23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Fatma: Sigombei urais TLS

Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

RAIS wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) anayemaliza muda wake, Fatma Karume, amesema hatawania tena nafasi hiyo kwa sasa  kutokana na majukumu yanayomkabili.

Fatma ambaye alichukua nafasi hiyo Aprili mwaka jana akipokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa mtangulizi wake, Mbunge wa Singida Mashariki,  Tundu Lissu (Chadema),  amevunja ukimya baada ya taarifa za awali kuonyesha si miongoni mwa waiojitokeza kuchukua fomu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Fatma alisema amechukua uamuzi huo kwa kuwa anahitaji kuelekeza nguvu kusimamia biashara zao.

“Sitagombea mwaka huu. Washirika wangu wanapendelea nitumie muda wangu mwingi kwa sasa katika biashara zetu na kutokana na ushirikiano walionipa kwa mwaka mzima uliopita, sitawaangusha,” alisema.

Kauli hiyo inamaliza utata uliokuwa umejitokeza awali kuhusu kama  atagombea nafasi hiyo kwa mara nyingine au la.

Ukimya mkubwa ulikuwa umetanda katika kipindi  cha kuomba nafasi ya uongozi wa chama hicho ambacho kinafikia tamati Jumatano   wiki ijayo.

Ukimya wa Fatma pia ulitajwa kuwaweka  njia panda zaidi  baadhi ya wanachama wa TLS hasa wale waliokuwa na matumaini ya kuona kiongozi huyo anatetea kiti chake.

Licha ya kamati ya uchaguzi ya chama hicho Februari 13 mwaka huu kutangaza imesogeza mbele hatua ya kupokea maombi ya wagombea hadi  Jumatano wiki ijayo,  Fatma alikuwa  hajajitokeza kuonyesha nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo katika akaunti yake ya Twitter yenye utambulisho wa jina la Fatma Karume a.k.a Shangazi, juzi aliandika ujumbe uliosomeka, “Good morning everyone . Najua nilikuwa kimya kwa muda. Don’t worry hawajaniteka ili nikae kimya, niko busy kidogo.” 

Katika uchaguzi wa mwaka jana, Fatma alijitokeza katika dakika za mwisho mwisho kuwania urais wa TLS  na kufanikiwa kiti hicho kwa kuonekana na ni mtu sahihi wa kumrithi Tundu Lissu ambaye alikuwa anamaliza muda wake.

Fatma alichuana na kufanikiwa kuwabwaga  Godwin Mwapongo, Godfrey Wasonga na Godwin Ngwilimi ambao tayari walikuwa wameonyesha kuwa na ushawishi mkubwa wa kuchaguliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles