23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN AKEMEA MAKUNDI NDANI YA UVCCM

BAKARI KIMWANGA Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameonya vitendo vya rushwa na makundi ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, amesema kama vitendo vya rushwa vitaendelea ndani ya umoja huo, chama hakitasita kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika.

Dk. Shein aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akifunga mkutano mkuu wa UVCCM, uliofunguliwa juzi na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

“Rushwa na makundi yalikuwa yanaitesa UVCCM na katika hili kama itabainika kati ya waliochaguliwa kuna wanaoendekeza makundi, tutayafyeka mara moja,” alisema Dk. Shein.

Hata hivyo, alisifu uchaguzi huo kufanyika kwa amani na utulivu huku akiwataka viongozi waliochaguliwa wafanye kazi kwa masilahi ya chama badala ya kuendekeza ubosi.

“CCM siyo chama kinachoshabikia mvutano, malumbano na misuguano na kumbukeni kwamba kukubaliana na matokeo ni tabia ya uungwana na ndiyo utamaduni wa CCM.

“Pia, UVCCM tumieni mitandao ya jamii na hata majukwaa ya siasa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika kutekeleza jukumu la kukilinda na kuitetea CCM,” alisema Dk. Shein.

Aliwahimiza kuzitumia mbinu bora zilizotumiwa na UVCCM ya miaka iliyopita ambayo ilijibu hoja kwa wakati na ambayo iliungana kwa mambo makubwa yalioamuriwa na chama wakati wote.

Wakati huo huo, Mwenyekiti mpya wa UVCCM, Kheri James, alisema kitendo cha yeye kuchaguliwa kuiongoza jumuiya hiyo ni kielelezo cha CCM kuwa na akiba ya kutosha ya vijana.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka waliokuwa wagombea wenzake, washirikiane naye   waweze kujenga uwezo wa pamoja kwa ajili ya kusaidia umoja huo.

James alitoa kauli hiyo mjini hapa jana baada ya kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, William Lukuvi, kuwa ndiye mshindi.

Katika uchaguzi huo, James aliwashinda wapinzani wake kwa kupata kura 319 huku mpinzani, Thobias Mwesiga akipata kura 127.

Wagombea wengine walikuwa ni Simon Kipala aliyepata kura 67, Kamana Simba aliyepata kura 27, Juma Mwaipaja aliyepata kura (19), Seif Mtoro aliyepata kura 16 na Mganwa Nzota ambaye alipata kura moja.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo uchaguzi wake ulifanyika mara mbili, Tabia Maulid Mwita, alishinda kwa kupata kura 286 huku mpinzani wake, Rashid Mohamed Rashid, akipata kura 282.

“Jana (juzi), Mwenyekiti   wetu wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, alikemea rushwa wakati akifungua mkutano wetu.

“Kauli zake, zitumike kama mwongozo na makatibu na wenyeviti wa mikoa na wilaya, hakikisheni mnakwenda kujadili hotuba hiyo kwenye vikao vyenu kwa ajili ya utekelezaji.

“Pia, toeni ushirikiano kwa Serikali   iweze kutimiza wajibu wake kwa ngazi zote na isikwamishwe kwa sababu yetu sisi vijana ambao tuna kazi kubwa ya kubeba ajenda za wananchi.

“Najua changamoto zinazowakabili vijana kwa sababu nimekulia katika umoja huu kupitia mwenyekiti wa wilaya nafasi ambayo nimeitumikia kama ngazi ya kuwaunganisha vijana wawe kitu kimoja.

“Kaimu Katibu Mkuu Shaka, ninakuagiza mkachapishe hotuba ya Mwenyekti Rais Dk. John Magufuli neno kwa neno na iende ikajadiliwe katika vikao vya ngazi zote za CCM kama dira na mwongozo kwetu na mimi nitapita kila sehemu kufuatilia utekelezaji wake.

“Pamoja na hayo, ninatambua uzito wa nafasi niliyokabidhiwa na vijana na nitahakikisha ninawaunganisha kwa kuwawakilisha vema kwenye vikao vya chama na kueleza matatizo yao kwa vitendo,” alisema James.

James alitumia mkutano huo kumuomba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, wakubali mapendekezo yake  kuhusu vijana wanaotakiwa kupata nafasi za uteuzi ndani ya chama na Serikali.

Kwa mujibu wa James, ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake  atakwenda kila mkoa na wilaya   kukagua uhai wa jumuiya na kutekeleza ahadi zote alizozitoa wakati anaomba kura.

Katika uchaguzi huo, wajumbe wengine waliochaguliwa kwa uwakilishi wa makundi ni Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), aliyechaguliwa ni Doto Nyirenda kwa kura 306 huku Jumuiya ya Wazazi akichaguliwa Amiri Mkalipa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles