26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Facebook inavyotumika kufanya biashara ya wanyamapori

Bakari Kimwanga – Aliyekuwa Thailand

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizobarikiwa kuwa na wanyama wa aina mbalimbali, ambapo katika kuhakikisha utulivu unapatikana kwenye hifadhi, Serikali imekuwa ikitunga sheria mbalimbali kwa lengo la kulinda rasilimali hiyo muhimu.

Katika uso wa dunia, Tanzania inatajwa kuwa nchi iliyofanikiwa kudhibiti biashara ya wanyama kwa kuwa na sheria kadhaa zinazozilinda hifadhi.

Wizara ya Maliasili na Utalii, imepewa jukumu la kutayarisha sera ya wanyamapori, kusimamia utekelezaji wake  na kuratibu maendeleo ya sekta ya   wanyamapori nchini.

Sera ya wanyamapori inaeleza kwamba matarajio ya sekta hiyo miaka 20 ijayo ni kwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Kwa hapa nchini, historia ya uhifadhi wa wanyamapori inarudi nyuma hadi mwaka 1891 wakati sheria ya kudhibiti uwindaji ilipoanzishwa na utawala wa Wajerumani.

Sheria hizi zilidhibiti uvunaji wa wanyama;  mbinu za uwindaji na biashara ya wanyamapori, ambapo baadhi ya aina ya wanyama waliokuwa hatarini kutoweka walilindwa ipasavyo. Hifadhi za kwanza za wanyamapori, zilianzishwa na Wajerumani mnamo mwaka1905 katika eneo ambalo sasa linaitwa Pori la Akiba la Selous.

Maeneo ya kuhifadhi wanyamapori   yalichaguliwa kutokana na kuwapo kwa wanyama wakubwa, na wala si kwa sababu za makundi anuwai ya kibaiolojia.

Wanyamapori wa Tanzania ni urithi wa asili wa pekee na rasilimali yenye umuhimu mkubwa kitaifa na kimataifa. Umuhimu wake umejikita katika thamani ya kibaiolojia ya spishi zenyewe na mazingira ya asili yaliyopo nchini, thamani  yake ya kiuchumi na uwezo wake katika   kuchangia maendeleo endelevu nchini.

Kupitia sheria zilizopo za uhifadhi wa wanyamapori kama vile Sheria ya Uhifadhi wa Wanayamapori Na12 ya mwaka 1974,   Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro Kifungu cha 413 ya mwaka 1959, Sheria ya TANAPA kifungu cha 412 ya mwaka 1959 na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Serengeti ya mwaka 1980 zinaweka mkazo katika kulinda rasilimali za wanyamapori.

Kutokana na muhimu huo, hivi majuzi Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la RTI ambao wanatekeleza mradi wa usafirishaji haramu wanyamapori chini ya USAID Protect, iliwakutanisha waandishi wa habari wa Tanzania na Thailand, ambayo ni moja ya nchi za Kusini mwa Asia inayotajwa kuwa na kiwango kikubwa cha wanyama wanaopita nchini humo kutoka nchi za Afrika kwenda mataifa mengine.

Wanahabari hao kutoka nchi hizo kila upande waliweza kubadilishana uzoefu na taarifa za kina kuhusu usafirishaji haramu wa wanyamapori ambapo kila upande waliweza kwenda kwa nchi husika na kujifunza na hata kuona hali halisi ya ulinzi wa hifadhi za taifa.

Ripoti ya Traffic ya mwaka 2018 iliangazia tathmini ya haraka kuhusu utumiaji wa mtandao wa kijamii wa Facebook kama kiunganishi cha biashara ya wanyamapori nchini Thailand.

Ripoti hiyo pia ilichapishwa katika mtandao wa Thailand 24 Traffic kwa ajili ya ufuatiliaji biashara ya wanyamapori.

Ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ulimwenguni kote katika biashara ya wanyama wa porini na mimea kwa muktadha wa uhifadhi wa biolojia wa aina zote na maendeleo endelevu.

Katika ripiti hiyo mpya ya Traffic, inaelezwa kuwa mamia ya wanyama hai wa porini wanauzwa kupitia mtandao wa  Facebook nchini Thailand, bila usajili kwa sababu wao sio wa asili ya nchi hiyo.

Wanyama wengi wanaouzwa walikuwa watoto wachanga, waliopewa dhamana ya biashara ya wanyama. Karibu nusu ya aina ya wanyama wanaopatikana  katika biashara hiyo, asilimia 47 bado hawajapewa ulinzi chini ya sheria ya msingi ya wanyamapori ya Thailand, Sheria ya Hifadhi ya Wanyama wa Porini na Sheria B. 2535 (WARPA) nyingi kwa sababu sio wa asili ya nchi hiyo.

Wanyama hao, Black Pond Turtle Geoclemys hamiltonii, ambao si wa asili, wameorodheshwa katika taarifa ya CITES na ni marufuku kufanyika kwa biashara hiyo, lakini mara kwa mara hubebwa nchini humo.

Hivi sasa, ni aina 12 tu ndio sio wa asili wakiwamo mamalia saba, ndege moja, reptilia watatu na kipepeo mmoja, wanaolindwa chini ya Sheria ya WARPA. Aina 200 zilizorekodiwa na utafiti wa Traffic zilikuwa na mamalia, ndege na wanyama watambaao.

Kukua kwa biashara ya wanyamapori mtandaoni kumeongoza zaidi kwa aina zisizo za asili ambazo kwa sasa hazina kinga ya kisheria au kanuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Mkoa wa Traffic Asia ya Kusini, Kanitha Krishnasamy, anasema ipo haja ya kuwapo kwa sheria ili kulinda haki za wanyama na kukomesha bishara hiyo.

“Kupeana aina za ulinzi chini ya sheria za Thailand na kuwezesha watekelezaji kuchukua hatua, ndiyo njia nzuri zaidi ya kushughulikia tatizo hili katika sekta ya hifadhi,” anasema Krishnasamy.

BIASHARA INAVYOFANYIKA

Tathmini ya haraka juu ya utumiaji wa Facebook kufanya biashara ya wanyama wa porini nchini Thailand, inaonesha kuwa nchi hiyo inajitolea kwa hali na mali kukabiliana na ujangili wa wanyamapori kupitia Kitengo cha Hawk cha Pori chini ya Idara ya Hifadhi za Taifa, Wanyamapori na Uhifadhi wa Mimea (DNP).

Hata hivyo, bado inaonyesha kuna mianya ya kisheria inayodhoofisha juhudi hizi na kuweka spishi zisizo za asili hatarini.

Aidha, ripoti hiyo inaeleza namna ambavyo waandishi wanavyotaka marekebisho ya sheria na kuwasihi viongozi kuongeza juhudi zao katika utekelezaji kwa kufanyakazi karibu na Facebook kama njia ya kukuza mikakati ya pamoja ya kushughulikia biashara haramu ya wanyamapori mitandaoni.

Biashara haramu ya wanyamapori nchini Thailand, inayojumuisha aina za asili na zisizo za asili, inajumuisha ununuzi na uuzaji wa wanyama hai katika masoko maarufu ya wikendi na Chatuchak.

Njia hii ya kufanya biashara mtandaoni inazidi kushamiri ulimwenguni na wakati mwingine ni matokeo ya kuhamishwa kutoka masoko ya asili kwenda mtandaoni.

Utafiti uliofanywa nchini Malaysia juu ya biashara ya torto na turtle za maji safi ulipata mabadiliko makubwa katika mifumo ya biashara, mfano kuhama kutoka kwa mtandao wa kijamii (Bouhuys na van Scherpenzel).

Mfano, nchini Thailand Facebook ni maarufu na mtandao wa Thais. Mitandao ya kijamii umeona ukuaji mkubwa wa watumiaji nchini Thailand baada ya 2010 na sasa inafanya kazi kama mtandao mkubwa zaidi wa kijamii na jukwaa la biashara nchini humo.

Biashara haramu ya wanyama pori pia hufanyika, ambapo inaripotiwa  kuwa wafanyabiashara kadhaa wamekamatwa na vyombo vya kutekeleza sheria.

Desemba 2015, viongozi wa Thailand waliripoti kwamba watuhumiwa wawili ambao walikuwa wakitangaza Burmese Star Tortoises Geochelone platynota ya kuuza kupitia Facebook walikamatwa. Turmese Star Burmese ambao sio asili ya Thailand na ni aina ya sambayo, hupimwa ulimwenguni kote kama ilivyowekwa hatarini na IUCN1.

KAULI YA KIKOSI KAZI

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi Kazi cha Ulinzi wa Wanyamapori Ofisi ya Hifadhi ya Wanyamapori, Thiradej Palasuwan, anasema wamekuwa wakipambana kupitia kikosi kazi na watu wanaofanyabishara hiyo haramu ya wanyamapori.

“Kwa mfano hapa kuna mtu alijitambulisha anaitwa kina kwenye Facebook akiwa anauza wanyama, lakini tulipofanya uchunguzi tuliweza kubaini ni mtu mzima, na tulifanikiwa kumtia mbaroni kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Haya ni mapambano ambayo hatuchoki na kubwa tunawataka wanahabari muendelee kuwafichua watu hao ambao wamekuwa wakifanya hii biashara,” anasema Palasuwan.

RIPOTI YA INTERPOL

Katika kukuza na kuunga mkono utekelezaji wa mapambano hayo, Interpol nchini Thailand imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali katika uhalifu wa wanyamapori na hatari ya baonuai.

Kikosi hicho kimekuwa kikibadilishana taarifa mbalimbali na nchi wanachama kuhusu mtandao wa biashara hiyo, malengo na kuchunguza kwa kina na hatimaye kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles