27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Familia ya Balali yamlilia Rais Magufuli

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

FAMILIA ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Daudi Balali imemuomba Rais Dk.John Magufuli, kuingilia kati ili jarada la uchunguzi wa mali za marehemu mama yao, Rahel Vasolela Balali lifanyiwe kazi.

Jalada hilo linadaiwa kuwa kwa sasa lipo kwa Mkurugenzi wa Mashataka nchini (DPP), hivyo kuliibua kutasaidia kumaliza mgogoro wa mali uliopo baina yao na watu wanaodai kuwa ni wamiliki wa mali zao.

Familia hiyo imedai kuwa kwa sasa wamekuwa wakiishi maisha magumu licha ya mama na kaka yao marehemu Balali, kuacha mali nyingi ambazo zimevamiwa na watu waliodai ni matapeli wenye lengo la kutafuta fedha kwa nguvu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mpwa wa marehemu Balali, Yassin Mgunda, alisema kwa miaka kadhaa wamekuwa wakiishi maisha magumu huku mama yao Elizabeth ambaye ndiyo alipewa nguvu ya kusimamia mali hizo kwa mujibu wa sheria, akijikuta akiwekwa ndani kwa kesi za kusingiziwa ikiwamo utakatishaji fedha hali ya kuwa hana hata uwezo wa kupata Sh 10, 000 kwa sasa.

Kutokana na hali hiyo, alisema marehemu bibi yao, Rahel Vasolela Balali, alikuwa akimiliki kiwanja namba 83 kilichopo Msasani Beach ambapo kilinunuliwa mwaka 2002 kutoka kwa Kampuni ya raia wa Italia aliyoitaja kwa jina la Beach Properties.

“Hata hivyo baada ya bibi kununua kiwanja hiki na baadae baada ya kifo cha mjomba Daudi alijitokeza mtu ambaye alidai kuwa kuwa ni mke wake na kudai ni mali yake. Hata hivyo Polisi walianza uchunguzi wa kina na ilipofika mwaka jana walibaini nyaraka zote za mauziano ikiwamo aliyeuza kiwanja hicho kwa bibi.

“Baada ya kifo cha bibi mwaka 2010, familia ilitulazimu kutafuta msimamizi wa mirathi yetu ambaye pia alikuwa na jukumu la kusimamia mali, lakini cha kushangaza amegeuziwa kibao kutokana na yeye kuonekana ana herehere. Kwa hali hiyo tunamuomba Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa Watanzania wanyonge atusaidie ili jarada la uchunguzi ambalo lipo kwa DPP wamalize kazi ili tuweze kupata haki zetu,” alisema Yassin

Naye Magreth Balali, alisema kuwa wamenashangazwa na yanayoendelea hasa kwa watu wanaodai kuwa wanahusika na mali huku akiwaomba kama kweli wao ni wanafamilia wa Balali wajitokeze ili wakae nao ili kupata amani ya kudumu katika familia yao.

“Leo sisi kaka yetu alikuwa Gavana wa BoT lakini haya ndiyo maisha yetu, dada yangu Elizabeth amewekwa ndani kwa utakatishaji fedha, licha ya kuomba kwamba aachiwe na tuko tayari kulipa hawataki, kwa hali hiyo wale wanaocheza kwenye mtandao wa kudhulumu mali wanaona akiwa ndani ndio nafuu yao jambo ambalo si haki.

“Tumevumilia vya kutosha na sasa tunajitokeza kwa umma kuomba msaada kwa Rais Magufuli walau aweze kuliingilia kati suala hili, ili amani ya kudumu ipatikane kwetu,” alisema Magreth.

Alipotafutwa, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Bizwalo Mganga, ili kupata ufafanuzi wa jalada la uchunguzi ambalo limekwama kwake kwa zaidi ya mwaka sasa, alisema kuwa ofisi yake iachwe kwani inafanya kazi kwa utaratibu na si kwa kushinikizwa.

“Ninaomba tuachwe sisi tunafanyakazi kwa utaratibu na si kwa kushinikizwa,” alisema DPP Mganga

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles