24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DEREVA THAMINI MAISHA YAKO, YA ABIRIA NA WENGINE

Na Reubeni Lumbagala

KWAKO Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania (IGP).

Nimeamua kuandika barua hii ikufikie kupitia gazeti makini la MTANZANIA. Nikiwa kama raia wa Tanzania na mdau wa usalama barabarani, nimeona nitoe mchango wangu wa mawazo katika kupambana na ajali za barabarani.

Nikiwa kama mwalimu wa somo la uraia na mdau wa masuala ya usalama barabarani, napendekeza kuanzishwa kwa kampeni ya kitaifa ya kupambana na ajali za barabarani itakayobeba ujumbe usemao ‘Dereva thamini maisha yako, ya abiria na wengine’.

Ajali nyingi za barabarani zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa madereva kwa ulevi na kutozingatia alama na sheria za barabarani. Naamini kampeni hii itasaidia kupunguza ajali za barabarani.

Kampeni hii iwaelimishe madereva na iwasisitize jinsi wanavyotegemewa na familia, ukoo, jamii na Taifa lao katika gurudumu la maendeleo. Kampeni iwaonyeshe jinsi ambavyo vifo vya madereva vinavyoleta simanzi kubwa na kuathiri maendeleo ya nchi. Hivyo, madereva daima wawapo katika vyombo vyao vya usafiri, waviendeshe kwa tahadhari kubwa wakijua kuwa kama ajali itatokea itakuwa na madhara makubwa kwa maisha yao, hivyo wathamini maisha yao kwa kuzingatia alama na sheria za barabarani katika kukomesha ajali.

Kampeni pia iwaelimishe madereva kuwa, kama ambavyo wanathamini maisha yao, basi pia wathamini maisha ya abiria waliowapakiza katika vyombo vyao vya moto. Madereva wazingatie kuwa wamebeba roho nyingi za abiria ambao wana matumaini ya kufika salama katika safari zao.

Hivyo, madereva waache uzembe na kuzingatia sheria zote za barabarani ili kuepusha ajali ambazo si tu kuwa zinasababisha vifo na ulemavu kwao lakini na abiria wao pia. Kampeni iwahamasishe madereva kuthamini maisha ya abiria wao ambao mara nyingi ajali zinapotokea zinakatisha maisha ya abiria wao wengi ambao ni nguzo muhimu kwa familia, ukoo na taifa lao katika harakati za maendeleo.

Kampeni iwasisitize madereva kuwa wathamini maisha ya wengine kama wapita njia na watembea kwa miguu, kwani nao wamekuwa ni wahanga wakubwa wa ajali za bararani. Kampeni iwaelimishe madereva kuwa ajali zinazotokea si tu kuwa zinaleta athari kwa maadereva na abiria, lakini pia ajali zimekuwa zikileta athari kwa wale ambao si wasafiri katika vyombo vya moto kama wapita njia na watembea kwa miguu.

Hivyo, upo umuhimu wa madereva kuthamini maisha ya wengine kwa kuhakikisha wanazingatia sheria zote za usalama barabarani ili kuokoa uhai wa wapita njia na watembea kwa miguu.

Kampeni ya ‘Dereva thamini maisha yako, ya abiria na wengine’, imelenga kuwajengea madereva hamasa kubwa ya kuzingatia sheria za usalama barabani kama njia ya kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikikatisha uhai wa madereva, abiria na wengine na kuacha majonzi kwa familia, ukoo, jamii na Taifa na kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo. Naamini kampeni hii italeta matokeo chanya katika kupunguza ajali za barabarani.

Kampeni ionyeshe namna ambavyo maendeleo ya Taifa lolote duniani linavyotegemea nguvukazi. Hivyo vifo vinavyosababishwa na ajali barabarani vinaathiri sana kasi ya ukuaji wa maendeleo. Madereva wasisitizwe jinsi ambavyo ajali za barabarani zinavyoweza kuepukika kama wao madereva wenyewe watatanguliza kuthamini maisha yao, ya abiria na wengine.

Kampeni ionyeshe kuwa dereva ambaye anathamini maisha yake kamwe hawezi kutumia kileo wakati akiendesha chombo cha moto. Hivyo, dereva anayetumia kileo hawezi kusema anathamini maisha yake na ya abiria na watumiaji wengine wa barabara kwani kwa kufanya hivyo, anahatarisha maisha yake na ya watu wengine. Kampeni iweke mkazo kuwa kuanzia sasa madereva watangulize thamani za maisha yao, ya abiria na ya watumiaji wengine wa barabara kwa kuepuka uzembe unaoleta madhara makubwa kwa vifo vya madereva na abiria.

Sambamba na kampeni hii kuwalenga sana madereva, lakini pia itoe elimu kwa abiria kuwa wasikae kimya pale wanapoona dereva anaendesha gari kwa mwendo kasi kupitiliza. Mwendo kasi kupitiliza unachangia ajali nyingi za barabarani.

Abiria wawapo katika vyombo vya usafiri waungane na wawe na sauti moja katika kumuamuru dereva kupunguza mwendo. Na kama dereva atakaidi amri ya abiria wake, basi abiria wapige simu Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya dereva wao.

Naamini kila dereva akizingatia thamani ya maisha yake, ya abiria na ya watumiaji wengine wa barabara, basi ajali ambazo zinatokana na uzembe wa madereva zitapungua kwa kiwango kikubwa sana.

Abiria nao wakisimama katika nafasi zao za kupinga uzembe wa madereva kwa kuwaripoti katika mamlaka husika, naamini matokeo chanya yatapatikana katika mapambano ya ajali za barabarani

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles