24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DUNIA YA AJABU NA KISHETANI YA GUINEA YA IKWETA TANGU UHURU

JOSEPH HIZA NA MTANDAO             |           


GUINEA ya Ikweta si Taifa linalofahamika sana duniani pengine kutokana na udogo wa eneo lake sambamba na idadi yake ndogo ya watu, isiyozidi milioni 1.5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015.

Hata hivyo, ilikuja angaziwa na dunia wakati ilipoangukiwa na moja ya majanga makubwa katika karne ya 20, karibu sawa na kilichoitokea Cambodia, likisababishwa na Rais wake wa kwanza baada ya Uhuru, Francisco Macias Nguema.

Rais huyo mlozi aliyedai kuwa na nguvu zisizoshinda uchawi aliacha makovu, ambayo bado yangalipo baada ya kutesa, kuua na kulazimika theluthi moja ya watu wa Taifa hilo kuikimbia nchi wakati wa utawala wake.

Mrithi wake, mpwa wake, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo (76), ambaye bado ni Rais miaka 39 sasa baada ya kumpindua mwaka 1979, hamfikii  mjomba wake huyo kwa ukatili na viroja lakini naye ni wale wale na si mtu wa watu!.

Teodoro huyu anamwandaa mwanae kipenzi sharobaro mpenda matanuzi, Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue (49), maarufu kama Teo Nguema kumrithi.

Wakati wa utawala wa awamu ya kwanza, umeme ulikuwa ukizimwa kila Rais alipoondoka kutoka Mji Mkuu wa Malabo.

Kwamba hakukuwa na ulazima wa kuuwasha kisa rais (mungu) hayupo mjini na hivyo uzimwe ili kutoharibu fedha na kwamba waliobakia mjini humo hawakuwa na hadhi ya kustahili nishati hiyo.

Hakuwa rafiki wa uhuru wa kutoa maoni na hivyo wanahabari hawakuthubutu kutamka fani yao, vinginevyo hugeuzwa bucha na kutupwa baharini.

Watu walitoweka katika Guinea ya Ikweta na hakukuwa na mtu aliyethubutu kuinua mdomo kuhoji utata  wa mtoweko huo.

Bidhaa pekee kutoka nje zilizokuwa sokoni kipindi hicho zikitokea nje zilikuwa samaki wa makopo na shampeni rangi ya pinki, ambazo zilikuwa sehemu ya mabaki yaliyoingizwa maalumu kwa mkutano wa kilele wa marais wa Afrika Magharibi uliokuwa umefanyika hapo Malabo.

Msaada wa kigeni wakati huo ulifikia asilimia 90 ya Pato la Ndani la Taifa (GDP), ambapo sehemu kubwa liliishia kwa vitu visivyo na umuhimu kama vile shampeni pinki.

Awali taifa hili lilipokuwa chini ya utawala wa Kikoloni wa Hispania, huduma za afya zilikuwa bora na kiwango cha vifo kilikuwa chini na pato kubwa kwa upili Kusini mwa Sahara Afrika.

Macias Nguema, ambaye mwaka 1968 alichaguliwa kidemokrasia, hakuchukua muda akabadili yote hayo, akageuka kuwa dubwana hatari lenye kiu ya damu.

Serikali na uchumi ukawa suala la kifamilia, huku mawaziri karibu wote wakitokea kijiji kimoja akiwamo kijana Teodoro.

Kijana huyo akachaguliwa na mjombake huyo kuwa mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Taifa, akiwa mmoja wa jamaa wengi wa Macias walipewa madaraka ya juu.

Macias, ambaye alikuwa mtupu kichwani akiwa amefeli mara tatu mitihani ambayo ingemwezesha kuingia katika utumishi wa umma wakati wa ukoloni, daima alikosa utulivu na raha kila alipowaona wasomi.

Haikuchukua muda, akawa akiua kila mtu aliyevaa miwani, ambao kwa mtazamo wake walikuwa wasomi na ilikuwa hatari kwa yeyote nchini humo kumiliki ukurasa wowote mkubwa wa karatasi za kuchapishwa.

Chini ya Macias, kazi za lazima sawa na utumwa zilirudishwa, ijapokuwa hiyo haikuzuia uzalishaji wa cacao, zao kuu la biashara kipindi hicho kushuka kwa asilimia 56.

Akijitangaza mwenyewe kuwa rais wa maisha, mlozi na mtenda miujiza asiye na mfano, alijipachika pia ujaji mkuu akihukumu mwenyewe maelfu ya watu kwenda kaburini.

Akiwa haamini mtu, alitumia muda mwingi katika kijiji alikozaliwa cha Mongomo, ambako aliweka hazina ya taifa chini ya kitanda chake au makasha ya fedha kibandani mwake.

Wakati ukafika kumwondoa Macias. Ilianza hivi, mwaka 1979, walinzi wa Kikosi cha Taifa alichokiongoza mpwa wake chenye wanafamilia wakiwamo kaka zake Teodoro walimwendea Macias huko Mongomo.

Walimtaka aachie sehemu ya fedha alizohifadhi kwenye makasha ili kulipia maofisa wa Kikosi cha Ulinzi, ambao walikaa bila mishahara kwa miezi kadhaa.

Akiwa amekasirishwa na kile alichokiona kukosa kwao uvumilivu, Macias aliwapiga risasi na kuwaua wote hao.

Obiang na wengine waliomzunguka Macías’ walikuwa na hofu kuwa Rais ameingiwa na wazimu na hivyo kuna haja ya kumuwahi kwa njia ya Mapinduzi, ambayo wataitumia kuanika madhambi yake na hivyo kujihalalisha uamuzi wao. ,

Ikiwa na maana mpango huo haukumaanisha kusikitishwa na madhambi yake, maana Teodoro mwenyewe tayari alifahamika kuwa mtesaji hatari hasa wakati akiwa mkuu wa gereza la Black Beach lililojulikana kwa mateso ya kutisha. Bali alifahamu fika siku inakuja janga litamwangukia, hivyo ilibidi amuwahi mjomba wake na kumuua.

Hivyo akampindua Agosti 3, 1979 katika Mapinduzi ya umwagaji damu na kumhukumu kwa matendo yake ikiwamo mauaji ya kimbari ya watu wa Bubi, mwongo mmoja kabla.

Macías alihukumiwa kifo na kuuawa na kikosi cha mauaji Septemba 29, 1979.

Hata hivyo, kutokana na sifa zilizoenezwa kuhusu nguvu zake za kichawi, askari wa Guinea waliogopa kumpiga risasi ikabidi kiundwe kikosi kipya kwa msaada wa Kikosi cha Rais cha Morocco.

Obiang akatangaza Serikali mpya na mwanzo mpya wa kudai kuachana na ukatili na ukandamizaji wa Macías.

Alitoa misamaha ya kisiasa kwa wafungwa na kusitisha utumwa.

Hata hivyo hakueleza chochote juu ya ushiriki wake katika unyama ulioendeshwa na utawala wa mjombake.

Mwaka 1992, ikiwa ni miaka 13 baada ya Mapinduzi, mafuta yakagundulika katika pwani ya nchi hiyo na mara paap!, Guinea  ya Ikweta na hasa Familia ya Teodoro Obiang Nguema Mbasogo – ikawa tajiri.

Pamoja na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, katika uchaguzi wa 1996 na 2002 alichaguliwa kwa kishindo akipata asilimia 98 ya kura. Mwaka 2009, alishuhudia umaarufu wake ukianguka, lakini bado akipata asilimia 97 ya kura.

Pengine kitendo cha mmoja wa viongozi wa upinzani Severo Moto Nsa, kufungwa jela miaka 101 kilisaidia wapiga kura kuamua nani wa kumpigia kura hasa kwa vile kura hazikuwa za siri.

Na kama Mpwa wa Macias maarufu kama ‘Miijuza Halisi’ alivyosema kwa kujitapa, “yeyote asiyenipigia kura ni wa daraja la chini’ ndivyo alivyosema Teodoro.

Tangu hapo Obiang akaunda utawala katili wa chama kimoja unaohusisha familia yake na kupenda kusifiwa redioni kama Mungu.

 

Julai 2003, redio inayoendeshwa na Serikali ilimtangaza kuwa Mungu, ambaye “ana mawasiliano ya kudumu na Muumba” na “ana uamuzi wa kuua bila mtu yeyote kumzuia na bila kwenda kuzimu.”

Yeye binafsi aliwahi kutoa ufafanuzi unaolingana na huo mwaka 1993.

 

Nguema pia amedaiwa ingawa hakuna ushahidi kuwa kama mjomba wake amekuwa akila nyama za wapinzani wake hasa bongo zao.

Mmoja wa washauri wake wa zamani alimzungumzia Nguema: “Anaweza kuamua kuua bila kufanywa chochote na hudai haendi jehanamu kwa vile yu Mungu mwenyewe, ambaye huwa karibu naye daima na amempa nguvu zake.”

Msaidizi huyo aliyeko mafichoni nje ya nchi anasema Nguema alimtaka arudi, lakini anahofia maisha yake akisema; ‘siwezi rudi, kwani atanikamata na kunikata kende zangu na kuzila nikishuhudia,:

Kuna minon’gono kwamba anaugua saratani ya tezi dume lakini hakuna uthibitisho wa hilo.

Awali ni watu wachache wa nje waliokuwa wakilijali taifa hilo hadi ulipogundulika utajiri wa mafuta.

Kisha kampuni kubwa za nishati za Kimagharibi zikahamia hapo na familia ya kwanza ikajiunga katika orodha ya mabilionea wa dunia.

Kuhusu ufisadi uliopo, Obiang, huwatupia lawama wageni kuwa ndio waliouleta na huwaambia watu kwamba anahitaji kusimamia hazina ya taifa ili kuzuia wengine isiangukie katika mikono mibaya.

Kwa mujibu ya wapelelezi wa Marekani Obiang anadhibiti akiba ya dola milioni 700 pekee huku asilimia 80 ya wananchi wake wakiwa maskini wa kutupwa.

Ajabu Waziri wa Kazi na Usalama wa Jamii, Estanislao Don Malavo, aliwahi kukaririwa akisema: “Tulikuwa maskini sana. Kisha Mungu akajibu maombi yetu, tuligundua mafuta,”

Lakini wakati Waziri wake wa Mambo ya Nje Agapito Mba Mokuy alipojaribu bahati yake kuwania uenyekiti wa Tume ya Afrika hivi karibuni, alibanwa kwanini taifa hilo linafanya vibaya katika maendeleo ya jamii pamoja na utajiri wake huo mkubwa.

Mwaka 2015, zikiwa takwimu za karibuni zaidi zilionesha mtoto mchanga mmoja kati ya wanne wanaozaliwa nchini humo hupewa chanjo ya polio na surua.

Aidha mmoja kati ya watatu chanjo ya kifua kikuu, viwango ambavyo ni moja ya vile vya chini kabisa duniani.

Wastani wa umri wa kuishi na kiwango cha vifo vya watoto wachanga pia viko chini ya wastani uliopo kwa mataifa ya Kusini mwa Sahara Afrika.

Karibu nusu ya wakazi wake hukosa maji safi ya kunywa.

Mwaka 2012, watoto wanne kwa kila watoto 10 wenye umri wa miaka sita hadi 12 nchini humo hawakuwa shuleni, idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na mataifa yenye pato dogo.

Nusu ya watoto wanaoanza shule kamwe huwa hawakamilishi elimu yao na wachache wasiozidi robo moja ya wanaoikamilisha ndio pekee huendelea na shule ya kati.

Katika viashiria vya elimu na afya mara nyingi taifa hilo huburuza nyuma ya majirani zake maskini lakini kukiwa na utajiri binafsi waliojilimbikizia maofisa waandamizi wa Serikali.

Maofisa hawa hutumia utajiri wa akiba ya mafuta kujinufaisha wao, marafiki na jamaa zao.

Sababu nyingine ni namna taifa hilo linavyowekeza utajiri huo, au kwa maneno mengine kutojiwekezea kwa manufaa ya wakazi wake na vizazi vijavyo.

Matumizi makubwa ya kiholela ng’ambo yanayofanywa na mtoto wa Rais Teodoro Obiang Nguema yamesababisha chunguzi za utakasishaji wa fedha, ambazo zimefichua lundo la ushahidi unaoonesha uwapo wa ufisadi wa kiwango cha kutisha serikalini.

Moja ya majaribio ya awali ya Obiang kusafisha taswira yake ni miongo miwili iliyopita alipotoa ufadhili wa pauni milioni mbili kwa Shirika la Sayansi na Elimu la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Fedha hizo zililenga tuzo ya sayansi kitu kilichosababisha kelele duniani kutoka makundi ya haki za binadamu.

Na hivyo basi tuzo hiyo haikutolewa, lakini ameweza kushika urais wa Umoja wa Afrika licha ya pingamizi nyingi.

Wakati kuna njia nyingi, ambazo maofisa wa serikali hufuja utajiri wa umma wa mafuta, miradi ya umma ya miundombinu inaonekana kuwa mahala pazuri zaidi kwao kujichotea mabilioni kwa njia ya rushwa.

Badala ya kuwekeza katika sekta za afya na elimu kwa wananchi wake, serikali humimina karibu mapato yake yote ya mafuta katika miradi ya ujenzi na mara nyingi zabuni huziangukia kampuni, ambazo maofisa waandamizi akiwamo rais wana hisa.

Mtu hatari katika ukoo wa Teodorín, ni mwanae kipenzi na mrithi wake mtarajiwa. Kwa mfano kabla hajawa Makamu wa Rais, mshahara wake kama Waziri wa Kilimo na Misitu mwaka 2001 ulikuwa dola 5,000 kwa mwezi.

Lakini katika miaka mitatu tu ya kwanza alitumia kiasi mara tatu ya Bajeti ya Wizara ya eElimu kufanya manunuzi ya kufa mtu.

Alibambwa akijaribu kununua boti ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 234 mapema mwaka huo na baadaye akaripotiwa kupoteza begi lenye dola 250,000 ndani yake. “Ni mpuuzi na mjinga fulani,” aliwahi kusema ofisa mmoja wa mashirika ya kijasusi Marekani.

Nchini humo jina lake lilianza kuvuma katika kitongoji cha matajiri cha Malibu, Jimbo la California nchini Marekani katika miaka ya 1990, wakati akisoma katika Chuo cha Pepperdine nchini humo.

 

Umaarufu wa haraka akiwa katika kitongoji hicho, ulitokana na staili yake ya kupenda starehe; matanuzi au makamuzi ya kufa mtu kama waitavyo vijana wa mjini.

 

Aliishi katika jumba la kifahari huku masomo yake yakigharimiwa na kampuni moja ya Marekani, ambayo ilikuwa na mkataba wa kuchimba mafuta kwao- Guinea ya Ikweta.

 

Alitumia fedha kujirusha na kunasa warembo wa kila aina huku akiwa hakosekani katika vilabu vya usiku jimboni humo.

 

Na alipoanza kunogewa, akaanza kutumia fedha za umma au zilizopatikana kifisadi kuweka makazi ya kudumu jimboni humo na kwingineko Ulaya.

 

Akanunua mahekalu na magari ya kifahari, ndege ya kifahari na kujiweka karibu na watu maarufu.

 

Aidha kipenzi huyo wa Dikteta Teodoro alivuma zaidi wakati akitoka na rapa na mcheza filamu maarufu wa Marekani, Eve baada ya kumfukuzia kwa muda mrefu ikiwamo kukodi boti kwa dola 700,000 ili kumvuta himayani mwake.

 

Mbali ya Eve, mwingine nchini humo ni nyota wa tamthilia maarufu ya The Real Housewives of Atlanta, Porsha Williams.

 

Mafanikio yake ya kunasa wasichana warembo, yanastahili kuendana na msemo kwamba ‘fedha ni mtawala wa dunia.’

 

Hivyo, wengi wanaona kilichowafanya warembo wengi wakiwamo hao maarufu kumkubali Mangue si kingine zaidi ya fedha bila kujali uhalali wake.

 

Miaka kadhaa iliyopita Idara ya Mahakama nchini Marekani ilimlazimisha Mangue kurudisha mali zenye thamani ya dola milioni 30 kwa watu wa nchi yake.

 

Wakati mahakama ikimtaka auze mali hizo ili fedha zikabidhiwe kwa asasi ya hisani nchini mwake, ilimruhusu abaki na glavu mng’ao aliyoitumia Michael Jackson wakati wa enzi za uhai wake.

 

Mali hizo ni pamoja na hekalu lake la

California, gari lake aina ya Ferrari na sehemu kubwa ya vitu vilivyowahi kutumiwa na Michael Jackson.

 

Mahakama ilisema maliasili za nchi hiyo zinavunwa katika michakato na miradi hewa yenye lengo la kujaza mifuko ya rais, mtoto wake na maswahiba zao wa karibu.

 

Aidha Mahakama hiyo inasema kuwa njia nyingine iliyotumiwa na mtoto huyo kujilimbikiza mali ni ule mradi alioubuni wa kuweka mabati katika nyumba za wananchi maskini, lakini badala yake fedha ziliingia mifukoni mwake.

 

Mahakama pia imemruhusu kubaki na jaketi lililotumiwa na Michael Jackson wakati wa ziara yake ya ‘Thriller’ na ndege ya kifahari aina ya Gulfstream yenye thamani ya dola milioni 38. 5 kwa vile ziko nje ya Marekani.

 

Hata hivyo, mwenyewe alidai mali hizo alizipata kutokana na fedha alizojiwekea kwa mujibu wa sheria ya nchi yake na kupitia mikataba ya kibiashara ndani na nje ya Guinea ya Ikweta.

 

Aliongeza ana matumaini uamuzi wa mahakama na suluhu waliyokubaliana itaimarisha uhusiano baina ya nchi yake na Marekani.

 

Teo pia amekuwa akichunguzwa nchini Hispania na Ufaransa kwa tuhuma kama hizo.

 

Mwaka 2012, Ufaransa ilitoa kibali cha kukamatwa na kushikilia hekalu lake pamoja na baadhi ya magari yake ya kifahari.

 

Hekalu la Teodorin Obiang lililopo katika kitongoji tajiri cha Avenue Foch, katika Mji Mkuu wa Ufaransa, Paris, linakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 100.

 

Tangu anguko la Kanali Muammar Gaddafi Oktoba 2011, baba yake ameondokea kuwa mtawala asiye wa kifalme aliyeongoza kwa muda mrefu kuliko wote duniani.

 

Kama ilivyo kwa madikteta wengine wa Afrika; Idi Amin na Mobutu Sese Seko, Obiang amejipa mwenyewe vyeo kadhaa ikiwamo El Jefe yaani Bwana Mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles