27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

FETAL ECHOCARDIOGRAPHY: KIPIMO KINACHOPIMA MOYO KWA MTOTO ALIYE TUMBONI

Dk. Naiz akionesha jinsi kipimo hicho kinavyofanya kazi

 

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

GETRUDE Mwita (si jina lake halisi), Mkazi wa Masaki ni mama wa watoto wawili ambaye sasa ni mjamzito, anatarajia kupata mtoto wake wa tatu.

Ni miongoni mwa wajawazito waliofika katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya kipimo maalumu cha uchunguzi wa moyo.

Kipimo hicho kiitwacho kitaalamu Fetal Echocardiography, ni cha kipekee na cha tofauti kidogo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa Taasisi hiyo, Naiz Majani anasema kipimo hicho ni ultrasound ya kuchunguza moyo wa mtoto aliyepo tumboni.

“Hatutumii mionzi ya aina yoyote kufanya kipimo hiki, kinatuwezesha kumuona vema mtoto aliyepo tumboni na kuuchunguza moyo wake kama una tatizo lolote au la,” anasema.

Anasema kupitia kipimo hicho daktari huweza pia kuchunguza mapigo ya moyo wa mtoto kama yanadunda namna inavyopaswa au la.

“Tunaangalia kama mishipa yake ya moyo imetengenezwa vizuri au mapigo yake ya moyo yapo sawa sawa, kwa kawaida mapigo huwa mengi akiwa tumboni, yakipungua tunajua tatizo,” anasema.

 Kwanini Getrude anapima

Anasema alihamasika kufanya kipimo hicho baada ya kusikia kwamba huduma hiyo inatolewa hospitalini hapo.

“Ni mara yangu ya kwanza kufanya kipimo hiki, sina wasiwasi wowote, nipo tayari kwa majibu nitakayopewa na daktari, naona ni vizuri kumpima mwanangu kwani ikigundulika ana tatizo atapata matibabu ya haraka na kupona kabisa,” anasema.

 Takwimu za dunia

Dk. Naiz anasema inakadiriwa kwamba kati ya watoto 100 wanaozaliwa kila siku duniani, mtoto mmoja huzaliwa akiwa na magonjwa ya moyo.

Anasema tatizo kubwa ambalo watoto wengi hukutwa nalo baada ya kufanyiwa vipimo vya uchunguzi ni tundu kwenye moyo.

Daktari huyo anasema hata hivyo hali hiyo inaweza kuepukwa hasa mwanamke akizingatia kuuandaa mwili wake kubeba ujauzito miezi sita kabla.

“Huwa tunashauri mwanamke auandae mwili wake kubeba ujauzito miezi sita kabla, katika kipindi hicho anapaswa kula vyakula bora na kujiepusha kabisa na ulaji usiofaa,” anasema.

Anasema pamoja na hilo ni muhimu pia mwanamke kuwa makini katika kipindi cha wiki 12 ya kwanza ya ujauzito wake.

“Kipindi cha wiki 12 ya kwanza ya ujauzito ni muhimu mno, ni wakati ambapo viungo vya mwili wa mtoto huanza kuumbwa tumboni mwa mama, mara nyingi huenda hata mwanamke husika akawa bado hajajigundua kwamba ni mjamzito.

“Hivyo, anapokuwa amejiandaa kubeba ujauzito miezi sita kabla, kwa kula vyakula bora, kuacha ulaji usiofaa, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na mambo mengine kama hayo, moja kwa moja anakuwa amesaidia kumuepusha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo,” anafafanua.

 Hali ilivyo nchini

Dk. Naiz anasema mwaka jana inakadiriwa kuwa walizaliwa jumla ya watoto milioni moja nchini.

“Sasa kulingana na uwiano huo (mtoto mmoja kati ya 100 kuzaliwa na magonjwa ya moyo), inakadiriwa kwamba walizaliwa watoto 12,000 wenye matatizo hayo mwaka jana,” anasema.

Anasema watoto ambao walifikishwa katika taasisi hiyo na kutibiwa ni 750 tu kati ya 12,000 waliokuwa wamezaliwa.

“Ni idadi ndogo mno waliletwa hospitalini kupata matibabu,” anasema.

 Changamoto

Dk. Naiz anasema ingawa waliwapokea watoto hao, si wote ambao waliweza kuwatibu kwani wengine walifikishwa wakiwa tayari wapo katika hatua mbaya za ugonjwa.

“Magonjwa yote ya moyo yanatibika, tiba kubwa kwa watoto ni kuwafanyia upasuaji mapema, asilimia 20 ya watoto wanaoletwa hapa huwa wanafikishwa umri ukiwa umeenda, wengi wanaletwa wakiwa kwenye umri wa miezi sita na kuendelea.

“Katika hali ya namna hiyo wapo ambao huwa tunashindwa kuwasaidia na hata tukiwafanyia upasuaji tatizo linaweza kuendelea au wanaanza kupata matatizo  mengine ambayo huambatana na upasuaji huo,” anasema.

 Matatizo yenyewe

“Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo husababisha kuchanganyika damu safi na chafu, haya yanaweza kusababisha matatizo ya ubongo iwapo mtoto atakaa nayo muda mrefu.

 “Hivyo, watoto wenye matatizo ya moyo ya namna hiyo ni vizuri wafanyiwe upasuaji katika muda mwafaka, ukichelewa akakaa muda mrefu ubongo unaweza kupata madhara na usirudi katika hali yake ya kawaida.

 Je, hilo linajulikana?

Happy Godfrey, Mkazi wa Sinza ambaye ni mjamzito anashtushwa na suala hilo huku akibainisha kwamba hajawahi kuelezwa kabla.

“Huu ni ujauzito wangu wa pili, sikuwa najua awali kama mtoto akizaliwa na tatizo la moyo na asipopata matibabu inaweza kumsababishia matatizo ya ubongo,” anasema.

Happy anasema amekuwa akihudhuria kliniki na kufanyiwa vipimo mbalimbali lakini si hicho cha kuchunguza afya ya moyo wa mtoto wake.

“Nadhani labda hawana kipimo hicho, kwa kuwa umenijulisha nitakwenda huko na mimi nikapime ili nijue hali ya mtoto wangu,” anasema.

 Faida za kipimo hicho

Dk. Naiz anasema kwa kutumia kipimo hicho wana uwezo wa kuona asilimia 90 ya magonjwa ya moyo kwa mtoto.

“Kwa asilimia 10 tu huwa hatuwezi kuona, awali nimeeleza kwamba tatizo kubwa ni matundu kwenye moyo, kawaida inaweza kutokea mtoto akiwa tumboni moyo ukawa na matundu, hata hivyo yanapasa kufunga pindi anapozaliwa,” anafafanua.

Anasema lakini ikiwa watampima tena baada ya kuzaliwa na kuona matundu bado yapo, moja kwa moja wanajua kwamba hilo ni tatizo linalotakiwa kutibiwa haraka kwa upasuaji.

“Tulianza kufanya kipimo hiki rasmi mwishoni mwa mwaka jana, tuliwapima wajawazito 25, watano kati yao tuligundua mioyo ya watoto ilikuwa na tatizo, hawa wanatarajiwa kujifunga mapema mwaka huu,” anasema.

Anasema wajawazito hao waliwashauri kufika kujifungua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili iwe rahisi kuwatibu mara baada ya kuzaliwa.

Anasema; “Kwa kuwa hawa tutawatibu katika muda unaotakiwa tutakuwa tumewaondoa katika matatizo mengine yanayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa matibabu.

“Nchi za wenzetu wamepiga hatua zaidi na sasa wapo katika majaribio, wakigundua tatizo wanamtibu mtoto akiwa bado yupo tumboni mwa mama yake, na sisi tunatamani kufikia viwango hivyo,” anasema.

Anasema wanatarajia kipimo hicho kitasaidia pia kupunguza idadi ya vifo vya watoto vinavyotokana na magonjwa ya moyo.

 Gharama

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema zimegawanyika katika makundi manne.

“Kuna wagonjwa ambao wapo kwenye kundi la msamaha, kuna wanaochangia kiasi kidogo, kuna wanaotumia bima mbalimbali hasa NHIF, kuna wanaolipa ‘cash’ ambayo huwa ni Sh 50,000,” anasema.

Anatoa wito kwa wajawazito kufika kufanyiwa uchunguzi huo huku akisisitiza wasiogope kwani kipimo hicho hakina madhara yoyote.

“Tanzania imepiga hatua sasa, tumetoka kwenye kusubiri watoto wazaliwe ndipo tuwatibu, tunataka tuwagundue kabla hawajazaliwa.

“Hii itasaidia hata kutoa ushauri kwa wenzetu iwapo mtoto azaliwe kwa njia ya kawaida au kwa upasuaji kuokoa maisha yake kulingana na jinsi tutakavyoona tatizo,” anasema.

Anasema wameona vema kuanzisha huduma hiyo ili kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na magonjwa hayo.

Anaongeza; “Watoto ni Taifa la kesho, ni lazima tufanye kitu cha ziada kuwatambua mapema, ikiwa sisi hatujachukua hatua za awali kuwatambua na kuwatibu watakuwa mzigo kwa Taifa hapo baadae.

Profesa Janabi anasema si kweli kwamba miaka ya nyuma watoto walikuwa hawaugui magonjwa hayo kama wengi wanavyodhani bali hayakugundulika mapema.

“Ni kwa sababu tulikuwa hatuna wataalamu na vifaa vya kisasa, wengi walifariki kwa kile kilichoelezwa ama ni kuugua Nimonia, Typhoid, surua na magonjwa mengineyo.

“Leo hii wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu na tumerudi kusaidia nchi yetu na vifaa tunavyo, tunashukuru sasa jamii imeanza kupata uelewa, watu wanajitokeza na kupima afya zao,” anasema.

JKCI ni tegemeo EAC

Mkurugenzi huyo anasema taasisi hiyo inategemewa hivi sasa na nchi zote zilizopo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki katika kufanya upasuaji kwa watoto wanaougua magonjwa ya moyo.

 “Tupo juu mno, tunaongoza katika kufanya upasuaji huo, tumeshapokea na kutibu watoto kutoka nchini Komoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya wakati  madaktari wao walipokuwa kwenye mgomo,” anasema.

Anasema changamoto wanayokabiliana hivi sasa ni ufinyu wa nafasi, lakini Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kulifanyia kazi suala hilo.

“Tunatamani kuwa na jengo maalumu kwa ajili ya kufanya upasuaji kwa watoto peke yao, tukipata jengo lao tutafanya vitu vingi zaidi kuliko ilivyo sasa,” anasema.

Anasema taasisi hiyo ina jumla ya madaktari wa moyo 15, watatu kati yao wakiwa ni wa watoto na wengine wapo masomoni nchini Israel na Afrika Kusini.

“Mahitaji ni makubwa, inakadiriwa kuwa Watanzania tupo milioni 50, hivyo daktari mmoja anahudumia wagonjwa kati ya 25,000 hadi 30,000, bado kuna uhitaji,” anabainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles