27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU YASAIDIA KUPUNGUZA MASAHIBU YA USAFIRI KWA WANAFUNZI

Na CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

KERO ya usafiri kwa wanafunzi  na wananchi wa kawaida hasa waliopo mjini, kwa kiasi fulani imechangia kudidimiza uchumi na elimu.

Hii ni kwa sababu ya watu kukosa usafiri wa uhakika wa kwenda kwenye shughuli za kimaendeleo na wanafunzi kukosa baadhi ya vipindi vya asubuhi darasani.

Hali hiyo imechangia baadhi ya watu kuamka alfajiri ili kuwahi usafiri, lakini kwa upande wa wanafunzi huendelea kuteseka kila kukicha.

Unyanyasaji wa wanafunzi unaofanywa na makondakta na madereva wa daladala unasababishwa na kiasi kidogo cha nauli wanazochangia pindi wanapotumia usafiri huo.

Changamoto wanayoipata wanafunzi ilisababisha Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Baraza la Ushauri watumiaji Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC), watoa huduma za usafiri na wadau wengine kukaa meza moja kuzungumzia suala hilo.

Majadiliano hayo yalizaa matunda kwa kupitisha maazimio ya kumjali mwanafunzi na kuacha kunyanyasika ndani ya usafiri wa umma pindi anapokwenda shule au kwenye shughuli nyingine.

Moja ya maazimio ya mjadala huo ilikuwa ni SUMATRA kutunga kanuni zinazomtaka mwanafunzi kulipa nauli nusu kwa usafiri wa katikati ya mji na kutoa onyo kwa watoa huduma kuacha kuwanyanyasa pindi wanapotumia usafiri huo.

Hata hivyo, licha ya kupitishwa kwa kanuni hiyo, baadhi ya makondakta na madereva wameendelea kuwanyanyasa na hivyo kusababisha wengi wao kuchelewa masomo wakati wa kwenda shule na kuchelewa  kurudi nyumbani nyakati za jioni.

SUMATRA CCC kwa kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kwa pamoja waliona haja ya kutoa elimu ya usalama barabarani na haki za abiria kwa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.

Elimu hiyo ilitolewa ili wanafunzi wafahamu haki zao pindi wanapokuwa safarini tangu wakiwa na umri mdogo.

Katibu Mtendaji  wa SUMATRA CCC, Oscar Kikoyo anasema mafunzo hayo yamesaidia kujenga uelewa kwa wanafunzi kuhusu masuala ya usalama wa barabarani pamoja na haki zao pindi wanapokuwa safarini.

Anasema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa wa kujikinga na ajali kwa sababu ya kuanzishwa kwa vilabu  vya SUMATRA CCC katika shule za msingi na sekondari.

Kikoyo anasema hadi sasa wanafunzi 2,500 nchini wamepatiwa mafunzo hayo kupitia klabu hizo shuleni.

Anasema wanafunzi hao wanatoka katika shule za msingi 20 na shule 26 za sekondari katika mikoa wa Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kigoma, Mbeya, Arusha, Tabora, Mwanza na Kagera.

Anasema tangu kutolewa kwa elimu hiyo shuleni, manyanyaso kwa wanafunzi yamepungua.

“Tunashukuru tangu tufungue vilabu shuleni na kutoa elimu ya usalama barabarani pamoja na haki na wajibu wao wawapo safarini, imesaidia kujenga uelewa na kupunguza manyanyaso katika daladala,” anasema Kikoyo.

Anasema tatizo  lililokuwa likichangia awali wanafunzi na baadhi ya abiria kunyanyasika katika vyombo vya usafiri ni uelewa mdogo wa elimu ya usalama barabarani na haki zao kama abiria.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Elimu kwa Umma wa baraza hilo, Nicholous Kinyariri anasema wameamua kuwajengea uwezo wanafunzi kwa sababu watasaidia kusambaza elimu hiyo kwa watu wengi zaidi.

Anasema SUMATRA CCC ina amini kwamba abiria akifahamu wajibu wake na kuutimiza haki yao hatapotei.

Kikoyo anasema huwa wanashuhudia wanafunzi wakigombana na makondakta pindi wanaponyanyasika wawapo safarini, jambo ambalo linaonesha kuwa jamii imeanza kutambua haki zao.

Anasema kila abiria anapaswa kufahamu kuwa ana haki ya kupewa tiketi yake pindi anapolipa nauli, haki ya kurejeshewa nauli kama usafiri utachelewa kwa muda mrefu, kufikishwa mwisho wa kituo na nyinginezo.

Anasema abiria wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kwa sababu ya kupenda maisha nafuu ikiwamo kukata tiketi kwa wapiga debe ambao huwasababishia matatizo kwa kuwapa tiketi za kughushi au kuwaelekeza kwenye mabasi yasiyo na uhakika wa safari.

Aanasema ni vema abiria wakajenga mazoea ya kufuata taratibu na sheria zilizopo ambazo zitamlinda mtumiaji na mlaji wa huduma za usafiri.

“Ifike wakati abiria wajenge mazoea ya kukata tiketi kwenye ofisi za mabasi na kuachana na wapiga debe,” anasema Kinyariri.

Anasema abiria anaposafiri na kukata tiketi anaingia mkataba na mmiliki wa basi husika hivyo ni muhimu kuzingatia sheria ili kujilinda endapo kutatokea dharura yoyote.

“Zipo kesi nyingi za wadau tumeshindwa kufika nazo mbali kwa sababu ya kukosekana ushahidi wa tiketi,” anasema Kinyariri.

Anasema msafiri anapaswa kukumbuka kuwa pindi ajali inapotokea anatakiwa kulipwa fidia na mwenye basi husika lakini cha muhimu awe na vielelezo kamili vitakavyoweza kuthibitisha kwamba kweli alikuwa ni msafiri ndani ya basi husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles