31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Escrow yazamisha watatu urais 2015

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)

Na Mwandisi Wetu

KASHFA ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, imewachafua viongozi watatu ambao walishaanza harakati za kuusaka urais kwa mwaka 2015.

Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Kwa upande wa Pinda, ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa bungeni, ilionyesha kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni alilidanganya Bunge kwa matamshi yake.

Mara kadhaa Pinda alisikika akiueleza umma kuwa fedha hizo hazikuwa za umma bali mali ya Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya IPTL.

Katika maazimio ya PAC, Pinda alitakiwa pia kuwajibika kutokana na kushindwa kusimamia Serikali kwani katika hatua zote za kutolewa kwa fedha hizo, alikuwa akijulishwa.

Pinda ambaye alitangaza kuanza harakati za urais kimya kimya, akiwa jijini London, Uingereza alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha BBC, alijikuta kwenye wakati mgumu pale Bunge lilipopitisha azimio la kumpeleka kwa mamlaka ya uteuzi kabla baadae jina lake kuondolewa.

Hali hiyo ilijitokeza pale Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alipolishauri Bunge kupeleka majina ya watu wote waliotakiwa kuchukuliwa hatua kwa mamlaka zao za uteuzi ili hatua zaidi zichukuliwe.

Baada ya kauli hiyo ya Zitto, Spika wa Bunge Anne Makinda alilihoji Bunge na kwa sauti moja likakubali kabla ya Mbunge wa Simanjiro, Ole Sendeka kusimama na kuomba mwongozo wa Spika ambaye baadaye alitengua uamuzi wake.

Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema jina la Pinda kupelekwa kwa rais ingetosha kuonyesha Bunge halina imani naye, hivyo mamlaka yake hiyo ya uteuzi ingebidi itengue nafasi ya kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni.

Alisema pia kamati yake ilikubali kuondoa jina la Pinda kwenye orodha ya vigogo waliopaswa kushughulikiwa baada ya mazungumzo kati ya wabunge wa upinzani na wale wa CCM.

Kutokana na hali hiyo, Pinda ambaye anajulikana zaidi kama ‘mtoto wa mkulima’, harakati zake za kwenda Ikulu zimetiwa doa kwani mwanzo alihesabika kuwa ni kati ya wagombea wasio na kashfa.

Kwa upande wake, Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, anadaiwa kupewa Sh milioni 40.4 kutoka kwenye akaunti ya Escrow huku Profesa Tibaijuka ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akidaiwa kupewa Sh bilioni 1.6.

Viongozi wote hao wawili ambao hawajawahi kutangaza rasmi kuwania urais mbali na majina yao kutajwa kwenye orodha hiyo, Bunge limeazimia wachukuliwe hatua.

Kwa upande wa Profesa Tibaijuka, rais ametakiwa kumvua wadhifa wa uwaziri huku Ngeleja ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, spika akishauriwa kumchukulia hatua ya kumvua wadhifa huo.

Akichangia bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven Wasira, aliwataka wote wanaotumia suala la ripoti ya PAC kwa vigezo vya kuwaondoa wenzao katika mbio za urais hawastahili kupewa nafasi hiyo.

“Wanaotaka urais kama wapo ni pamoja na mimi, ambao wanaona mbinu ni kuwaondoa wengine kwa nguvu, hao hawafai kupewa urais wa nchi hii. Urais ni lazima ushindaniwe kwa haki na vyama vyote vipewe nafasi ya kushiriki. Kama unataka urais ushindani uwe kwa njia sahihi,” alisema.

Alisema ni bora kuwa maskini anayeheshimika kuliko kukubali kuwa tajiri anayedharauliwa na kutukanwa kutokana na mapato yasiyokuwa halali.

Wasira alieleza kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema baadhi ya watu walikwenda kuchukua fedha wakiwa na magunia, mifuko ya sandarusi, rumbesa na maboksi katika moja ya benki, ni vyema uchunguzi ukifanyika ili kuwatambua watu hao na hatua zaidi zichukuliwe.

“Ni lazima tufuatilie na vyombo vyetu vya sheria vituambie ni kina nani hao, vinginevyo hatuna nchi. Tukubali hawa watu wabebe mizigo yao, hakuna CCM ya wezi, ila kuna wezi ndani ya CCM, hivyo wezi ni lazima wabebe mizigo yao,” alisema.

Alisisitiza kwamba ripoti hiyo ya PAC inatakiwa kuheshimiwa na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuihoji uhalali wake kwa kuwa inatokana na kamati maalumu inayotambuliwa na Bunge iliyokusanya taarifa kutoka kwa vyombo vinavyoaminika vya Serikali, ambavyo ni Takukuru na CAG.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles