27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

FIFA YAIPIGA PANGA TFF

NA ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limepitisha panga kwa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kulitaka kupunguza idadi ya wajumbe wake kutoka 23 hadi 13.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, alisema wamepokea mapendekezo kutoka FIFA yanayowataka kufanya mabadiliko  ya katiba ya shirikisho hilo.

“Kulingana na mapendekezo hayo, mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ni idadi ya watu katika Kamati ya Utendaji  na kipindi cha kufanya mikutanao..

“Kwa mujibu wa Fifa,  Kamati ya Utendaji inatakiwa kuwa na watu 13 kutoka 23, lakini pia kuwa na vikao  kila baada ya miezi miwili na si miezi mitatu. 

“TFF imeangalia mapendekezo hayo pamoja na uhitaji wa watu katika Kamati ya Utendaji na kupeleka mapendekezo mengine ambayo tunaona yatatusaidia katika utendaji kazi wetu, kwani idadi iliyotakiwa kupungua ni asilimia 45.

“Wajumbe wa mkutano mkuu wanatakiwa kupungua kutoka 129 hadi 87, ikimaanisha katika mikoa  26 kila mmoja utatoa wajumbe wawili, wakati 20 watatoka kwenye klabu na vyama vitatoa wajumbe 15 tu,” alisema Kidau.

Februali mwaka jana, Rais wa Fifa, Gianni Infantino alishiriki mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika hapa nchini. 

Ni wazi agizo hilo la Fifa linalengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hiyo inayosimamia mchezo wa soka hapa nchini.

Katika  hatua nyingine, Kidau alisema mabadiliko ya Katiba ya TFF yaliyofanyika katika mkutano mkuu jijini Arusha, yaligusa moja kwa moja mfumo wa uongozi kuelekea uchaguzi ujao.

“Moja ya sehemu iliyoguswa katika marekebisho ya katiba ni nafasi ya makamu wa rais, ambayo itakuwa ni ya kuteuliwa na rais atakayechaguliwa badala ya kuchaguliwa kama ilivyo sasa,”alisema

Kidau alisema mkutano mkuu wa kawaida wa shirikisho hilo umepangwa kufanyika  Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam, hivyo upo uwezekano wa kujadili mapendekezo yaliyotolewa na FIFA.

Wakati huo huo, Kidau alisema aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania(TPLB), Boniface Wambura ameteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Masoko ya TFF.

Alisema  amepewa kitengo hicho, baada ya kumaliza mkataba wake TPLB mwanzoni mwa mwezi huu.  

“Wambura ni mzoefu katika masuala ya habari kitaaluma na kwa kuwa TFF ina mpango wa kutanua idara ya habari na masoko kwa kuanzisha online radio, magazine na kuboresha ‘newsletter’  Kamati ya Utendaji imeona ni mtu sahihi kukaa hapo.

“Kwa maana hiyo,  siku  si nyingi tutatoa tangazo la ajira katika nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi| na tunatarajia kumpata mtu bora,” alisema Kidau.

Kidau pia alisema  Kamati ya Utendaji ya TFF, imemteua Oscar Milambo kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Mirambo anachukua nafasi ya Ammy Minje, aliyemaliza muda wake, huku akitarajiwa kushiriki mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Fifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles