25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Fatma Karume awafunda vijana ACT Wazalendo

ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM

MWANAHARAKATI wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Fatma Karume amewataka vijana kuwa jasiri katika kudai haki zao, kwa kuwa ndio wanaotakiwa kuamua hatma ya taifa la kesho.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana wa ACT Wazalendo jana Dar es Salaam, ambapo Fatma alisema kuwa vijana wanatakiwa watambue kuwa hakuna kitu cha kukiogopa isipokuwa woga wenyewe kwa sababu woga ni kama jela uliyoitengeneza mwenyewe na kujiweka mwenyewe.

“Woga humfanya mtu ajisitishe na kujikwamisha mwenyewe, hivyo vijana wasikubali kutiwa woga ili washindwe kutimiza malengo yao,” alisema Fatma.

Alisema katika hilo, vijana wanatakiwa kutokuwa waoga katika kudai na kutetea demokrasia kwa kuwa haijawahi kuombwa kwa mtu, bali ni haki ya msingi inayohitaji kupiganiwa.

“Na niwaambie, kama mnangoja kugawiwa demokrasia mtanyang’anywa kila siku. Msifikiri kwamba kwenye nchi yetu ambayo kuna chama kimeamua kuhodhi dola, mambo haya yatakuwa mepesi mepesi,” alisema Fatma ambaye pia ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea.

Alisema mapambano ya kisiasa katika mazingira kama yaliyopo nchini huwa yanaonyesha matokeo baada ya muda, hivyo wanasiasa lazima wawe na pumzi.

“Ninaposema muwe na pumzi, mfano mmoja ni kwa Nelson Mandela ambaye ilimchukua miaka 27 jela hadi walipoamua kuvunja mfumo wa ubaguzi wa rangi na kutengeneza katiba mpya.

“Katika mapambano haya msitegemee kirahisi kuona matokeo ya moja kwa moja leo wala kesho, maana CCM imeshasema imeshahodhi dola, hivyo si jambo la lelemama.

“Aliyekuwa na pumzi ndiye atakayeshinda katika mapambano haya. Kazi hii ni muhimu kwa ngome ya vijana kwa sababu vijana ndio waishio leo na tumaini letu kwa siku zijazo,” alisema Fatma.

Alisisitiza kuwa vijana ndiyo leo ya taifa kwa sababu ni muhimu kwa walioko kwenye madaraka waambiwe kuwa vijana ndio mtakaoongoza nchi kwa siku zijazo.

Fatma alisema ni vyema vijana watambue kuwa maisha yao bado yapo kwa hiyo wanatakiwa kujitambua na kujenga taifa la leo na kuamua wanataka kukumbukwa kama mambo waliyoyafanya kwenye maisha yao kwa siku zijazo.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu aliwataka washiriki wote kupokea matokeo na kuunga mkono kwa kutoa ushirikiano kwa atakayekuwa ameshinda kwenye uchaguzi wa ngome ya vijana.

Alisema kwa watakaopata fursa waambiwe jukumu wanalokwenda kulibeba siyo lele mama hasa wakati huu aliodai kuwa demokrasia ya nchi hii imedorora, na vijana wengi wamekuwa waoga.

“Demokrasia tunayoihubiri kwingine, ambayo tumekuwa tukipiga kelele pale Serikali ya Magufuli inapoivunja, leo kifanyike humu ndani,” alisema Dorothy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles