24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru: Siogopi kusema ukweli

Na ANDREW MSECHU

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Alli, amejibu mapigo kutokana na mjadala uliosababishwa na kauli yake akisema kuwa haogopi kusema ukweli.

Kutokana na hali hiyo, amesema hatasita kuzungumza ukweli katika mambo yaliyo wazi, ikiwamo suala la rushwa za mavazi na fedha katika uchaguzi.

Dk. Bashiru alitoa msimamo huo jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa simu, kuhusu mijadala ya watu mbalimbali inayoendelea kutokana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni.

Akiwa mjini Morogoro katika mkutano wa Mviwata, Dk. Bashiru aliibua mjadala kuhusu idadi ya wapiga kura kupungua kutokana na wananchi kukosa imani na mifumo ya uchaguzi na suala la vyama kutoa rushwa za mavazi na fedha na kununua kura.

Dk. Bashiru alisema kutoka na hali hiyo idadi ya wapigakura imezidi kupungua kwa sababu hivi sasa wananchi wengi wanaona uchaguzi ni kama kituko na maigizo.

Pamoja na hayo, Dk. Bashiru alisema kama kuna mtu anaona amekwazika kutokana na kauli yake  hiyo, ajitokeze hadharani.

Katika mahojiano hayo, Dk. Bashiru alisema moja ya sifa nne za kiongozi ni kusema ukweli na kuusimamia bila kujali kama atabezwa, atatukanwa, atakebehiwa au hata kufukuzwa kwenye chama na kwamba kiongozi anayeogopa au kupindisha ukweli, hana sifa ya kuongoza.

“Katika mjadala ule, watu wapime niliyoyasema yana ukweli kiasi gani. Mimi mwenyewe ninaamini niliyoyasema yana ukweli na siwezi kurekebisha msimamo wangu huo kwa sababu ninaanini nilisema ukweli.

“Lakini, hata kama unasema ukweli na kuusimamia, ukweli huo pia uutende kwa sababu mimi siwezi kuomba uongozi kwa rushwa. Kwa hiyo, nilitegemea watu wajitokeze waseme niliyoyasema hawayafanyi hayo, kuliko kuzunguka zunguka mbuyu.

“Ukweli usemwe hata kama ni mkali ili tujisahihishe, lakini kama sijasema ukweli, niko tayari kukosolewa na kukosolewa hakutatokea kwa kuzima mijadala au kupindisha mijadala na kuzua mambo ambayo hayako kwenye mjadala,” alisisitiza.

Alisema kwa nafasi yake kwenye chama ambayo ni kusimamia utekelezaji wa ilani na kuwavutia wanachama wengi kujiunga na chama chake, ataendelea kueleza msimamo wa chama, kwamba chama hakitakuwa na soko la kura kwa mujibu wa Katiba na ilani ya CCM.

“Vyote kwa pamoja, kwa maana ya ilani na Katiba, hakuna kinachokubali kuwa na soko la kura, yaani kwa ajili ya kuuza au kununua kura kama njugu.

“Ili kukabiliana na hayo, tayari nimeshapewa nyenzo, hivyo sitaripoti kwa yeyote katika chama, bali nitasimamia yale ninayoyaamini kupitia maelekezo ya Katiba na ilani ya chama.

Akizungumzia kuhusu mijadala inayoendelea kuhusu kauli yake ya mjini Morogoro, Dk. Bashiru alisema ameshazungumza na wamemsikiliza, hivyo ni zamu yake sasa kutumia mijadala hiyo kuwasikiliza.

“Sifa ya kwanza ya kiongozi ni usikivu, huwezi kuwa msikivu kwa kumshambulia mtu kwa matusi au kebehi. Lazima usikilize maoni ya mtu hata kama hukubaliani naye, ni jambo muhimu sana bila kujali ni nani.

“Sifa ya pili ya kiongozi ni kujifunza hata kwa njia ya mijadala pia, kuna mafunzo mengi kwenye mijadala hiyo na kwa waandishi wa habari pia ni muhimu kwenu kwa kuwa humo kuna shule ya demokrasia ambako mtapata jambo la kujifunza.

“Katika ripoti yangu ile, Gazeti la MTANZANIA liliripoti vizuri na nilizungmza mambo manne yaliyokuwa yakishabihisana, hivyo sikutarajia kwamba litachukuliwa jambo moja na mengine yakaachwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, katika maadhimisho ya mjini Morogoro, alizungumza katika mwelekeo wa wazalishaji wadogo na wakulima ambapo aliwataka wajenge uwezo wao wa kujua mambo, suala ambalo hajaona likijadiliwa.

“Sasa hapo nashangaa kwani wapo wanaoona masuala ya uwezo wa wakulima kujua wanyonyaji na wasiowanyoya, kuwajua wanasiasa wanaosema na kutenda, kuwajua wanasiasa wanaopenda vyeo na wanaopenda kutoa huduma, si muhimu.

“Siku ile nilieleza ardhi ni uhai, isiuzwe kama kofia na ikifanywa hivyo, tutakufa kama Taifa kwa kuwa ardhi ina uhai wa chakula, uhai wa ajira, uhai wa mapato na kila kitu.

“Lakini, sikuona mjadala kuhusu suala la ardhi kugeuzwa bidhaa, jambo ambalo lina uhai na zito zaidi kama alivyo Zitto mwenyewe. Kwa ujumla, nilitamani hata wanahabari waliokuwepo pale, watoe kipaumbele katika maeneo hayo.

“Katika hilo, tunaona watu wetu wananyang’anywa ardhi, wanapoteza ardhi, wanauza ardhi kiholela, viongozi wanalimbikiza ardhi na hawaitumii, wananchi wanakodishwa ardhi katika nchi yao na hakuna mjadala.

“Tujiulize katika hili suala la uwezo wa wakulima kujihami kwa kuwa na maarifa ya kujua mambo na kuwa kimya kuhusu umuhimu wa wakulima kuwa na ushirika ili walinde mifumo ya uzalishaji wao ili wasinyonywe na lumbesa.

“Hapo watu wako kimya, hakuna anayezungumza kuhusu ushirika, wote wamekuja kuparamia jambo la uchaguzi kwa sababu wote ni wapenda vyeo.

“Suala la nne nililozungumzia ni kuwataka wakulima wasigeuze kura zao kuwa bidhaa kwa sababu kura ina thamani na haina bei na kama ikiwa na bei, watu watadharau uchaguzi. Hapo utaona baadhi ya watu walibeba jambo ambalo wanadhani litanichonganisha na wana CCM wenzake.

“Ninaomba tusifanye mijadala kwa kuchonganishana bali kwa kujenga Taifa letu na Zitto ahangaike na chama chake, ajibu maswali, kwamba kwanini watu wake wanamkimbia, alikuwa na mwenyekiti wake (Anna Mghwira ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro) amemkimbia, alikuwa na Kitila (Kitila Mkumbo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji) amemkimbia.

“Kama kweli Zitto ni mjamaa na chama chake, inakuwaje mjamaa anaacha kujadili suala la ushirika, kwani hilo halimhusu.

“Suala la haki za wakulima kuhusu ardhi, si angelijadili huyo mjamaa, aache mambo ya kutafuta mijadala myepesimyepesi, mimi nilizungumza mambo manne kwa ujumla wake. Kwa hiyo, siwezi kulumbana na Zitto naye anajua, kwa sababu ana mbunge mmoja kwenye chama chake ambaye ni yeye mwenyewe wakati mimi nina mamia ya wabunge, Zitto si saizi yangu, naye anajua.

“Pamoja na hayo, naheshimu mawazo yake Zitto, lakini pia apanue mjadala aguse hata masuala yanayohusu chama chake anachokiita cha kijamaa kwa sababu suala la ardhi kwa chama cha kijamaa ni mjadala mkubwa kuliko hata uchaguzi na ushirika pia kwa chama cha kijamaa, ni mjadala mkubwa,” alisema Dk. Bashiru

Baada ya Dk. Bashiru kuyasema hayo akiwa mjini Morogoro, katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari, uliibuka mjadala ambapo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliandika katika mtandao wake wa twitter akisema “Siasa za nyimbo za mbele kwa mbele ni za CCM, sasa ni vyema Mwalimu Bashiru akaeleza hayo katika vikao vya kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama chake, asiishie kwenye Mviwata.

Pia Zitto aliandika, Upinzani umelalamika sana suala la rushwa kwenye uchaguzi, tuangalie hili suala la chaguzi za marudio. Wananchi wamechoshwa na siasa za hamahama ya wabunge na madiwani, hilo nalo Mwalimu Bashiru alizungumzie kwenye vikao vya CCM.

 

Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Waziri wa Zamani wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki ambaye aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema.

“Nimeyaelewa vizuri sana maelezo ya Dk. Bashiru kuhusu upigaji kura wa wananchi, uhalali wa Serikali, matamshi ya viongozi nk. Anao mtazamo mpana kuhusu chama chetu na Taifa letu. Maneno yale yale ningeyasema mimi, naamini baadhi ya wanachama wenzangu wasingeniacha salama,” alisema.

Naye Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wassira, aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema: “Hoja ya Dk Bashiru Ally kuhusu watu kujitokeza kwa uchache kupiga kura, uhalali wa Serikali inayochaguliwa, inahitaji utafiti na mjadala wa kina ili kuelewa kwa nini watu hawajitokezi kupiga kura na kiwango cha elimu ya uraia kabla ya kuhitimisha

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles