26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DEREVA WA LISSU ASEMA HAYUKO SAWA

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

DEREVA aliyekuwa akimwendesha Tundu Lissu juzi wakati tukio la kupigwa risasi lilipomkuta, Adam, amesema hawezi kuzungumza chochote kwa sasa kutokana na kutokuwa sawa, baada ya bosi wake huyo kunusurika kifo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Adam alimwomba mwandishi wa habari hizi amwache kwanza hadi atakapokuwa sawasawa.

“Siko sawa, siwezi kuzungumza chochote kwa sasa, bado siko sawa,” alisema kwa kifupi.

Dereva huyo ndiye anayejua mbinu alizozitumia kumwokoa Lissu asipatwe na risasi nyingi zaidi.

Si hilo tu, ndiye mtu pekee anayeweza kuelezea kwa undani tukio alivyoliona na jinsi alivyoweza kunusurika risasi zaidi ya 20 zilizopigwa kwenye gari alilokuwamo pamoja na Lissu.

Iwapo angepatikana, pia angeweza kuelezea mazingira ya tukio lenyewe, iwapo kulikuwa na walinzi katika eneo hilo ambalo nyumba ya Lissu ipo jirani kabisa na ile ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, yenye askari wenye silaha nzito.

Adam iwapo angezungumza, angejibu pia maswali iwapo ana mafunzo yoyote juu ya mbinu za kujihami.

Dereva huyo angeweza kujibu maswali wanayojiuliza wengi iwapo kama anaweza kuwatambua wahusika wa tukio hilo, ambalo katika moja ya maelezo yake, alidai kuwa aliliona gari jeupe aina ya Nissan iliyokuwa ikiwafuatilia ambalo watu hao waliomjeruhi Lissu walikuwa ndani yake.

Angeweza kujibu pia ni watu wangapi walihusika kummiminia risasi Lissu na ndani ya gari pia walikuwa wangapi.

Juzi kiongozi mmoja wa Chadema alisema dereva huyo aliwaambia kuwa wakati wanatoka bungeni, waliliona gari hilo likiwafuatilia kwa nyuma, hivyo akalitilia shaka kwa sababu Lissu amekuwa akilalamika kwamba kuna watu wanamfuatilia.

“Kwa hiyo, alichokifanya ni kwamba, baada ya kukaribia kuingia nyumbani kwake, dereva alimshauri asiteremke kwenye gari ili ajiridhishe na usalama wa gari hilo.

“Wakati wanasubiri kuona mwisho wa hilo gari, mfyatuaji wa risasi alishuka kwenye gari hilo lililokuwa nyuma yao na kumimina risasi kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo na kisha akarudi kwenye gari na kuondoka,” alisema kiongozi huyo kwa kifupi, akikariri maelezo ya dereva huyo, ambaye alionekana pia hospitali akiwa amebeba nguo za Lissu zilizokuwa zimetapakaa damu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles