24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Finland yatarajia kuwa na Waziri Mkuu mdogo zaidi duniani

SANNA Marin, ni Waziri Mkuu mpya nchini Finland, anayetarajiwa kuapishwa wiki hii.

Waziri huyu atakuwa ndiye waziri mkuu mwenye umri mdogo zaidi akiwa na umri wa miaka 34.

Waziri huyo wa Uchukuzi alichaguliwa na chama chake cha Social Democratic baada ya kiongozi wake, Antti Rinne, kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.

Ataongoza muungano wa mrengo wa kati-kushoto na vyama vingine vinne, vyote vikiongozwa na wanawake, watatu kati yao wakiwa na umri chini ya umri wa miaka 35.

Rinne alijiuzulu baada ya kupoteza uaminifu miongoni mwa wajumbe wa muungano kwa jinsi alivyoushughulikia mzozo wa maandamano ya wahudumu wa posta.

Atakapochukua mamlaka, Marin atakuwa ndiye Waziri Mkuu mwenye umri mdogo zaidi duniani aliyekuwapo madarakani kwa sasa.

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern ana umri wa miaka 39, huku Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksiy Honcharuk, akiwa na umri wa miaka 35.

Atakuwa ni Waziri Mkuu wa tatu wa kike kuhudumu katika taifa hilo lililoko Kaskazini mwa dunia.

Maisha ya awali ya Marin

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa Sanna Marin alikulia katika familia iliyoishi katika nyumba ya kupanga akiwa na mama yake pamoja na mpenzi wake wa kike.

Aliuambia wavuti wa Menaiset (nchini Finland) mwaka 2015 kwamba kama mtoto alihisi kama ”asiyeonekana” kwa sababu hakuweza kuzungumzia wazi juu ya familia yake.

Lakini anasema mama yake amekuwa akimsaidia na kumfanya aamini kuwa anaweza kufanya chochote alichokitaka.

Alikuwa ni mtu wa kwanza katika familia yake kusoma Chuo Kikuu.

Marin Rose alipanda vyeo haraka katika chama cha Social Democrats na kuongoza utawala wa Jiji la Tampere, akiwa na umri wa miaka 27 na kuwa mbunge mwaka 2015.

Amekuwa waziri wa uchukuzi na mawasiliano tangu mwezi Juni mwaka huu na sasa ana mtoto msichana wa miezi 22.

Wachambuzi wanasema huenda likawa ni jambo ambalo halikutarajiwa kwa Finland ambayo sasa ina Waziri Mkuu mwanamke na viongozi wanne wa chama katika muungano tawala ambao ni wanawake, lakini usawa wa jinsia bado ni tatizo na wanawake katika siasa za Finland wamekuwa nyuma.

Miongo kadhaa iliyopita, watafiti walibaini kuwa vyama vingi vilikuwa na wanawake wenye umri mdogo katika nyadhifa muhimu, nafasi ya pili au ya tatu katika ngazi zinazochukua uamuzi, hii ni kwa mujibu wa Reetta Siukola, Meneja wa Maendeleo wa Kituo cha Habari cha Usawa wa Jinsia.

Kumekuwapo mawaziri wakuu wawili wanawake katika karne hii, ingawa wote walihudumu kwa kipindi kifupi.

Ni dhahiri kwamba wanawake, hususan vijana, wamekuwa wakakamavu katika siasa za Finland na katika miaka ya hivi karibuni umma umekuwa ukitegemea asilimia 40 au zaidi ya wanawake mawaziri katika serikali ya nchi zao.

Hilo lilibadilika mwaka 2015, wakati serikali iliyokuwa na wanaume wengi ya mrengo wa kati – kushoto ya Juha Sipila, ilipochukua madaraka- ni asilimia 36 ya mawaziri wake walikuwa ni wanawake.

Pamoja na kuongezeka kwa kampeni ya Vuguvugu la MimiPia la Dunia, yaani ‘MeToo movement worldwide.’ “Huu ulikuwa ni mwamko mkubwa wa utetezi wa usawa wa jinsia uliochochea mjadala mkubwa wa kijamii juu ya usawa wa jinsia,” anasema Siukola.

Anaweza kuchukua mwelekeo upi?

Kuna uwezekano wa kuwapo kwa mabadiliko makubwa ya sera, kwa sababu muungano ulikubaliana juu ya mpango ulipochukua madaraka.

Hata hivyo, Marin aliyeshinda uchaguzi wa Waziri Mkuu kwa kura chache, aliweka wazi kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyo sasa.

“Tuna kazi nyingi za kufanya ili kujenga upya uaminifu,” anasema wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alipuuzilia mbali maswali juu ya umri wake, akisema: “Sijawahi kufikiria juu ya umri au jinsia. Ninafikiria sababu iliyonifanya niingie katika siasa na mambo yake ambayo tumeaminiwa kufanya na wapigakura.

Social Democrats kilionekana kuwa ni chama kikubwa katika uchaguzi uliofanyika Aprili na kwa hivyo kinaweza kumteaua Waziri Mkuu ambaye ataongoza serikali ya muungano.

Rinne alijiuzulu baada ya mpango wa kukata malipo kwa ajili ya mamia ya wafanyakazi wa posta kusababisha maandamamo makubwa na chama cha mrengo wa kati kikasema kimekosa imani naye.

Hata hivyo, bado ni kiongozi wa Social Democrats.

Wakati huo huo, chama cha mrengo wa kati kilisema kuwa Katri Kulmuni, atatajwa kuwa waziri wa fedha. Kulmuni mwenye umri wa miaka 32, alichukua mamlaka kama kiongozi wake Septemba.

Viongozi wengine watatu walikuwa ni mawaziri katika serikali ya Rinne na wanatarajiwa kuendelea katika nyadhfa zao, kiongozi wa muungano wa mrengo wa kushoto, Li Andersson akiwa Waziri wa Elimu; Kiongozi wa chama cha kijani Maria Ohisalo, kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani; na Anna-Maja Henriksson wa Chama cha Swedish People’s Party akiwa Waziri wa Sheria.

Finland kwa sasa inashikilia urais wa Muungano wa Ulaya na wabunge huenda wakaidhinisha mkuu mpya wa serikali katika mkutano wa EU mjini Brussels.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles