30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DALILI ZA MOYO, FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI ZATAJWA

VERONICA ROMWALD NA ABDALLAH NG’ANZI (TUDARCO) – DAR ES SALAAM

HALI ya tumbo na miguu kuvimba mara kwa mara, imetajwa kuwa ni miongoni mwa dalili za awali za moyo na figo kushindwa kufanya kazi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo, alisema hayo jana alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

“Watu wengi hawana mwamko wa kupima afya mara kwa mara… mtu anaona tumbo linavimba anadhani ni hali ya kawaida au miguu inavimba, anaendelea kukaa nyumbani bila kuchukua hatua ya kwenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi, hizi si dalili nzuri,” alisema.

Alisema kwa kawaida dalili hizo zinaashiria kwamba mtu ama ana tatizo kwenye moyo au figo zake, kwa hiyo ni muhimu kupima afya mara kwa mara.

“Aidha kuna uhusiano mkubwa mno kati ya tatizo la upungufu wa damu wa muda mrefu, moyo kushindwa kufanya kazi na figo, kitaalamu tatizo linaitwa Cardio Renal Anaemia Syndrome,” alisema.

Aliongeza: “Mtu anapokuwa na tatizo mojawapo linaweza kumsababishia tatizo jingine, moyo ukifeli unaweza kusababisha pia figo kufeli na hata kusababisha ukosefu wa damu katika baadhi ya viungo vya mwili.”

Alisema mtu ambaye moyo na figo zake zinashindwa kufanya kazi ipasavyo, anakuwa kwenye hatari zaidi ya kufariki dunia kuliko yule mwenye tatizo mojawapo kati ya hayo.

“Hapa JKCI tuliwahi kufanya utafiti kwa wagonjwa 463 ambao walilazwa wodini, asilimia 44.6 kati yao tulikuta wana tatizo hili (Cardio Renal Anaemia Syndrome), mara nyingi watu wenye tatizo hili huwa hatarini kupoteza maisha mara mbili hadi tatu ya wale ambao hawana tatizo,” alibainisha.

Dk. Pallangyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI, alisema kati ya wagonjwa hao ambao walifanyiwa utafiti, asilimia 55.4 walikutwa moyo peke yake umeshindwa kufanya kazi.

“Wagonjwa ambao moyo wao hufeli, hupungukiwa damu na kushindwa kukidhi mahitaji ya mwili, matokeo yake viungo muhimu hupokea damu chache kuliko kiwango kinachohitajika. Kwa mfano figo na hali hiyo husababisha nazo kufeli,” alifafanua.

Aliongeza: “Damu yote ya mwili kwa kila mzunguko mmoja hupita kwenye figo, kwa wastani binadamu ana damu kiasi cha lita tano hadi sita, moyo unapofeli hushindwa kupeleka damu kwenye figo na kwa kuwa figo ni kiungo cha mwili, hivyo kinapokosa damu ya kutosha nacho hushindwa kufanya kazi yake sawa sawa.”

Alitaja vitu vinavyosababisha tatizo hilo ni pamoja na ulaji usiofaa hasa vyakula vyenye mafuta na chumvi nyingi, uvutaji wa sigara, unywaji pombe kupitiliza na kutokufanya mazoezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles