24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Demokrasia ni rafiki, chaguzi ndiyo adui

Na ALOYCE NDELEIO

IKIWA ni siku tatu tu zimepita tangu kufanyika kwa kumbukizi ya 19 tangu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki yapo mambo mawili ambayo ni muhimu kuyarejea kutokana na baadhi ya wanajamii hususani viongozi kwenda kinyume nayo.

Mwalimu aliyaweka wazi mambo hayo kuwa moja ni uongozi wa kueleza na la pili ni demokrasia katika kuamua mambo.

Alibainisha, “Maana uongozi sio kukemea watu; maana yake sio kuwatukana watu au kikundi cha watu usiokubaliana nao; wala maana yake sio kuamuru watu kutenda lile wala hili.

“Uongozi maana yake ni kuzungumza na kushauriana na watu ukawaeleza na kuwashawishi. Maana yake ni kuwa mmoja wao na kutambua kwamba wao ni sawa na wewe,”

Hoja inayoibuka ni kwamba Je, viongozi waliopo wanatambua kuwa maamuzi yao yanawaathiri na kwamba wamejieleza kwa wananchi hao kabla ya kufanya maamuzi yao? Je, wanaweza kudai kuwa wako sawa?

Mara nyingi wananchi wanaweza kuelezwa kwamba wamekuwa ni wasikilizaji na mara zote hujikuta wakipeperushwa na upepo ambao hawauelewi ni wa aina gani.

Kimsingi watu wote hawawezi kufanana katika uwanja wa siasa licha ya kwamba mwelekeo  unakuwa ni katika mabadiliko au maendeleo.

Hiyo inamaanisha kuwa kuwapo kwa upande  unaotekeleza  ni lazima uwepo  upande unaotoa msukumo ambao mara nyingi hukubalika au kupokelewa na hata kufanyiwa marekebisho.

Hapo ndipo suala la demokrasia huonekana kuchukua mkondo wake na kuonekana kuwa si adui wa watu.

Katika mdahalo wa kumbukizi hiyo mwaka huu ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Oktoba 12, wanataaluma na wanasiasa kadhaa walichangia mada iliyokuwa mezani ya ‘Mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika’.

Profesa  Musambayi Katumanga kutoka Nairobi, Kenya alisema kuwa nchi nyingi za Afrika zinatumia fedha nyingi kwenye chaguzi badala ya kutumia rasilimali hizo kunufaisha watu wake na akapendekeza kuwa  mataifa ya Afrika yaje na ajenda za kitaifa zitakazolenga kuwanufaisha watu wake na siyo katika kutafuta vyeo.

Alibainisha,”Uchaguzi kwa sasa imekuwa vita baina ya wanaotafuta madaraka na jamii ambayo inatafuta kiongozi, mara nyingi viongozi wetu wamekuwa wakipigana vita hii bila kujua kama wanakiuka miiko ya demokrasia,”

Kutokana na hali hiyo alifahamisha, “Demokrasia siyo adui wa watu wa Afrika lakini adui mkubwa wa Wafrika ni uchaguzi jambo ambalo limekuwa likileta migogoro na kuondoa uwezekano wa kujenga taifa imara,”

Hali hiyo kimsingi imanaanisha matokeo mengi ya chaguzi yamekuwa ni kama njia ya kudhoofisha misukumo au michango ya kuhimizana katika kuleta maendeleo na hivyo kusababisha hasara kuliko kuleta faida.

Katika mazingira yaliyopo hivi sasa  ya kujivua uanachama na kujiondoa katika nyadhifa ambazo zilipatikana kupitia kura za wananchi kumesababisha kuibuka kwa marudio ya chaguzi kwa nia ya kuziba nafasi hizo.

Hali hiyo ya kuhama  kidemokrasia inakubalika na inaonesha matumizi ya uhuru anaokuwa nao mtu ndani ya mfumo wa demokrasia yenyewe jambo haliwezi kupingwa.

Aidha katika kukubali kuwa matukio kama hayo ni ya kidemokrasia hata upande walikotoka  unakubali kwa hoja chanya inayosema, “Walioamua kuondoka waache waende tu, sisi tutabaki,”

Jambo ambalo limekuwa likifuatia baadaye limekuwa ni chaguzi hapa ndipo panapoonekana kuwa taswira ambayo si rahisi kueleweka kwa wananchi kwa sababu ya ile hoja ya Mwalimu  Nyerere ya kuzungumza na kukubaliana na wananchi.

Inasadifu kusema kuwa wakati walipokuwa wanaomba ridhaa ya kuchaguliwa wengi walijiweka karibu na wananchi kwa kuwaeleza na kuwashawishi na kukidhi ile maana ya uongozi ya kuwa mmoja wao na kutambua wananchi hao ni sawa na wao.

Matarajio ya wananchi ambao ndio wenye uchaguzi hujikuta wakiona kuwa walichokuwa wamekifanya hakikuwa na tija na kulazimika kurudia tena.

Kurudia jambo ambalo limeshafanyika ni hasara kwani huhitaji gharama. Wapo wanaoweza kuona kuwa hakuna hasara na ni kutekeleza masuala ya demokrasia.

Lakini kama rejea tu ni kurudiwa kwa mtihani wa darasa la saba kwa baadhi ya shule ambako kulibainika kuwapo udanganyifu, hilo lilielezwa wazi kuwa udanganyifu huo umesababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Hata hivyo rejea nyingine inaweza kuwa ni Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally aliposema kuwa chama hicho kimepata kura chache katika baadhi ya chaguzi ni dhihirisho kuwa wananchi wanaweza kuwa na dhana  kuwa yale yanayofanyika hayana tija kwao na hivyo kutojitokeza kupiga kura.

Mazingira hayo ndiyo yanafanya chaguzi ndio adui kwani wananchi wanakuwa wamepewa demokrasia ya mpito na kubakia kuwa wasikilizaji wa tambo za kisiasa, wakikodolea macho matumizi ya rasilimali bila kupata manufaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles