25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

El Chapo ahamishiwa gereza lenye ulinzi mkali

COLORADO, Marekani

BAADA ya mapema wiki hii mlanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya,  Joaquin maarufu kama “El Chapo” Guzman kuhukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha genge la mauaji ya kihalifu, sasa amehamishiwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali zaidi.

Guzman  amehamishiwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali lililopo Colorado ambako hakuna mfungwa aliyewahi kutoroka.

Taasisi inayosimamia magereza nchini Marekani imethibitisha taarifa hiyo.

Guzman alihukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja na miaka mingine 30 siku ya Jumatano baada ya kukutwa na makosa ya biashara ya dawa za kulevya na kushiriki njama za mauaji wakati akiwa kiongozi wa genge kubwa zaidi la biashara hiyo la Sinaloa.

Guzman aliwahi kutoroka mara mbili kwenye magereza yenye ulinzi wa hali ya juu, kabla ya kukamatwa tena mwaka 2016.

Hata hivyo taasisi hiyo haikueleza zaidi kuhusu gereza hilo alikohamishiwa Guzman lililoko kilomita 185 kusini mwa Denver.

Gereza hilo lina wafungwa 375 na lilifunguliwa mwaka 1994.

Hukumu dhidi ya Guzman iliyotolewa Jumatano  inachukuliwa kama hitimisho la hujuma hiyo ya muda mrefu iliyofanywa na genge lak hilo.

Hukumu ya kesi hiyo iliyosikilizwa na mahakama ya serikali kuu ya Brooklyn iliangazia kisa cha mtu mmoja aliyearifu kwamba alinusurika kuuawa katika shambulizi lililopangwa na Guzman.

Mnamo mwezi Februari, Guzman, 62 alikutwa na hatia ya kufanya biashara haramu ya maelfu ya tani ya dawa za kulevya aina ya cocaine, heroin na bangi, pamoja na kujihusisha na kupanga matukio kadhaa ya mauaji, wakati akiwa kama kiongozi wa genge la Sinaloa.

Genge hilo  kwa muda mrefu lilitambulika kuwa genge kubwa zaidi miongoni mwa mengine, lenye ubabe na linalouza madawa kwa wingi zaidi.

Kabla ya hukumu hiyo waendesha mashitaka walimwomba jaji wa mahakama ya wilaya, Brian Cogan kumuhukumu kifungo cha maisha gerezani, pamoja na miaka 30 ya kutumia silaha za moto.

Guzman ambaye jina lake linamaanisha “Mfupi” aliwahi kujizolea umaarufu mkubwa kwenye eneo la jimbo lake la Sinaloa, alikozaliwa.

Alizaliwa kwenye makazi masikini yaliyoko katika kijiji kilichoko milimani.

Awali kabla ya hukumu alikuwa kizuizini, katika chumba alichofungiwa peke yake kwenye gereza la Metropolitan, lenye muundo wa ngome huko Manhattan.

Mwezi uliopita, jaji Cogan alitupilia mbali ombi la Guzman la kufanya mazoezi kwenye dari ya gereza hilo, baada ya waendesha mashitaka kusema anaweza kutumia upenyo huo kutoroka.

Kabla ya kukamatwa mwaka 2016, Guzman alifanikiwa kutoroka mara mbili kwenye magereza yenye ulinzi mkali nchini Mexico. Alirejeshwa Marekani kukabiliana na mashitaka dhidi yake mwezi Januari, 2017.

Guzman, alijitangazia umaarufu wa jina lake kama mfanyabiashara wa dawa hizo za kulevya miaka ya 1980, wakati alipochimba mahandaki katika mpaka wa Mexico, ya kupitisha na kufanya biashara hiyo kwa haraka zaidi kuliko wapinzani wake wa kibiashara.

Alijiimarisha zaidi kibiashara katika miaka ya 1990 hadi 2000, kupitia vita vya mara kwa mara na wapinzani wake, na hatimaye kuja kujulikana zaidi kama kiongozi wa genge hilo la Sinaola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles