31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kalemani: GGM ijiandae kutumia umeme wa gridi

Na VERONICA SIMBA– GEITA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa mtambo wa kupoza umeme unaotarajiwa kujengwa Geita, kutawezesha Serikali kupeleka umeme wa gridi ya taifa katika mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mine (GGM) na kuondoa sababu ya wao kutokulipa kodi stahiki kwa Serikali kwa kigezo cha kutumia mafuta katika uzalishaji.

Akikagua eneo utakapojengwa mtambo huo juzi, Dk. Kalemani alisema mtambo huo utafua umeme wa megawati 100, hivyo pamoja na kuwanufaisha wananchi wa Geita na maeneo jirani, utatosheleza pia mahitaji ya mgodi husika ambayo ni takribani megawati 25.

“Ni matumaini yangu kufikia Desemba 2019 GGM watakuwa wameanza kutumia umeme wa gridi ya taifa ili waanze kulipa kodi stahiki kwa Serikali.

“Waache kupata msamaha wa kodi wanaopata sasa kutokana na kuingiza mafuta wanayotumia kuendeshea shughuli zao mgodini,” alisema.

Aidha Dk. Kalemani aliongeza kwamba kuwaunganisha GGM na umeme wa gridi kutakamilisha azma ya Serikali kuwaunganishia umeme wachimbaji wa madini wakubwa wote nchini kwani kwa sasa ni mgodi huo pekee uliobaki.

Aidha alimtaka Meneja Tanesco Mkoa wa Geita, Mhandisi Joackim Ruweta kuwapa taarifa uongozi wa mgodi huo ili waanze kufanya maandalizi ya kuupokea umeme kwenye miundombinu yao.

Kuhusu mradi wenyewe, Dk. Kalemani alieleza kuwa Serikali imetoa takribani Sh bilioni 23 kuujenga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa Geita na maeneo jirani na kwamba mradi unahusisha kusafirisha umeme mkubwa kutoka Bulyanhulu, umbali wa kilomita 55 hadi Geita.

Alisema taratibu zote za maandalizi zimekamilika hivyo akamtaka mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya CAMC Engineering ya China kuanza mara moja shughuli za ujenzi, ambao kwa mujibu wa mkataba utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 17.

“Pamoja na kuwa mkataba unabainisha muda wa kukamilisha ujenzi ni miezi 17, lakini tumekubaliana na mkandarasi ajitahidi kukamilisha ndani ya miezi 12,” alifafanua Dk. Kalemani.

Akizungumzia majukumu ya mkandarasi kwa mujibu wa mkataba, Dk. Kalemani alisema yanajumuisha ujenzi wa mtambo wenyewe wa kupoza umeme katika eneo la Mpomvu, nje kidogo ya mji wa Geita, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi eneo la mtambo, umbali wa kilomita 55 pamoja na kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji 11 vinavyopitiwa na mradi vikiwemo vya Nyantororo na Buyagu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles