25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru: Ukabila, udini havina nafasi UVCCM

Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema vitendo vya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, rushwa na kila jambo linalokwenda kinyume na katiba, kanuni na desturi nzuri, havina nafasi katika Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).

Kauli hiyo aliitoa jijini hapa jana wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza Kuu la UVCCM.

Pia alisema chama hicho kimeweka bayana msimamo na mwelekeo wake katika masuala ya kilimo, viwanda, ulinzi, usalama, sayansi na teknolojia katika mapambano ya kujikomboa kiuchumi na mwelekeo wa siasa za kidunia.

Alisema katika mazingira ya sasa ya kidunia mapambano ya kiuchumi yamejikita katika namna ambavyo nchi masikini zinasimamia ipasavyo sekta ya kilimo, uzalishaji wa kilimo wenye tija sambamba na viwanda vitakavyochakata bidhaa za kilimo na kujenga uwezo wa kuzalisha chakula, kujitosheleza ndani na ziada.

Pia alisema unyeti wa suala la ulinzi na usalama, vijana ndio walinzi wa mwanzo na wananchi kwa ujumla.

“Hivyo uzalendo, nidhamu, kufanya kazi, utii na kujitoa ni misingi muhimu kwa vijana wa CCM,” alisema.

“Jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi hazitapokewa vizuri na wasiotutakia mema na maadui walioko ndani na nje ya nchi.

 “Kwa mantiki hii, vijana wa ki-Tanzania wana jukumu la kuilinda nchi yetu, kutetea msimamo wetu na kuyasemea mazuri yanayofanywa na Serikali yetu,” alisema.

Kuhusu sayansi na teknolojia, alisema wigo wake ndio ulipo uwanja wa mapambano na ni muhimu kujihami mapema na kuwa tayari kukabiliana mashambulizi ya kimtandao, na wanaotumia mitandao kupotosha kazi nzuri inayofanywa na Serikali lazima wajibiwe kwa hoja na kwa ushahidi wakati wote.

Pia aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwapatia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka UVCCM aliye tayari kusimama imara kuulinda Muungano, kujenga umoja, kulinda uhuru, mtu mwenye msimamo usioyumba, atakayelinda heshima ya viongozi na anayeakisi maono na mwelekeo wa Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles