26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KIMEI: MIKOPO YA VIWANDA IMEONGEZEKA CRDB

Na ELIYA MBONEA -ARUSHA

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, amesema Serikali inatakiwa kuanza kutengeneza masoko ya kuuza bidhaa za wazalishaji wadogo na wa kati wanaochukua mikopo benki kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kuzalisha na kusindika bidhaa.

Pia alisema tangu Serikali ianze kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda, benki hiyo imeanza kupokea maombi mengi ya mikopo yanayoelekezwa katika viwanda.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, katika mkutano wa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Arusha uliokusudia kusikia maoni yao kuhusu huduma zitolewazo na benki hiyo.

“Wakopaji wengi ambao ni wazalishaji wadogo na wa kati wameanza kuagiza mashine kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya  kuzalisha na kusindika bidhaa mbalimbali.

“Watu wamegundua kumbe wanaweza kuwa na viwanda vidogo na vya kati vya kusindika na kuzalisha, baadhi yao wameagiza hadi mashine za Dola 50,000 za Marekani.

“Tuombe na tuone wakishaanza kuzalisha waweze kujiunganisha na soko kwa sababu bado ni tatizo, hasa masoko ya nje. Naamini Serikali pamoja na kuwezesha na kuhamasisha viwanda, wasaidie kutengeneza masoko,” alisema Dk. Kimei.

Alisema hadi sasa CRDB ipo vizuri kwa sababu katika sekta ya viwanda inachukua asilimia 12 ya mikopo yao na hadi kufikia mwakani wanatarajia itafikia asilimia 24.

“Tumemtembelea Tanfoam hapa Arusha, wao wanataka kupanua kiwanda chao na kwa vile wana uzoefu tutawasaidia, ili waongeze uzalishaji na bahati nzuri wamepata masoko ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Tunaendesha biashara kwa kuangalia mwelekeo wa Serikali, ikisema inakwenda upande wa viwanda nasi lazima twende huko kwa sababu wakopaji wengi watakwenda eneo hilo.

“Lakini pia mnyororo huo hauishii kwenye viwanda, unakwenda hadi katika miundombinu, mfano ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge. Wapo wanaokopa ili kujenga viwanda kweye maeneo ambayo wanaamini reli

ikikamilika bidhaa zao zitafika kwa haraka bandarini na maeneo mengine kwa ajili ya kusafirishwa kwenye soko la nje,” alisema.

Kuhusu ukopaji kwa wafanyabiashara, alisema mtu yeyote anayeendesha biashara zake kwa kutegemea fedha zake bila kukopa hujikuta amedumaa na kuchelewa kupenyeza katika mafanikio aliyojipangia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Daqarro, alisema CRDB imekuwa chachu ya kusukuma uwekezaji na maendeleo katika nchi.

“Bila kukopa huwezi kutengeneza maisha na siku zote yataendelea kuwa magumu kwa upande wako.

“Ni vyema wananchi wakakopa ili kujikwamua kiuchumi, jambo la msingi unakopa kwa ajili ya kwenda kuzifanyia nini fedha hizo,” alisema Daqarro.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles