29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Funza, buibui na mende, kuwa chanzo kikuu cha protini

MWIGIZAJI mashuhuri wa Marekani, Angelina Jolie, alizua mjadala mkali wakati akiitangaza filamu yake mpya nchini Cambodia baada ya kuonekana akikaanga na kuwala buibui akiwa pamoja na watoto wake.

Mwigizaji huyo anasema walikuwa na ladha tamu sana.

Kula wadudu ni jambo lililohusishwa kwa muda mrefu na uigizaji, katika vipindi vya runinga kama vile I’m a Celebrity… Get Me Out Of Here.

Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2050, idadi ya watu duniani itafikia bilioni tisa.

Ili kuweza kuwalisha, itabidi uzalishaji wa chakula uongezeke maradufu.

Kadiri idadi ya watu duniani inavyoongezeka, ndivyo juhudi za kutafuta njia mbadala za kupata chakula zinaongezeka, hasa cha protini badala ya vyakula vya kawaida.

Hii ni kwa sababu samaki na mifugo, vinaweza visitosheleze tena.

Mpango huu wa wadudu kuchukua nafasi ya samaki na mifugo mingine, inasifiwa na wataalamu wanasema ni endelevu kimazingira, wana virutubisho vingi na wanaweza kupatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu na katika hali nzuri.

“Wadudu ndio chakula halisi chenye virutubisho karibu vyote,” anasema Shami Radia, mwanzilishi mwenza wa Grub, duka linalouza wadudu wanaoliwa nchini Uingereza.

“Wana protini, madini mengi na asidi za amino hivyo, wana faida ukiwala na ni bora kwa mazingira ukilinganisha na ufugaji,” anasema.

Anasema wanaweza kula taka, hawatoi gesi zinazochangia ongezeko la viwango cha joto duniani, hawahitaji maji mengi na huhitaji eneo kubwa la shamba kuwafuga.

Wadudu pia wana kiwango cha juu cha kubadilisha mali ghafi kuwa chakula kwa sababu hawahitaji kudhibiti joto katika miili yao kwa kutumia damu kama wafanyavyo mifugo na wanyama wengi.

Kwa kawaida, wadudu wanaweza kubadilisha kilo mbili za lishe kuwa sehemu ya mdudu.

Ng’ombe atahitaji kula lishe ya kilo nane ndipo aweze kuongeza kilo moja katika uzani wake.

Ni wadudu wa aina gani wanaoliwa?

Shirika la Chakula Duniani (FAO), linasema kuna takribani aina 1,900 za wadudu wanaoweza kuliwa duniani.

Wadudu hao ni pamoja na mende, viwavi, nyuki, nyigu, nzige, jamii ya funza, kumbikumbi, nge, vipepeo na kerengende.

Licha ya kwamba wadudu hawa wanapatikana kwa wingi, ni aina chache wanaoliwa na jamii za Afrika Mashariki.

Grub wanaamini bado itachukua muda kwa watu kukubali kuwala buibui na nge kama alivyofanya Angelina Jolie.

Lakini pia tafiti zimeonesha kuwa maziwa ya mende ni chanzo bora cha protini.

Mende huchukiwa na watu na huhusishwa na uchafu na maradhi. Lakini wanapaswa kutambua wadudu hawa wana manufaa makubwa kwa binadamu.

Wengi huenda wakawa hawawezi kuwavumilia, hata walau kuwatazama, lakini wanasayansi wakiwamo wa nchini India wanasema huenda mende wakatoa tumaini kwa binadamu, katika lishe miaka ijayo.

Wanasayansi hao wamegundua kwamba chembe za protini za maziwa kwenye mende zina virutubisho vingi mno.

Wanasema vinaweza kutumiwa kama tembe ama chakula chenye virutubisho vya protini kwa kiwango cha juu.

Wanasayansi katika taasisi ya sayansi ya seli katika Mji wa Bengaluru nchini India, wamefanya ugunduzi huo baada ya kutafiti muundo wa chembe za protini zinazopatikana katika utumbo wa mende aina ya Diploptera puncata, ambao ndio pekee hujifungua.

Ingawa mende wengi kwa kawaida hawatoi maziwa, mende aina ya Diploptera puncata huwa wanatengeneza aina fulani ya maziwa yenye protini kwenye utumbo, ambayo hutumiwa kulisha watoto wake.

Chembe moja ya protini hiyo inakadiriwa kuwa na kiwango mara tatu cha nguvu ya mwili ikilinganishwa na kiasi sawa cha maziwa ya nyati.

Aidha, chembe hizo zina nguvu mara nne kushinda maziwa ya ng’ombe.

“Ni chakula kamili, unapata protini, mafuta na sukari,” amenukuliwa mmoja wa watafiti waliohusika na utafiti huo, Sanchari Banerjee.

Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika jarida la utabibu la International Union of Crystallography.

Anasema kwa kutumia ufahamu wao wa muundo wa protini hizo, wanaweza kutumia hamira kuzalisha chembe kama hizo kwa wingi kwenye maabara.

Isitoshe, anasema muundo wa chembe hizo unaonesha matumaini kwamba zinaweza kuundwa na kutumiwa katika vidonge vya dawa.

Aidha, wanasayansi kwa miaka mingi wamekuwa wakishangazwa na uwezo wa mende kukaa muda mrefu maeneo yenye sumu na uchafu bila kudhurika. Wamegundua kwamba huwa wanatoa kemikali za kupigana na sumu.

Wanaweza kusaidia katika kutengeneza dawa za kusaidia binadamu kukabiliana na bakteria zinazosumbua watu kama E. Coli na MRSA ambazo zimekuwa hazisikii dawa.

Hii si mara ya kwanza mende kutumiwa kwa sababu za kimatibabu. Mwanahabari Lafcadio Hearn, karne ya 19 alipitia maeneo ya kusini mwa Marekani na kuripoti jinsi watu wenye pepopunda walivyokuwa wakipewa chai iliyotengenezwa kwa kutumia mende.

“Sijui ni mende wangapi hutumiwa hadi upate kikombe cha chai, lakini wakazi wa New Orleans, nchini Marekani wana imani na tiba hii,” anaandika.

Leo katika hospitali kadhaa nchini China, krimu inayotengenezwa kwa kutumia ungaunga wa mende waliosagwa hutumiwa kutibu vidonda vya moto, pia humezwa kutibu ugonjwa huo.

Mende wanahitajika kiasi kwamba Wang Fuming aliamua kufungua biashara ya kuwafuga eneo la Shandong, Mashariki mwa China.

Huwa anafuga mende milioni 22 kwa wakati mmoja. Anasema tangu mwaka 2010, bei ya mende waliokaushwa imepanda mara 10.

Aidha, nchini humo mfanyabiashara mwingine Matilda Ho amekuwa akiendesha kampeni za kula wadudu ili kuimarisha tabia za kula chakula bora nchini humo.

Alizungumza katika mkutano wa Teknonolojia, utumbuizaji na mitindo kuhusu umuhimu wa kusambaza ujumbe wa chakula chenye afya.

Anaunga mkono vyakula ikiwamo vile vilivyo na protini kutokana na wadudu aina ya viwavi.

China ina tatizo la ukuaji kutokana na kunenepa kupitia kiasi na ugonjwa wa kisukari unaosababishwa na staili mbaya ya ulaji.

Mtu mmoja kati ya raia wanne wa China anaugua ugonjwa wa kisukari na mmoja kati ya watu wanne amenenepa kupita kiasi.

Makala haya yameandaliwa na mwandishi wetu kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles