24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein amtaja Karume mafanikio sekta ya elimu

Mwandishi Wetu- Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu kutokana na misingi bora iliyowekwa na mwasisi wa taifa hilo, marehemu Abeid Amani Karume.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Shule ya Sekondari Mwembeshauri, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema ukombozi uliofanywa na Chama cha ASP chini ya uongozi thabiti wa Karume mwaka 1964, umeweka misingi bora ya upatikanaji wa elimu na kubainisha kuwa itaendelea kutolewa bure katika awamu zijazo.

Dk. Shein alisema kabla ya Mapinduzi hayo, elimu ilitolewa kwa malipo, watoto wa wazalendo wa Zanzibar, hususan wanyonge walishindwa kupata fursa ya kusoma, sambamba na kutolewa kwa misingi ya ubaguzi kutegemea na kabila la mtu alikotoka.

Alisema kupitia ilani ya uchaguzi ya ASP, Karume alitangaza elimu kutolewa bure pale chama hicho kitakaposhinda na kukamata hatamu, jambo ambalo limeendelea kutekelezwa hadi sasa.  

“Katika awamu tofauti za uongozi, Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuendeleza sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa skuli hadi kufikia 381 hivi sasa, kati yake skuli 284 zikiwa za sekondari,” alisema Dk. Shein.

Alisema Zanzibar inasifika kwa kuwa na mfumo bora wa utoaji wa elimu katika ukanda wa Mashariki ya Afrika na bara lote kwa ujumla.

“Ujenzi wa shule tisa mpya utaondoa kabisa tatizo la mlundikano la wanafunzi katika skuli mbalimbali,” alisema Dk. Shein akitoa mfano wa baadhi ya skuli walimu watatu kufundisha darasa moja kwa wakati mmoja, kutokana na wingi wa wanafunzi.

Alisema Serikali inaendelea kufanya juhudi kubwa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya elimu, ikiwamo upatikanaji wa vitabu na madawati, akibainisha awamu ya pili ya uagizaji madawati 42,135 kutoka nchini China kwa skuli za msingi.

Dk. Shein alisema Serikali inaendelea kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) kwa kuongeza vitivo na programu mbalimbali za masomo ili kuhakikisha taifa linapata wataalamu wengi kupitia nyanja tofauti.

Alisema Serikali imelipa kipaumbele suala la elimu na kubainisha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2019/20, imetenga Sh bilioni 178.9 kwa sekta ya elimu.

Dk. Shein alisema changamoto ya upungufu wa walimu wa Sayansi tayari imeanza kupatiwa ufumbuzi kwa msaada wa wahisani mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dk. Shein alipingana na mitazamao ya baadhi ya watu wanaodai elimu imeshuka, akisema haijulikani kipimo gani kilichotumika kuhusisha dhana hiyo, kwa kuzingatia kuwa hivi sasa Zanzibar imekuwa na vyuo vikuu kadhaa, wakati zamani havikuwapo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema ujenzi wa shule hiyo ya ghorofa mbili, una lengo la kuondokana na ufinyu wa nafasi.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idriss Muslih Hijja alisema Shule ya Mwembeshauri ni miongoni mwa shule tisa zilizokamilika ujenzi wake Unguja na Pemba.

Alizitaja shule nyingine zinazohusika na mradi huo kuwa ni pamoja na Kinuni, Chumbuni, Bububu na Fuoni kwa Unguja na Wara, Mwambe, Kizimbani na Micheweni za kisiwani Pemba ambazo nazo zimepewa majina mbalimbali ya viongozi wa kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles