDA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amesema katika vita ya dawa za kulevya ni muhimu kwa watu wenye taarifa wakazipeleka vituo vya polisi wilaya na mkoa ili zifanyiwe kazi, ikiwamo kuangaliwa kama zina ukweli au si kweli.

Gambo alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, ikiwa ni wiki moja sasa tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aanze vita hiyo kwa kutaja hadharani majina ya watu aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya wakiwamo wasanii, wanasiasa na wafanyabiashara.

Hata hivyo, kitendo cha Makonda kutaja majina hayo hadharani, kilikosolewa na wanasheria na wabunge bungeni kwa hoja kwamba hakufuata taratibu za kisheria.

Gambo, akizungumza wakati akizindua mazoezi yatakayofanyika kila wiki ya pili ya mwezi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakazi wa Arusha kutoa taarifa za dawa za kulevya kwa masilahi mapana ya nchi badala ya kutanguliza tabia za unafiki.

 “Kama una taarifa zozote, nakuomba zipeleke kwa kamanda wa polisi wilaya au mkoa, kwa nafasi zao watazichuja, wataangalia hao uliotaja umetaja kwa ukweli na kwa haki au umetaja kwa sababu ya chuki na unafiki.

 “Isiwe mmenyang’anyana mwanamke mahali halafu unaenda kumchongea mwenzako polisi. Tukijua umechomekea, hakika tutakukamata wewe kwa uongo wako. Nisisitize nendeni mkatoe taarifa za kweli kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Lakini isiwe tabia za kinafiki, mimi siku zote huwa naamini kijana ukiwa mnafiki ukizeeka lazima utakuwa mchawi,” alisema.

Pia Gambo alitumia uzinduzi huo kuueleza umma kuwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha tayari linawashikilia watu kadhaa wanaodaiwa kukutwa na kete za dawa za kulevya.

 “Tumewaambia polisi hawa watu wasiwapeleke mahakamani kwanza, badala yake wakae nao kwanza kwa sababu tunacho kikosi kazi maalumu. Tutakaa nao kimyakimya hadi watuambie wameanzia wapi na wanaishia wapi.

“Kutoa tamko la jambo hili tutalitoa wakati ambao tayari tutakuwa na taarifa zote muhimu za kina na za kutosha,” alisema.

Gambo alisema kwa miaka mingi Arusha imekuwa njia kuu ya kuingia kwa dawa za kulevya aina ya mirungi zikipitia mji wa Namanga uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya.

 “Ni bahati mbaya kwamba katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zipo ambazo mirungi imeruhusiwa kisheria kama ilivyo Kenya, wakati Tanzania kitu hicho kimepigwa marufuku kisheria hii ni changamoto,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles