25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

CUF wazidi kuparurana

Na Grace Shitundu, Dar es Salaam

JINAMIZI la mgogoro linaendelea kukitesa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya upande unaomuunga mkono Mwenyekiti wake anayetambulika na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kuanza kuparurana wenyewe kwa wenyewe katika uchaguzi wa viongozi wa Wilaya ya Kinondoni.

Kwa muda mrefu sasa CUF imekuwa na mgogoro uliowagawa katika makundi mawili ya wafuasi huku moja likimuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad na jingine linamuunga mkono Lipumba aliyejiengua mwaka 2015 katika nafasi yake na baadaye kurudi.

Wakati uchaguzi huo ukifanyika wilayani humo jana, wagombea saba walijitoa kwa madai kwamba katiba ya chama hicho imekiukwa kwa kumpitisha mgombea wa nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu ambaye hana vigezo.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wagombea wa uchaguzi huo, Idd Mkanga anayetokea Kata ya Kigogo, alisema anagombea nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho kwa kukidhi mchakato wote kuanzia ngazi ya tawi, kata na kisha kuingia wilayani.

“Katika nafasi ile tulijaza watu watatu ambao ni mimi, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Abdul Kambaya na mwingine anaitwa Akili Akili anayetokea Kata ya Bunju,” alisema.

Hata hivyo, alisema Kambaya kwa kutumia nafasi yake, hajapita mchakato wowote na katika orodha ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Kata ya Tandale hayupo.

“Sifa ya mjumbe wa mkutano mkuu kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 2 (a), inasema watachaguliwa wajumbe wawili na kati yao walau awepo mwanamke mmoja awe ni miongoni wajumbe hao wa kata.

“Sasa Kambaya amekuwa hana sifa ya kuwa mgombea na tumemuweka pingamizi kwa kufuata michakato yote lakini tumepuuzwa,” alisema.

Pia alisema kwa hali hiyo wanaona kuna baadhi ya wanachama hawafuati haki kama ambavyo wamekuwa wakisema na kudhani wako juu ya sheria.

Mwandishi wa habari hii alifika Ukumbi wa Shule ya Hazina uliopo Magomeni, Dar es Salaam ambako uchaguzi huo ulifanyika na kukuta unaendelea na alipozungumza na Msimamizi, Yusuph Mbungiro, alisema umekwenda kihalali.

“Uchaguzi huu ni wa halali na akidi ya wajumbe imetimia, walitakiwa 240 na waliofika katika uchaguzi ni 186,” alisema.

Pia alisema ni kweli kuna wagombea saba walijitoa akiwamo mwanamume na mwanamke katika nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu na wagombea watano wa kamati tendaji.

Kwa upande wake, Kambaya, alisema masharti ya kutokuchaguliwa ndani ya CUF yapo katika ibara ya 117 ambayo ni matatu.

“Moja ni ikiwa ulijiuzulu uanachama unatakiwa ukae miaka miwili pasipo kugombea, pili ikiwa ulifukuzwa uongozi pia unatakiwa ukae miaka miwili na tatu endapo ulifukuzwa uanachama.

“Sasa mimi sijafukuzwa uanachama, sijafukuzwa uongozi wala sijajiuzulu, wanaposema sina sifa ya kugombea kwa kufuata katiba gani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles