23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Foleni siku mbili kupata maji Kiteto

Wanawake jamii ya wafugaji wakisubiri kuchota maji
Wanawake jamii ya wafugaji wakisubiri kuchota maji

Na MOHAMED HAMAD-MANYARA

WILAYA ya Kiteto ilizinduliwa mwaka 1974, wakati huo kulikuwa na idadi ya watu 12,000, hivi sasa idadi ya watu imeongezeka na kufikia zaidi ya 240,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Wakati wilaya inazinduliwa maji yalitosha kulingana na idadi ya watu waliokuwepo na waliweza kufanya  shughuli za maendeleo, tofauti na ilivyo sasa ambapo wakazi wengi wanalazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo.

Hali hii imekuwa tishio kubwa kwa familia na wananchi wa Kibaya hasa wa vijijini ambao vipato vyao vinaishia kununua maji,
huku kukiwa na mahusiano mabaya kati ya wanandoa kufuatia huduma hiyo ambayo inapatikana kwa  taabu kubwa.

Viongozi wilayani Kiteto wamekuwa wakilalamikiwa kwa kushindwa kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi, huku kukiwa na ahadi zisizotimia kuwa Serikali iko mbioni toka kuzinduliwa mwaka 1974 hadi leo 2016.

Wilaya hiyo ina uwezo wa kujimudu kwa maji safi na salama kwa asilimia 36 vijijini na asilimia 37 mjini.

Pia miundombinu inayotumika bado ni ile ya mwaka 1974 kama matenki na mabomba licha ya jitihada zinazofanywa kubadilisha, zikilenga kuondoa adha hiyo bado hali hiyo imekuwa tishio.

Urasimu nao umetajwa kuwa kikwazo cha huduma hiyo ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ally Mohamed Shein ambaye kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, aliwahi kuzindua tanki la lita 300,000 mjini Kibaya na baada ya kuondoka halikuweza kuingiza maji.

WANANCHI

Asha Issa mkazi wa Kaloleni, anasema wakati mwingine huwa wanapanga foleni kwa siku mbili ili kuweza kupata maji.

“Tunaamka alfajiri tunaacha watoto nyumbani kwa ajili ya kwenda kutafuta maji, lakini unaweza kushinda siku nzima na maji usipate kwa sababu foleni inakuwa kubwa…unaweza kupanga foleni siku mbili ndio unapata maji,” anasema Issa.

Anaiomba Serikali kuhakikisha inatatua kero ya maji kutokana na ukubwa wa tatizo hilo ambalo linawagharimu na hivyo kushindwa kuendesha maisha yao na familia zao.

Naye Elias Kona mkazi wa Kijungu, anasema ndoo moja ya maji katika maeneo ya vijijini huuzwa kati ya Sh 500 mpaka 700 huku maeneo ya mijini ikiuzwa kati ya Sh 100 hadi 300.

“Tunashindwa kufikia malengo yetu kwa kutumia muda na fedha nyingi kusaka maji. Hali huwa mbaya zaidi kuanzia Julai hadi Desemba kwani maji huwa machache kutokana na ukame.

“Angalau mvua ikinyesha huwa kuna nafuu lakini kiangazi tunapata taabu sana, tunatembea umbali mrefu kutafuta maji na kushindwa kufanya shughuli zetu zingine,” anasema Kona.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Dongo, Elia Dengea (CCM) anasema, kuna kila sababu ya kufanyika utaalamu kwa kina katika maeneo ya Kiteto hasa kata yake ambako walichimba maji zaidi ya mara sita bila mafanikio.

“Hali hii imekuwa tatizo kubwa hakuna mwananchi anayemwamini kiongozi, wanasema tutakutana kipindi cha uchaguzi,” anasema Dengea.

Naye Diwani wa Kata ya Matui, Kidawa Othman (Chadema), anasema tatizo lililopo ambapo kwa sasa linagharimu wananchi kuhusu sekta ya maji ni kukosa watumishi wa Serikali ambao ni waadilifu akisema kuna hujuma nyingi zinafanyika huku kukiwa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Anasema katika eneo lake wananchi wanatumia maji ya visima vifupi vya kuchimbwa kwa mkono ambavyo si salama kiafya.

Mbunge wa Viti maalumu Manyara, Esther Mahawe (CCM), alilazimika kwenda kumuomba Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe, kuja kutembelea katika Mkoa wa Manyara kujionea hali ilivyo katika upatikanaji wa maji.

Anasema, Serikali haina budi kutatua kero ya majini hasa vijijini kwani hali ni mbaya kwa wananchi.

“Wananchi wanatumia muda mwingi kutafuta maji kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo. Naibu Waziri umejionea mwenyewe hali ilivyo, tunaomba msaada wako ili kusaidia akina mama wa Kiteto na Manyara wanaotaabika kila kukicha,” anasema Mahawe.

Naye mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian (CCM), anaiomba Serikali kuendelea na jitihada za kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi ili wananchi wawe na imani na viongozi waliopo madarakani, na kuwasihi wananchi kutunza miradi katika maeneo yao.

Anasema kukosekana kwa vyanzo vya maji vya uhakika kumechangia kuwapo kwa uhaba mkubwa wa maji.

“Visima vingi vinapochimbwa huwa havitoi maji, tunawaomba wataalamu wa maji waliobobea waje Kiteto kusaidia wananchi ambao wanataabika,” anasema Papian.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wilayani hapo, vyanzo vya maji vilivyopo ni visima virefu 74, visima vifupi 8, chemchem 6, mabwawa makubwa 5, mabwawa madogo 36 na matenki ya kuvunia maji ya mvua 80.

HALI ILIVYO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto, Tamimu Kambona, anasema kumekuwa na ongezeko la gharama katika baadhi ya hivyo kuna uhitaji mkubwa wa fedha ili kukamilisha miradi ambayo imekwama na kusababisha wananchi kupata adha kubwa ya maji.

Kulingana na Mkurugenzi huyo, baadhi ya miradi ilikuwa inatumia mifumo ya jua na kwamba linapokosekana upatikanaji wa maji huwa mgumu. Anasema lengo la Serikali ni kutekeleza sera ya kuwa wananchi wayafikie maji mita 400 pawe kituo, akisema kwa sasa makusanyo yameongezeka sambamba na kuzuia mianya ya wizi Serikalini hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa sera hiyo ambayo kila Mtanzania anatufaika nayo.

Kwa mujibu wa Kambona, miradi ya maji mjini Kibaya na Kaloleni, imetekelezwa kwa asilimia 75 ambapo kazi zilizofanyika ni
usanifu wa mradi, kufungwa mfumo wa nishati ya jua, kufungwa pampu moja, kulazwa mabomba na kufukiwa mitaro.

Mradi mwingine ni wa umwagiliaji uliopo Kijiji cha Orgira Kata ya Sunya, ambao umefikia hatua za mwisho za utekelezaji, uchimbaji wa kisima ulikamilika, ufungaji wa pampu, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, ujenzi wa kituo cha kunyweshea mifugo, pamoja na ujenzi wa tanki la maji na miundombinu yake.

NAIBU WAZIRI WA MAJI

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe, hivi karibuni alitembelea miradi ya maji na umwagiliaji mkoani humo na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati wa kumaliza kero za maji katika mkoa huo ifikapo mwaka 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles