Imechapishwa: Sun, Aug 13th, 2017

FIFA YAWAPA SOMO WAJUMBE TFF

Na ASHA MUHAJI, DODOMA

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limewaonya wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF, wakiwamo viongozi wapya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupiga vita rushwa kwa vitendo.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kufanyika kwa zoezi la uchaguzi mkuu wa viongozi uliofanyika jana mjini hapa, Mkuu wa kitengo kinachosimamia vyama vya soka vya nchi wanachama wa Fifa, Veron Masengo-Omba, aliwataka viongozi hao  kuiangalia rushwa kwa jicho la tatu.

Veron alisema Fifa inapinga vitendo hivyo kwa nguvu zote na kuonya yeyote atakayebainika, shirikisho lake halitamvumilia kuwamo katika familia ya soka.

“Anayekumbatia vitendo hivyo afahamu wazi soka si sehemu yake,” alionya bosi huyo wa Fifa.

Veron aliwataka wagombea wote kuwa kitu kimoja baada ya uchaguzi, kwa imani kuwa kutofautiana katika uchaguzi ni kitu cha kawaida.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho, Suleiman Waberi, pia alisisitiza suala la kupiga vita vitendo vya rushwa.

Suleiman, ambaye pia ni Rais wa Soka Djibout, alisema taasisi yake haiko tayari kufanya kazi na viongozi wanaokumbatia suala hilo.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

FIFA YAWAPA SOMO WAJUMBE TFF