25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu kwa njia mbadala inawatenga waliopo vijijini

Faraja Masinde

MWEZI huu tumeshuhudia jitihada kadha wakadha zinazoendelea kuchukuliwa kwa lengo la kunusuru elimu nchini, iliyoathiriwa na janga hatari la virusi vya corona lililosababisha kufungwa kwa shule na vyuo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Katika hilo tumeshuhudia Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) kwa kushirikiana na wadau wa elimu ambao ni vyombo vya habari husususan radio na televisheni vikiweka mipango kabambe kuhakikisha kuwa watoto wanapata muda wa kuendelea kujifunza wakiwa nyumbani.

Wapo waliokwenda mbali zaidi kwa kuanzisha majukwaa ya kufundisha kwa njia ya mtandao (Online Education) ambapo wazazi ndiyo wamekuwa waratibu wakubwa kwa watoto wao, lengo likiwa ni lile lile moja na jema la kuhakikisha wanafunzi walioko shule ya msingi na sekondari wanendelea kujifunza, utaratibu ambao unatumiwa zaidi na shule binafsi.

Binafsi naunga mkono uamuzi huu wala sipingani nao hata kidogo, kwa sababu unawasaidia wanafunzi hawa waliolazimika kukatisha masomo bila ridhaa yao kuendelea kuchota maarifa kulingana na madarasa waliyopo.

Hata hivyo, jambo linaloleta ukakasi kwenye uamuzi huu ni namna ambavyo kundi jingine la watoto linavyokosa fursa hii muhimu ya kupata elimu kwa njia ya mtandao au radio na televisheni.

Ni vigumu kwa watoto wa kijijini ambao mbali na kufikiwa na nishati ya umeme wa REA lakini hata mzazi kumiliki radio au televisheni imekuwa ni changamoto, ikizingatiwa maeneo mengi ya vijijini ndiko kuliko na wanafunzi wengi zaidi.

Hivyo, nadhani kuna haja ya wadau hawa wenye nia njema na elimu kwa wanafunzi wetu hawa wakaangalia namna nyingine nzuri ya kuhakikisha kuwa kundi hili ambalo linaishi huko ambako bado teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) iko chini nalo likapewa kipaumbele kwa serikali au taasisi zake kuja na mwarobaini wa kuwanufaisha wote.

Kwani iwapo hali hii itabaki hivi basi kutakuja kuwapo na pengo kubwa kwenye mitihani ya mwisho kati ya wanafunzi wa mjini na vijijini kwa sababu waliopo mjini watakuwa na maarifa ya ziada ikilinganishwa na wa kijijini.

Hivyo basi, naamini hili litafikiriwa tena vizuri na wadau husika kuona ni kwa namna gani watoto hawa nao wanaweza kunufaika na hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles