23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DIWANI CHADEMA ASIMAMISHWA KISA HAJUI KUSOMA, KUANDIKA

baraza-la-madiwani

Na RAYMOND MINJA – IRINGA

BARAZA la Madiwani la  Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, jana limemsimamisha Diwani wa Kata ya Boma, Julist Kisoma (Chadema) kutokuhudhuria vikao vya baraza  hilo  kwa tuhuma za kuidanganya Tume ya Uchaguzi na wananchi wake kuwa anajua kusoma na kuandika.

Kugundulika kwa diwani huyo kutokujua kusoma na kuandika, kulikuja baada ya kukacha kusoma taarifa ya kata yake mara tatu mfululizo, hali iliyoilazimu  kamati ya maadili ya baraza hilo kufanyia kazi tuhuma zilizokuwa zikimkabili za  kuidanganya Tume ya Taifa ya Uchanguzi  kuwa anajua kusoma na kuandika wakati si kweli.

Taarifa zilizoifikia MTANZANIA Jumapili na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Charles Makoga, zilisema kuwa diwani huyo amesimamishwa kutokuhudhuria vikao na shughuli zozote za kuwawakilisha wananchi hadi pale tume itakapotoa uamuzi juu yake.

Makogo alisema awali walisikia taarifa za diwani huyo kutokujua kusoma na kuandika, lakini walikuwa hawana uhakika nazo hadi walipokuja kupata shaka baada ya kukimbia mara tatu kusoma taarifa za kata yake.

“Unajua katika baraza letu tuna utaratibu wa kila robo mwaka madiwani huwa wanasoma taarifa ya kata zao, sasa mara ya kwanza aliomba udhuru akisema macho yake yanamsumbua, hivyo hawezi kusoma vizuri,” alisema.

Makoga alisema kuwa mara baada ya kupeleka tuhuma hizo kamati ya maadili ambayo ilimuita mhusika kumuhoji, alikiri kuwa hana uwezo wa kusoma mbali kwa kuwa ana matatizo ya macho na tayari daktari wake alishamwambia kuwa hatakuwa na uwezo kusoma vizuri.

Alisema kuwa mara baada ya tume hiyo kujiridhisha na kumaliza uchunguzi wao, aliombwa na kamati hiyo kuitisha kikao cha madiwani cha dharura kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo ili kuweza kujadili jambo hilo na ndipo walipofikia uamuzi wa kumsimamisha diwani huyo.

Makoga alisema kuwa ni kosa kisheria kwa mtu kudanganya kuhusu kiwango cha elimu aliyonayo, hasa akiwa kiongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles