23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

DC MNYETI: DAU LA NASSARI NI KUBWA

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, amesema wana uwezo wa kuwanunua madiwani wote 20 wa Chadema ili halmashauri hiyo iendeshwe na CCM, na kwamba Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, naye kama anataka aende atanunuliwa kwa hela nyingi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mnyeti kuzungumzia  tuhuma zilizotolewa na Nassari na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa DC huyo amekuwa akinunua madiwani wa Chadema kwa Sh milioni mbili.

Jana akiwa katika Kata ya Sambasha iliyopo wilayani Arumeru, mara baada ya kumaliza kutatua mgogoro wa maji kati ya kata hiyo na Shamba la Miti la Meru, Mnyeti alisema: “Acha nijibu kidogo maana kuna vyombo vya habari hapa, msije mkanukuu vibaya, moja ni hili la madiwani kununuliwa, walionunuliwa inasemekana wako sita, bado hawajatosha.

“Nahitaji kununua 20, ili wawe 26, uchaguzi turudie kata zote, kwahiyo na wale ambao wanataka kununuliwa nao tunawakaribisha, fedha tunazo.

“Na tuko tayari kuwanunua, mwisho wa siku tunataka halmashauri yote iwe ya CCM, CCM hoyee. ‘Message sent’, uongo kweli? Kwa hiyo kama ni kununua, wacha niondoe hii habari ya kelele ndogondogo za pembeni, wanaotaka kununuliwa karibuni.

“Na yeye mbunge Nassari kama anataka kununuliwa, naye tunamkaribisha, kwa kuwa ni mbunge, eneo lake ni kubwa zaidi, basi yeye tutamnunua kwa hela nyingi zaidi, kwahiyo yeye kama yuko tayari basi aje tumnunue kwa fedha nyingi zaidi. Sambasha hoyee.”

Awali Diwani wa Kata hiyo, Lengai ole Sabaya (CCM), alisema kuna watu wanatengeneza filamu ya hovyo na kulalamika madiwani wao kununuliwa.

Alisema anashangaa Chadema kulalamika madiwani wao kununuliwa, jambo ambalo linawafananisha na bidhaa.

“Ni nani aliwaambia waende na bidhaa na kuwafanya madiwani badala ya kuwa na mtu? Madiwani ni watu, ukisema wamenunuliwa unawalinganisha na karanga au tikiti, wale ni watu wenye akili timamu, wameridhishwa na utendaji wa rais,” alisema.

Sabaya alisema kuwa madiwani wataendelea kuhama Chadema na kumwomba mkuu huyo wa wilaya kumchagua ili akasimamie uchaguzi mdogo katika kata hizo.

Oktoba Mosi mwaka huu, Nassari na Lema, waliweka hadharani ushahidi wa video unaoonyesha baadhi ya madiwani wao walivyokuwa wakishawishiwa kuhama Chadema na kujiunga na CCM.

Katika ushahidi huo, madiwani hao wanaonekana kwa nyakati tofauti wakizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mnyeti, Katibu Tawala wa Wilaya ya Meru, Timotheo Mzava na Mkurugenzi wa Halmashauri

ya Meru, Christopher Kazeri.

Video ya kwanza ya ushahidi huo iliyochukua dakika 30, inayoonekana kuchukuliwa Agosti 28, mwaka huu, Mzava anaonekana ofisini akizungumza na mmoja wa madiwani na mkurugenzi.

Diwani huyo anaomba kabla hajajiuzulu atekelezewe miradi miwili ya soko na barabara iliyopo kwenye kata yake.

Anasikika akisema: “Nia ya kuhama ninayo ila nina mashaka, na wengine wameshatangulia kuondoka, mimi ni wa tofauti na wenzangu.”

Katika video hiyo, inaonekana siku nyingine tofauti, diwani huyo akifanya mazungumzo na DC Mnyeti na DED Kazeri, akidai kwamba anaogopa asije kuingia mkenge wa kuhama bila kulipwa.

Baada ya Nassari na Lema kuzungumza na waandishi wa habari, walipeleka video hizo kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo inasema kwa sasa inaendelea na uchunguzi wa suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles