23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DRU PRESA: UFUPI WA KIMO SI KIKWAZO KATIKA ULIMWENGU WA MITINDO

AKIWA amezaliwa na aina ya ufupi uliosababisha awe na urefu wa futi tatu na inchi nne, Dru Presta anafurahi kuionesha dunia kuwa hali hiyo si kikwazo cha kukwamisha ndoto yako.

Kwamba kwa kutumia mfano wake, anataka kuionesha dunia kwamba ufupi si sababu ya kutoweza kujitosa katika fani aipendayo kuliko kitu chochote kile duniani – uanamitindo.

Akiwa amekulia katika mji wa Reno, Nevada, Dru alikuwa mwathirika wa vitendo vya unyanyapaa kwa miaka 15 kwa sababu ya hali yake hiyo inayoitwa kitaalamu achondroplasia.

Lakini kwa sasa; ‘modo’ huyu kijana ni kichocheo kwa wengine waliodhani kwamba wasingeweza kuchomoza katika ulimwengu wa mitindo kutokana na ufupi wa vimo vyao.

Hakuna mtu anayemcheka tena kwani mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 21 amevunja vunja vikwazo katika dunia ya mitindo na kufanikiwa kuliteka jiji liliolojaa kila aina ya ‘mastaa; la Los Angeles.

Dru alihamia katika jiji hilo miaka miwili iliyopita na kuacha nyuma maisha hasi ya mji ule mdogo ili kusaka mafanikio ya ndoto zake kwa kuingia katika tasnia hiyo.

Sasa akisomea shahada ya masoko ya mitindo, modo huyo ameweza kuyabadili maisha yake na tayari amekuwa akifanya vyema katika dunia ya mitindo.

Sassy Dru aliiambia televisheni ya Barcroft TV: “Reno kule Nevada ni mji mdogo. Hivyo ni jamii ndogo mno mtambuka. Hivyo haikuwa rahisi kwangu kukubalika kwa vile ni kitu kigeni kwao. Kitu kisicho cha kawaida kwa jamii ile.

“Walininyanyasa tangu mdogo na shuleni, walinichokoza mno na kunibatiza kila aina ya majina mabaya na yenye kuumiza kwa sababu tu ya hali yangu.

“Wakati nilipokuwa mdogo nilizoea kukabiliana na ukosoaji kwa namna nyingi mbaya. Wakati mwingine nilihamaki na kujibu mapigo.”

Dru ikabidi asaidiwe na familia yake lakini kama mtu wa kwanza kuzaliwa na ufupi huo katika historia ya familia yao, kila mtu alijifunza kuishi na hali hiyo.

Ilikuwa ngumu kwa mwanamitindo Drew kupata nguo za kimitindo katika mji wake huo wa nyumbani lakini sasa mjini Los Angeles anaishi na kufurahia maisha ambayo aliyaota.

Dru anasema: “Niliamua kuingia katika tasnia hii kwa sababu sitaki yeyote ajihisi hawezi kujieleza mwenyewe kama nilivyokuwa huko nyuma.

“Nataka kuionesha dunia kupitia picha zangu za uanamitindo kwamba unaweza kuvutia ukiwa na kimo au ukubwa wowote ule.

“Unaweza kuwa mrefu mno na futi sita na inchi nne na unaweza kuwa futi tatu na inchi nne kama mimi ukawa bado mzuri na mwenye mvuto mkubwa.”

Akaunti yake ya Instagram imejaa picha mbalimbali za mitindo ikiwa na wafuasi 10,000 wanaomsifu.

Anasema: “Uanamitindo umepaisha kujiamini kwangu. Najisikia mzuri na mwenye mvuto mbele ya kamera, ni kama Dru tofauti apendaye kuanikwa. Niseme wazi hakuna maneno mengine, zaidi ya kwamba napenda kuwa mbele ya kamera.

“Ushauri wangu kwa watu wenye ufupi ambao wangependa uanamitindo wajitokeze bila kusita.”

Anaongeza: “Nataka kila mtu katika tasnia ya mitindo duniani akubalike. Nataka kila mtu aweze kutembea jukwaani kama wengine kwa kujiamini– iwe wanatembelea kwa miguu yao, baiskeli za miguu au kwa magongo, yote sawa!.

“Sitaki wajisikie kwamba wanatakiwa kuvaa kama wengine, kwa sababu kila mtu ana saizi yake. Nataka watu wawe huru kufanya kwa namna walivyoumbwa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles