26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa ahojiwa kwa saa sita Polisi

Aziza Masoud na Asifiwe George, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana lilimuhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa, kwa zaidi ya saa sita kuhusiana na tuhuma za mauaji dhidi yake.
Hilo limetokea siku moja baada ya mlinzi binafsi wa Dk. Slaa, Khalid Kagenzi, kueleza jinsi alivyoteswa na walinzi wa Chadema na hata kumuhusisha na tishio la mauaji ya kiongozi huyo.
Dk.Slaa alihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam jana kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni huku akiwa amefuatana na mawakili watatu wa chama hicho wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdalla Safari. Wengine ni Nyaronyo Kicheere na John Mallya.
Alipofika kituoni hapo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema aliingia moja kwa moja katika chumba maalumu na kuhojiwa na askari wa upelelezi ikiwamo kuchukuliwa maelezo ya kina kuhusu jinsi anavyolitambua tukio hilo.
Wakati akihojiwa na polisi, Dk. Slaa alikuwa akiongozwa na wanasheria wa Chadema ambao muda wote walikuwa wakisikiliza mahojiano hayo kati ya polisi na kiongozi huyo.
Mahojiano yalipokuwa yakiendelea ndani, nje ya jengo la polisi walionekana viongozi mbalimbali wa Chadema wakizunguka, huku wengine wakiingia ndani na kutoka.
Kutokana na mahojiano hayo kuwa marefu ilimlazimu mmoja wa mawakili hao wa Chadema, Profesa Safari kutoka ndani na kuondoka ilipofika saa 5.00 asubuhi.
“Ndani kuna mahojiano ya kawaida na anaeleza mazingira ya namna alivyotaka kuuawa… hivyo anaandika maaelezo ya kile anachokijua yeye,” alisema Profesa Safari.
Baada ya mahojiano hayo ilipofika saa 9:40 jioni, Dk. Slaa alitoka ndani kiwa na wanasheria John Malya na Nyaronyo Kicheere na kuzungumza na waandishi wa habari juu ya mahojiano yake na polisi.
Alisema utaratibu wa kuandika malalamiko katika sheria ni kawaida kwa kuwa pande zote zinapaswa kutoa taarifa za nini wanakifahamu kuhusu tukio lolote.
“Maelezo yana hatua mbili; hatua ya kwanza tunaelewana ni nini kimetokea, hatua ya pili ni muhusika kuandika malalamiko ama kuandikiwa kama hawezi, baadaye anayapitia na kuyakubali akiridhika nayo.
“Nimeandika kuhusu nini nakifahamu kuhusu tukio ambalo lipo kwa sasa, nimeandika page(kurasa) tisa na nayakumbuka kwa mtitiriko nimeandika nini masuala ya uchunguzi, polisi wameshapokea maelezo yangu kwa sasa jukumu la kutoa taarifa ni la kwao,”alisema Dk. Slaa.
Alisema kwa sasa anasimama kama shahidi namba mmoja kwa kuwa kesi za jinai ni za Jamhuri ambaye pia ndiye mlalamikaji mkuu.
Katibu huyo wa Chadema alisema mpaka sasa chama chake kama taasisi kimefanya uchunguzi wa kina na kina ushahidi wa kutosha kuhusu tukio hilo yakiwamo mawasiliano baina ya Kagenzi na waliokuwa wanahusika na mkakati huo.
Alisema wakati anaandika maelezo hayo walikuwapo maofisa wawili wa polisi na mmoja alimtaja kwa jina la afande Massawe na mwingine ni mpelelezi.
Akizungumzia kuhusu walinzi waliokamatwa kwa tuhuma za kumjeruhi Kagenzi ambao ni Benson Mramba, Hemed Sabura na Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob, Dk.Slaa alisema vijana hao wanashikiliwa na polisi katika Kituo Kikuu baada ya kutolewa Oysterbay.
“Yeye tumemshitaki lakini ameenda kufungua jalada jingine kuwashitaki wengine ndani ya chama, kuna vijana watatu wapo ndani bado wanahitaji kupata dhamana labda kesho(leo) wanaweza kutoka endapo tutakamilisha taratibu,”alisema Dk.Slaa.
Wakili wa Chadema, John Mallya, alisema Dk.Slaa alitoa maelezo ya tuhuma mbili ambako Kagenzi anadaiwa kupewa fedha na maofisa usalama kwa ajili ya kuwasiliana nao pamoja na kutoa siri za vikao vya ndani vya chama.
“Mlinzi wa Dk. Slaa kupewa fedha na Usalama ni kosa kwa mujibu wa sheria za chama pia kula njama za kutaka kumdhuru kiongozi nalo ni kosa pia; hayo ndiyo mambo ya msingi tunayoyasimamia,” alisema Mallya.
Kauli ya Kova
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliahidi kuzungumzia suala hilo leo.
Viongozi wafika kituoni
Wakati Dk. Slaa akiwa ndani akiendelea na mahojiano viongozi kadhaa wa Chadema walifika kituoni haponm kufuatilia kilichokuwa kinaendelea ndani.
Hao ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho(Bavicha), John Heche.
Juzi, akizungumza jijini Dar es Salaam, Kangenzi alikanusha madai ya kuhusika na mpango huo akisema kuna watu ndani ya Chadema wamekuwa wakimtuhumu bila kutoa uthibitisho wa madai hayo.
Alisema taarifa iliyotolewa Machi 8 mwaka huu kwa waandishi aliiandika yeye kwa kulazimishwa baada ya kupigwa na kuteswa huku akitishiwa kuuawa na walinzi wenzake wa Chadema.
Alisema Machi 7, mwaka huu aliitwa katika ofisi ya Makao Makuu Chadema na kuingizwa katika chumba kilichokuwa na watu watano aliowatambua kwa majina, ambao ni Boniface Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo, Hemedi Sambura, Benson Mramba, na watu wengine wawili aliowataja kwa jina moja moja; Jumanne na Mamba.
Alisema baada ya kuingizwa ndani ya chumba hicho aliona mfuko uliokuwa umehifadhia bisibisi, kisu, bikari na ‘pliers’ ambazo walizitumia kumpiga na kumtesa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles