DIAMOND, KIBA NANI MBABE AFRIMA 2017?

0
80

Na CHRISTOPHER MSEKENA

GUMZO kubwa kwenye tasnia ya muziki Afrika hivi sasa ni kile kinachoendelea nchini Nigeria ambapo tamasha kubwa lenye lengo ya kukuza muziki na tamaduni za Bara la Afrika linaendelea kurindima.

Tamasha hilo limeambatana na Tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA 2017) zinazotolewa kwa wasanii walioshinda katika vipengele mbalimbali, tukio linalochukua nafasi katika Ukumbi wa Host City, ndani ya hoteli ya Eko jijini Lagos.

Tukio hilo limeanza jana Ijumaa, leo ni siku ya pili  na tamati ni kesho ambapo tuzo hizo zitatolewa, huku wasanii kadhaa wa Bongo wakiongozwa na Diamond na Ali Kiba wakichuana na wenzao katika vipengele mbalimbali.

Tuzo hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya nne mfululizo zinazopewa shavu na Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) zimekuwa ni jukwaa kwa wasanii kufanya biashara na kutengeneza network ya kazi zao kwani huwahusisha mameneja, wasanii na wadau muhimu wa muziki na utamaduni huku likirushwa mubashara na vituo vya runinga 84.

Kama tunavyojua Bongo Fleva imeendelea kutikisa kwenye soko la muziki wa Afrika na safari hii mastaa kadhaa kutoka Tanzania wametajwa kuwania huku Harmonize, jana akiushangaza ulimwengu kwa kudondosha burudani kali sambamba na mastaa wengine zaidi ya 90 katika shoo ya ufunguzi iliyofanyika katika Kijiji cha Afrima Music.

Wasanii wa Bongo wataweza kutembeza mkong’oto kwa mastaa wengine na kuondoka na tuzo nyingi katika  vipengele wanavyowania?

Je, kati ya Diamond na Kiba ambao ndiyo wasanii vinara kwa sasa kwenye muziki wa Bongo Fleva, nani atamvimbishia mwenzake kifua? Ni suala na kusubiri na kuona lakini hapa chini cheki wababe kutoka Bongo ambao wanawania tuzo hizo katika vipengele tofauti.

KIBA, DIAMOND

Mahasimu hawa wapo kwenye vipengele kadhaa. Kipengele cha kwanza ni kile cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, cha pili ni Kolabo Bora ya Mwaka (Ali Kiba ft M.I- Aje) na (Jah Prayzah Ft Diamond-Watora Mari) na kipengele cha tatu ni Msanii Bora wa RnB & Soul ambavyo vyote hivyo wanashindana na wasanii kutoka nchi nyingine.

VANESSA, FEZA, NANDY, JIDE

Inaweza kuwa ni mara ya kwanza kwa wasanii wa kike kuingia kwa wingi kwenye tuzo kubwa kama AFRIMA. Safari hii Lady Jaydee amewaongoza wadogo zake kina Vanessa Mdee, Nandy na Feza Kessy ambao wanawania Tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki wakichuana na wenzao  kutoka Kenya, Uganda na Ethiopia.

DARASSA

Staa wa singo ya Muziki, Darassa ameingia kwenye tuzo  za AFRIMA katika kipengele cha Msanii Anayependwa na Mashabiki, yupo na wasanii kama Nyanshiski kutoka Kenya na wengine wa Afrika Kusini, Guinea, Nigeria, Namibia na Kongo.

MUZIKI WA ASILI

Msafiri Zawose ambaye ni mtoto wa mwasisi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, Dk Hukwe Zawose, ameendelea kupeperusha muziki wa Asili kutoka Tanzania katika anga la kimataifa baada ya kutajwa kuwania Tuzo ya Msanii Bora wa Muziki wa Asili.

Zawose ameingia kwenye tuzo hizo kupitia wimbo wake wa Asili Yangu ambapo katika kipengele hicho anashindana na wasanii kutoka Cameroon, Nigeria, Benin, Ethiopia, Niger na Zimbabwe.

FRENCH MONTANA

Staa wa singo ya Unforgettable, toka pande za Marekani, French Montana  anatarajia kuwa kivutio kikubwa mara baada ya  kutajwa kwenye tuzo za bara lake la asili kwa mara ya kwanza kwani mshkaji huyu ana asili ya Morocco.

Alizaliwa nchini huko na alihamia Marekani akiwa na miaka 13, hivi sasa ana miaka 33, ikiwa na maana kwamba ameishi Marekani kwa miaka 20 sasa.

AKON NDIYE MC

Mshehereshaji wa tukio la ugawaji wa tuzo hapo kesho ni msanii wa Marekani, Akon akishirikiana Sophy Aiida, staa wa filamu na muziki aliyezaliwa Ufaransa na kukulia Marekani kisha akarejea kwenye ardhi yake ya asili nchini Cameroon.

Dua zetu kwa mastaa hawa wa Bongo ili walete heshima kubwa nyumbani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here