25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DK. NAGU: SIKUKAMATWA, NILIHOJIWA POLISI

Na MWANDISHI WETU


MBUNGE wa Hanan’g, Dk. Mary Nagu (CCM), amesema hajawahi kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Hanan’g, Sarah Msafiri.

Dk. Nagu, ametoa ufafanuzi huo hivi karibuni, baada ya gazeti hili katika toleo lake la Julai 19, mwaka huu, kuandika habari za kukamatwa kwake kwa agizo la DC Msafiri, muda mfupi baada ya kuwapo vurugu katika kikao cha Kamati ya Siasa cha Wilaya ya Hanan’g.

“Nimelazimika kutoa ufafanuzi na kukanusha taarifa kwamba, nilikamatwa kwa agizo la mkuu wa wilaya.

“Nakumbuka siku hiyo, tulikuwa na kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ambapo kulitokea hali ya kutoelewana miongoni mwa wajumbe juu ya kanuni zetu za vikao na kusababisha mkutano uvunjike ambapo baadaye nilikwenda polisi kutoa maelezo ya kile kilichotokea na nakumbuka nilikaa ofisini kwa OCS  kama dakika 20 hivi, kisha nikaondoka,” alisema Dk. Nagu.

Wakati Nagu akitoa ufafanuzi huo, taarifa ambazo gazeti hili lilizipata siku ya tukio hilo zilisema mbunge huyo alikwenda polisi kwa maelekezo yaliyotolewa na mkuu huyo wa wilaya baada ya kuibuka kwa vurugu katika kikao chao.

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alikiri siku ya tukio, kwamba Dk. Nagu na wajumbe wenzake walikwenda kuhojiwa katika kituo cha polisi kwa maelekezo ya mkuu wa wilaya.

Katika maelezo yake, Kamanda Masawe alisema Dk. Nagu na baadhi ya waliokuwa wakishiriki kikao hicho, walishikiliwa katika Kituo cha Polisi Katesh kwa ajili ya kutoa maelezo.

MASHAMBA YA NAFCO

Kuhusu mashamba hayo, Dk. Nagu alisema hawajawahi kushiriki kwa namna yoyote katika suala la kuyagawa kwa wananchi au wafanyabishara wa aina yoyote tofauti na ilivyodaiwa katika habari iliyochapwa katika gazeti hili siku hiyo.

“Mimi sihusiki hata kidogo na suala la mashamba ya NAFCO na katika maisha yangu sijawahi kuhusika katika kugawa mashamba hayo kwa mtu yoyote au mfanyabishara wa nje ya Hanan’g.

“Ninapenda kuueleza umma, kwamba sijui lolote na hata katika kikao cha CCM ambacho mkuu wa wilaya alishiriki, suala la mashamba halikuwa moja ya ajenda,” alisema Dk. Nagu.

Kutokana na maelezo hayo, Gazeti la MTANZANIA, linamwomba radhi Mbunge Nagu kwa makosa ya kiuandishi yaliyotokea katika habari ile na kumsababishia usumbufu.

MHARIRI.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles