26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Fursa marais 16 wakitua nchini

Na ANDREW MSECHU –Dar es salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka Watanznaia kuchangamkia fursa zinazotokana na mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), unaotazamiwa kufanyika nchini Agosti.

Akizungumza na wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari jana Dar es Salaam, Profesa Kabudi alisema mkutano huo utawakutanisha viongozi kutoka nchi 16 wanachama ambao wataambatana na ujumbe wa watu zaidi ya 1,000 jambo ambalo ni fursa mpya kwa Watanzania.

“Kufanyika mkutano huu nchini, kuna fursa nyingi kama za utalii, hoteli, usafirishaji, vyakula na nyingine nyingi ambazo zinatokana na uwepo wa ugeni huo mkubwa, ambazo ni vyema Watanzania wajitokeze kuzichangamkia,” alisema.

Alisema fursa nyingine itakayoweza kutumiwa na Watanzania ni kwa soko la Kariakoo kupokea ugeni huo kwa kuwa baadhi ya nchi zinazohudhuria mkutano huo, hulichukulia kama Dubai.

Profesa Kabudi alisema katika ziara ya kimkakati ambayo Rais John Magufuli aliifanya hivi karibuni katika nchi za Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe, walibaini kuwa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika zinaiheshimu Tanzania na Kariakoo inachukuliwa kama soko kuu kwa nchi hizo.

“Tulibaini kuwa wafanyabiashara wa nchi hizi wengi wanaichukulia Kariakoo kama ndiyo Dubai yao, sehemu muhimu ya kuja kuchukua bidhaa mbalimbali, kiasi kwamba nikaanza kupata mashaka kuwa hivi hii Kariakoo ina hadhi inayopewa kweli?” alisema.

Alisema kwa sasa Tanzania ndiyo inayouza bidhaa nyingi katika soko la SADC ikilinganishwa na nchi zote za Afrika Mashariki, hivyo ni vyema kutumia fursa ya mkutano huo kukuza masoko ya bidhaa za ndani.

Kabudi alisema walibaini miongoni mwa bidhaa ambazo zinapendwa sana nchini Malawi ni sabuni aina ya Foma ambazo tayari kuna watu wameanza kutengeneza bandia na kwa bahati mbaya wafanyabiashara wanaozichukua nchini na kwenda kuziuza nje sio Watanzania.

Alisema mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 17 na 18, utatanguliwa na mkutano wa mawaziri na makatibu wakuu wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama, utakaofanyika kuanzia Agosti 9 hadi 16. 

“Hii ni heshima ya pekee kwa Tanzania,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema Julai 22 hadi Julai 26 yatafanyika maonesho maalumu ya maadhimisho ya awamu ya nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC eneo la Mlimani City, ambayo pia yatatotoa fursa kwa Watanzania. 

Kabudi alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa watafutaji wa masoko ya bidhaa, waagizaji na wazalishaji kujua namna ya kufika katika nchi wanachama za SADC na namna ya kushirikiana kibiashara.

Aliwaomba wamiliki, wahariri na waandishi wa habari kutumia nafasi yao kutangaza mkutano huo, kuelimisha wafanyabiashara na wananchi kuhusu namna ya kuchangamkia fursa wakati wa mkutano huo.

“Tunaomba pia vyombo vya habari na wanahabari kuandika habari za SADC kwa uzalendo na kwa ufanisi, pia kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na utulivu kipindi chote cha mkutano huu,” alisema.

Alisema mbali na agenda za mkutano huo, Tanzania itapokea kijiti cha uenyekiti wa SADC kutoka kwa Namibia, ambapo Rais Magufuli atakuwa mwenyekiti kwa mwaka mmoja, nafasi ambayo iliishika miaka 16 iliyopita.

Mkutano kama huu ulifanyika Tanzania mara ya mwisho mwaka 2003/2004 ambapo Rais wakati huo, Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles